Klabu ya Rotari Dar es Salaam-Mzizima leo wamempa tuzo ya umahiri Prof. Mohamed Janabi, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili ikiwa ni ishara ya kutambua utendaji wake mahiri na mchango katika jamii hususani kwenye sekta ya afya.

Tuzo hii ni ya pili kutolewa tangu klabu hii kuanzishwa mwaka 1991 ambapo wa kwanza kupokea tuzo hiyo alikua Bw. Nehemia Mchechu mwaka 2012 akiwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ambaye naye alifanya mageuzi makubwa katika shirika hilo.

Akikabidhi tuzo kwa Prof. Janabi, Rais wa Klabu hiyo Bw. Ambrose Ntangeki Nshala amesema tuzo hii imetolewa kutokana na mchango wake kwa taifa na jamii siyo tu kuleta mabadiliko katika sekta ya afya katika kutoa huduma bora bali pia kutumia ujuzi wake, na muda wa ziada anaotumia kutoa elimu kwa jamii ili kujikinga na maradhi mbalimbali ikiwemo lishe bora.

Pamoja na mambo mengine, Prof. Janabi amepewa tuzo hiyo kutokana na mchango wake wa kufanya mageuzi makubwa katika utoaji wa huduma za afya alioufanya katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) alipokuwa Mkurugenzi Mtendaji tangu mwaka 2015 hadi Oktoba 2022 alipoteuliwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Kwa upande wake Prof. Janabi amewashukuru Klabu ya Rotari Dar es Salaam Mzizima kwa kumpa tuzo hiyo na kuongeza kuwa ni faraja kuona jamii inatambua mchango huo.

Ameongeza kuwa tuzo hiyo ni ishara na heshima kwa wafanyakazi wote wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Upanga na Mloganzila chini ya usimamizi wa Bodi ya Wadhamini ambao walikubali kubadilika na kuifanya MNH kuonekana hivyo ilivyo sasa.

Katika kipindi chake cha mwaka mmoja MNH, Prof. Janabi amefanya mageuzi makubwa ikiwemo kuimarisha hali ya utoaji huduma, kuongeza kasi ya uwajibikaji kwa wafanyakazi, kuanzisha huduma mpya, kuboresha mazingira na mandhari ya hospitali kwa ujumla wake pamoja na kuboresha mifumo ya utendaji katika kampasi zote za MNH yani Upanga na Mloganzila.