Home Kitaifa Kisarawe wajipanga kukabiliana na mabusha

Kisarawe wajipanga kukabiliana na mabusha

by Jamhuri

Watu 450 wilayani Kisarawe, mkoani Pwani wamefanyiwa upasuaji wa mabusha katika kambi maalumu iliyoendeshwa na madaktari bingwa wa upasuaji. 

Akizungumza na JAMHURI, Mganga Mkuu wa wilaya hiyo, Dk. Starford Mwakatage, anasema kuwa tatizo la mabusha wilyani humo ni kubwa na ndiyo maana wameamua kukabiliana nalo kwa kuweka kambi maaalumu za mara kwa mara. Anasema upasuaji huo haulipiwi na wale wenye matatizo.

Anasema ni vema watu wakawa na mazoea ya kufanya upasuaji haraka pindi wanapogundua kwamba wana uvimbe katika miili yao ili kukabiliana na matatizo hayo katika hatua za awali na kuepuka usumbufu baadaye.

Dk. Mwakatage anasema kuwa mabusha husababishwa na kuziba kwa mirija na kusababisha kujaa maji katika korodani au katika miguu au mikono na kusababisha matende.

“Wapo watu wanaamini kuwa tatizo hili husababishwa na kurogwa, hakuna uchawi wowote. Ni tatizo linalotokana na kuziba kwa mirija, hasa baada ya kung’atwa na aina fulani ya mbu ambao wanasambaza ugonjwa wa matende na mabusha,” anafafanua.

Dk. Mwakatage anasema pia kuwa mabusha ni ugonjwa tofauti na ngiri, ingawa kuna baadhi ya watu wanaamini kuwa magonjwa hayo yanahusiana.

Anasema ingawa ngiri huambatana na maumivu makali kwa mgonjwa, mabusha hayana maumivu yoyote, isipokuwa ni shida ya kutembea kwa mtu ambaye busha lake limekuwa kubwa kupita kiasi.

Anasema pamoja na mabusha, magonjwa mengine yanayowasumbua watu wazima katika wilaya hiyo ni shinikizo la damu na kisukari, ambayo husababishwa kwa kiasi kikubwa na tabia ya kula vyakula vyenye mafuta na wanga mwingi na kutofanya mazoezi mara kwa mara.

Anasema wamekuwa wakipambana na magonjwa hayo kwa kutoa elimu kwa jamii, kwani ni magonjwa ambayo mtu anaweza kujikinga nayo kiurahisi anapozingatia mfumo mzuri wa maisha na mlo.

Anasema wilaya hiyo inasumbuliwa sana na mabusha kwa sababu ya kuwa na mazingira yanayowawezesha mbu kuzaliana kwa kiasi kikubwa.

“Hivyo iwapo jamii zitahamasishwa kuwa na tabia ya kuharibu mazalia ya mbu upo uwezekano mkubwa tukaukabili ugonjwa huu kwa ufanisi mkubwa,” anasisitiza.

Kwa upande wa watoto, Dk. Mwakatage anasema wengi wanasumbuliwa na magonjwa makali ya njia ya hewa ambayo pia huwaathiri wazee. Anasema takwimu zinaonyesha kuwa kati ya asilimia 23 na 24 ya wagonjwa wote wanaopatiwa matibabu katika hospitali ya wilaya hiyo ni wale wanaougua magonjwa makali ya njia ya hewa.

Anasema mara nyingi watoto hukumbwa na magonjwa makali ya njia ya hewa kutokana na kutotunzwa vizuri kwa kuvalishwa mavazi ambayo yatawakinga dhidi ya baridi na unyevunyevu.

Anawataka wazazi na walezi kuhakikisha kuwa wanawaweka watoto katika mazingira ambayo yatawaepusha na maambukizo ya magonjwa hayo.

Pamoja na hayo, amehimiza wazazi na walezi kuhakikisha kuwa watoto wote chini ya umri wa miaka mitano wanapatiwa chanjo zote zinazohitajika, kwani ni muhimu katika kukabiliana na maambukizo mengi.

You may also like