Yah: Nyuma ya pazia ni vilio tupu, lakini tuna furaha

Naomba niwasalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ninyi muitikie kwa sauti kubwa: “Kazi iendelee” huku mkijipiga vifua mara tatu. 

Tangu wiki jana naugulia maumivu ambayo ninadhani nikishayazoea nitaanza kushangilia badala ya kububujikwa machozi.

Leo ni wiki moja tangu tuanze kujua jinsi ambavyo kodi inachukuliwa mbele ya macho yako na unaiona. Siye ambao mara nyingi tunatumiwa fedha na wanetu pamoja na ya kutolea tumeona jinsi ambavyo maumivu ya mtumaji yanavyokuwa. Ukitumiwa muamala mdogo wa kati unaweza kuona kilichokatwa kinatosha kupata debe moja la sembe.

Najua inawezekana likawa jambo dogo la kupita na likarekebishwa ua tukazoea tukaliacha lakini naanza kuona namna ambavyo kwa namna moja ama nyingine linavyoweza kuwakutanisha watu au kupunguza misaada kwa watu kama siye akina kwangu pakavu.

Leo yule aliyekuwa akinitumia shilingi elfu kumi ya mafuta ya taa ana changamoto kubwa sana, kwanza kuna nyongeza ya bei ya mafuta japo si ya taa, lakini ya kutumia katika chombo cha  kusafiria kwenda katika kituo cha mafuta, bodaboda wamepandisha bei ghafla, hawa hawana mtu wa kuwadhibiti masuala ya nauli.

Ninapokwenda kwa wakala kwa nia ya kuchukua kilicho changu sasa kimepungua huku nikipewa manung’uniko mengi kutoka kwa mtumaji kwamba naye anakatwa mtumo mmoja maradufu, naona jinsi ambavyo ninapokea kiasi kidogo na kupata mafuta kidogo, inanilazimu nichague siku za kuwasha kandili ili nimalize wiki moja.

Nimeamua kuandika waraka huu ili niwape kwa ufupi tu kile ambacho kinanichanganya kwa sasa japo ninajua kuwa naongeza mapato kwa taifa langu, mapato ambayo yatajenga barabara, shule, zahanati na hospitali, nayaona mapato ambayo yataimarisha huduma za jamii na dawa kwa wagonjwa.

Pamoja na kuyaona yote hayo, lazima nikiri kuwa ninaona jinsi ambavyo baadhi ya huduma zitakapoongezeka, ukiritimba na kutupotezea  muda wa kufanya kazi zingine, naona jinsi ambavyo watu wataanza kutumia huduma za moja kwa moja benki na hali itarudia kama zamani.

Naona jinsi ambavyo sisi watumiaji wa simu za mikononi tutakavyokuwa makini na baadhi ya matumizi kama kutumia simu katika miamala hata ile ya kuwasaidia wenye matatizo, naona jinsi ambavyo teknolojia inavyokuwa na gharama zaidi na jinsi ambavyo tutakaa pembeni wakati dunia inakimbia.

Kodi kwa mwananchi ni lazima kabisa na hata vitabu vitakatifu vyote vimetaja umuhimu wa kulipa kodi, tena kwenye mamlaka, kwa maana ya serikali, jambo la kujifunza hapa ni namna ambavyo tunaweza kuchagua maeneo ambayo tunaweza kudai na kuchukua kodi.

Wakati fulani nilipokuwa katika ndoto zangu niliyaona maeneo ambayo hatukupaswa kudai kodi kwa maana ya kuinua hali ya kipato cha taifa, niliona pembejeo za kilimo na kila kitu kihusucho kilimo, niliona umuhimu wa kuimaarisha mfumo wa teknolojia lakini pia huduma za jamii kwa ujumla wake, hasa zinazolenga mahitaji muhimu zingelegezewa kamba ya kodi.

Niliona nafasi ya kodi katika vitu vingi vya anasa ambavyo tunaweza kuchangia kodi vizuri kama vile pombe, magari ya kifahari, vyakula kutoka nje,  nguo na kadhalika, pia niliona makosa mengi  ya raia yanayogharimu maisha ya Watanzania, iwe kwa mahitaji binafsi au kwa kutumia kitu kama magari, pikipiki na mengineyo.

Niliona fursa ya kupata kodi kupitia bidhaa za ndani zinazouzwa nje lakini baada ya kuwawezesha wakulima wa ndani kujitosheleza kuzalisha,  niliona fursa ya kuweka ruzuku katika kilimo, ufugaji na uvuvi kama sehemu ya kujikwamua kiuchumi kwa taifa na mtu mmoja mmoja na kisha kuongeza ajira ambayo ingevuna kodi kupitia ajira.

Niliona fursa ya uwekezaji katika kuongeza tija ya ajira na kodi, kuongeza kodi kutoka kwa wenye mitaji na kuwasaidia maskini wenye nchi. 

Niliona fursa ya kufufua viwanda na mashamba yetu ambayo tulikuwa nayo miaka ya sabini na huo kuwa mwanzo wa kufufua uchumi wetu, nyuma ya pazia ni vilio tupu lakini tuna furaha.

Najua nimepitwa na mengi lakini sina hakika nayo, sijui kama kuna ukweli kwamba bei ya mafuta imepanda. Na iwapo imepanda sina hakika kama suala la nauli litaendelea kuwa himilivu kwa bei hiyohiyo kwa muda wote, hili ngoja nifanye uchunguzi kwa kupiga simu mjini kabla ya tozo la simu ya kuongea halijaanza.