Watu ambao wanapenda kushiriki mnada kwa njia ya mtandao utakaokuwa unaendeshwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ni lazima wawe na simu ya mkononi au kompyuta mpakato iliyounganishwa na intaneti.





Baadhi ya wakazi wa Dar es Salaam wakishiriki katika moja ya minada iliyoendeshwa na TRA kwa njia ya kawaida. Hivi sasa watu watakuwa wakishiriki minada hiyo kupitia mtandaoni.

Hayo yamebainishwa na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo. Anasema ni muhimu pia kwa mshiriki kuwa na Namba ya Utambulisho ya Mlipa Kodi, yaani TIN, na kama hana TIN atatakiwa kujisajili kupitia tovuti ya TRA ya www.tra.go.tz ili kupata TIN, kwanza akiweka anwani yake ya barua pepe na namba ya simu.

Anasema kuwa lazima mteja awe amejisajili kwenye tovuti ya TRA kupitia ukurasa wa mnada kwa kubonyeza sehemu iliyoandikwa Auctions (minada).

Anaongeza kuwa wakati wa kujisajili, mshiriki atahitajika kuhakiki kama jina alilojisajili limekwisha kutumiwa na mtu mwingine ama la.

Anasema kupitia tovuti hiyo, mtu yeyote anaweza kuona bidhaa zilizotangazwa kupitia mtandao hata kama hajajisajili.

Anaongeza kuwa baada ya kujisajili, mshiriki ataweza kushindana na washiriki wengine kwa kuweka bei na atakuwa na uwezo wa kuongeza bei kadiri ushindani utakavyokuwa ukiendelea.

“Mtu ambaye bei yake itashinda atapata ankara ya malipo ya awali ya asilimia 25 na ankara ya malipo ya kumalizia ya asilimia 75 kupitia mtandao na atakwenda benki kwa ajili ya kufanya malipo hayo,” anafafanua Kayombo.

Anasema mshindi atatakiwa kulipa asilimia 25 mara baada ya kupata ankara ya malipo wakati ankara nyingine ya malipo ya asilimia 75 atatakiwa kuilipa ndani ya saa 48, ingawa kwa chombo cha moto kama vile gari, pikipiki n.k, kutakuwa na ankara nyingine kwa ajili ya kulipia ada ya usajili.

Kayombo anasema baada ya kukamilisha malipo, mshindi atatakiwa kufika eneo la forodha ulipohifadhiwa mzigo ili akabidhiwe akiwa na uthibitisho wa kuonyesha kuwa yeye ndiye mnunuzi halali.

Kayombo anabainisha kuwa mnada wa kwanza kwa njia ya  mtandao ulifunguliwa Januari 2 na ulitarajiwa kukamilika jana. Washindi wa mnada huo watatangazwa leo kupitia tovuti ya TRA.

Kayombo anawakaribisha Watanzania wote ndani na nje ya nchi kushiriki kwenye mnada huo kwa njia ya mtandao ambao umerahisisha ununuzi wa vitu vinavyonadiwa na TRA.

Anasema kama ilivyo kawaida, wanunuzi wanaruhusiwa kukagua bidhaa zinazonadiwa siku mbili kabla ya tarehe ya mnada kwa watakaoweza kufika zilipo bidhaa hizo.

By Jamhuri