ARUSHA

Na Thomas Laiser 

Februari 10, 2021, Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda, alitangaza kufutwa maonyesho ya kilimo, maarufu kama Nanenane, ambayo yamekuwa yakifanyika kila mwaka.

Lengo la maonyesho hayo ni kutoa fursa kwa wakulima kujifunza mbinu za uzalishaji, kuwakutanisha na watoa huduma za kilimo, pia kufahamu na kupata fursa mbalimbali za masoko. 

Pamoja na tamko hilo la serikali la kufutwa maonyesho ya Nanenane, waziri alielekeza fedha zilizotengwa kwa ajili ya maonesho ya mwaka huu kutumika kuboresha huduma za ugani nchini. Alifafanua zaidi kuwa serikali itautumia mwaka huu wa kutofanyika maonyesho kwa kufanya tathmini kwa minajili ya kuyafanya maonyesho ya siku zijazo kuwa na tija.  

Pasipo shaka, kauli ya serikali ya kufuta maonyesho ya mwaka huu, pamoja na kwamba hatua hiyo ilistahili kuchukuliwa mapema zaidi, ni wazi kuwa inapaswa kupongezwa kwani suala la maonyesho hayo kupoteza mwelekeo na kutokuwa na tija tarajiwa kwa walengwa ambao wengi wao ni wakulima wadogo imekuwa ni kilio cha muda mrefu.

Tathmini aliyoagiza waziri kufanyika itafaa ikaja na suluhisho la changamoto ya viwanja vya maonyesho kugeuka ‘magulio ya biashara’ badala ya maonyesho ya kilimo. 

Viwanja vya maonyesho kama vile vya Julius Nyerere kwa Kanda ya Mashariki, Themi (Kaskazini) vya kanda nyinginezo, kwa kiasi kikubwa vimegeuka miliki ya mashirika, kampuni na watu binafsi ambao wengi miongoni mwao wanafanya shughulizi zisizo na uhusiano wa moja kwa moja au pengine kutohusiana kabisa na kilimo, huku wakulima na vyama vyao wakiwa wametengewa maeneo madogo ya pembezoni au pengine wakiishia kujibanza kwenye viambaza vya ‘wanene hao’ ili kuonyesha shughuli zao za kilimo. 

Ushiriki duni wa walengwa umebainisha kasoro kubwa ya kile kilichokuwa kinaendelea kuitwa ‘maonyesho ya kilimo ya Nanenane’. Licha ya ukweli kuwa wakulima ndio walengwa wakuu wa maadhimisho haya, mamlaka zinazosimamia hazikuweka mipango thabiti ya kuhakikisha ushiriki wao. Bila shaka jambo hilo litatazamwa kwa umakini katika kipindi hiki cha mpito na maboresho. 

Kama hiyo haitoshi, wakulima wamejikuta wakiporwa maonyesho hayo na nafasi yao kuchukuliwa na watumishi wa serikali. 

Nafasi ya wataalamu katika mabanda ya maonyesho inafahamika na umuhimu wake kwani wanakuwapo kwa ajili ya kutoa ufafanuzi wa masuala ya kitaalamu. 

Lakini haiingii akilini kukuta takriban asilimia 75 ya washiriki kwenye banda wakiwa ni watumishi wa serikali ilhali wakulima wakiwa asilimia ndogo iliyobaki. 

Suala hilo litafaa kutazamwa vema kwani tunaamini watumishi wanayo matukio mengi ya kushiriki ikiwamo Mei Mosi, siku ya TAMISEMI na nyinginezo ambazo wakulima hawana nafasi. Ni vema basi watumishi wa serikali nao watoe nafasi ya wakulima kuwapo kwa wingi kwenye maonyesho ya kilimo. 

Wakati Waziri wa Kilimo ameelekeza mwaka huu kuwa wa kufanya tathmini, ni vema watakaopewa dhamana ya kutafakari hayo wakatazama pia suala la gharama za ushiriki wa maonesho kwa kuanza na viingilio vinavyotozwa milangoni mpaka zile wanazotozwa washiriki wa maonesho yenyewe. 

Kasoro kubwa iliyokuwapo ni ile ya kuyachukulia maonyesho kama chanzo cha mapato kuliko sehemu ya kukuza maarifa ya uzalishaji na kusaidia kuwaunganisha wakulima na masoko na wadau wengine walio katika mnyororo wa thamani. 

Mamlaka husika zinapaswa kutazama na kuyachukulia maonesho hayo kama huduma zaidi kuliko biashara.

Ni vema pia tathmini itakayofanyika ikaangazia kuona ni vipi maonyesho ya Nanenane kwa nyakati zijazo yatarejea misingi yake ya awali kwa kuhakikisha kuwa yanaadhimishwa vijijini na kwenye miji ya wilaya waliko wakulima, tofauti na ilivyo sasa ambapo maonyesho hufanyikia mijini. 

Kufanya hivyo kutatoa nafasi ya maonyesho kuakisi uhalisia kwa wakulima kujifunza kwenye mashamba-darasa yaliyo kwenye mazingira yao badala ya bustani za mazao zilizoandaliwa kwa ustadi na gharama kubwa isiyo akisi uhalisia. 

Mwisho, kwa serikali kubaini kuwa dhana nzima ya maonyesho ya Nanenane imeendelea kupoteza maana, kipindi hiki kitakuwa ni muda sahihi kutazamwa upya kwa vigezo vinavyotumika kuchagua washindi wa maonyesho katika makundi mbalimbali. 

Katika kufanya hilo, ubunifu unaojibu mahitaji na changamoto za wakulima kiteknolojia, kiuchumi na kijamii uwe msingi katika uoanishaji wa vigezo hivyo.  

Mwandishi wa makala hii ni Mhamasishaji Jamii-Mtandao wa Vikundi vya Wakulima na Wafugaji Mkoa wa Arusha.

0763-102883  

By Jamhuri