Serikali imesema itaendelea kutekeleza Sera yake ya kuunganisha mkoa kwa mkoa na wilaya kwa wilaya kwa barabara za lami ili kurahisisha usafiri na usafirishaji wa abiria, mazao na malighafi mbalimbali ili kukuza uchumi kwa haraka.

Akizungumza wilayani Kyela wakati wa utiaji saini mkataba wa ujenzi wa barabara ya Ibanda hadi Kajunjumele (KM 22), Kajunjumele hadi Kiwira Port (KM 6) na Kajunjumele hadi Itungi Port (KM 4) Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa  amesema kukamilika kwa barabara hizo kutaimarisha shughuli za kiuchumi kwa  wakazi wa wilaya za Rungwe na Kyela, na mikoa ya Ruvuma, Njombe na nchi jirani ya Malawi.

“Katika ukanda huu kuna malighafi na mazao ya kilimo,uvuvi na makaa ya mawe mengi yanayohitaji miundombinu rafiki kwa ajili ya kuwafikia watumiaji kwa wakati, ndio maana Serikali ya awamu ya sita imeamua kujenga barabara hizi kwa pamoja,’ amesema Waziri Prof. Mbarawa.

Waziri Prof. Mbarawa amewataka Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) kumsimamia vizuri  Mkandarasi anayejenga barabara hiyo ili azingatie viwango na thamani ya  fedha kulingana na mikataba.

Aidha, Waziri Prof. Mbarawa amewahakikishia wananchi wa Wilaya ya Kyela kuwa TANROADS itafanya uthamini upya ili kuhakikisha wananchi wanaopisha ujenzi wa barabara hizo wanapata stahili zao kwa mujibu wa sheria.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mhandisi Rogatus Mativila amesema Kampuni ya AVM Dillingham Construction International Incorporated ya Nchini Uturuki imeshinda zabuni ya kujenga barabara hiyo na inatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 24 kuanzia sasa.

Zaidi ya shilingi bilioni 38 fedha za ndani zinatarajiwa kutumika katika ujenzi huo ambao pia utahusisha taa za barabarani.

Mkuu wa mkoa wa Mbeya juma homera amewataka wananchi wa kyela kutumia fursa za ajira zitakazojitokeza wakati wa mradi huo kufanyakazi kwa bidii na uzalendo ili kuwezesha maradi huo kukamilika kwa wakati. Kwa upande wake Mbunge wa ileje ambae pia ni Naibu Waziri wa Ujenzi mhandisi Godfrey Kasekenya amesema ujenzi wa barabara wilayani kyela ni muendelezo wa mkakati wa serikali katika kuhakikisha barabara zote za nyanda za juu kusini zinazopiyta maeneo ya uzalishaji zinakuwa katika viwango bora na hivyo kutumika wakati wote na kuongeza tija kwa wananchi na taifa kwa ujumla

By Jamhuri