Na Bashir Yakub

Maombi au kesi inaweza kutupwa na mahakama kwa namna moja kati ya mbili.

Inaweza kutupwa katika namna ambayo huwezi kuirudisha tena/kuifungua upya, au inaweza kutupwa katika namna ambayo unaweza kuirudisha tena/kuifungua upya.

Kutupwa katika namna ambayo unaweza kuirudisha tena kitaalamu huitwa ‘STRIKE OUT’,  wakati ile ambayo huwezi kuirudisha tena huitwa ‘DISMISSAL’.

Kesi ya kina Mdee imetupwa katika namna ambayo inaweza kurudishwa tena/kufunguliwa upya (STRIKE OUT). 

STRIKE OUT maana yake kuna kitu kimekosewa ambacho kikirekebishwa kesi inarudishwa/kufunguliwa upya.  

Maana yake kesi ya msingi ya uhalali wao bungeni haikusikilizwa hata kidogo, bali mahakama imesikiliza makosa ya kiufundi na ikaamua iitupe kabla ya kusikiliza kesi ya msingi ili wahusika wakayarekebishe hayo makosa wairudishe tena au waachane nayo, uamuzi ni wao (tayari wameirudisha).

Aghalabu, namna ya kuirudisha ni kuwa kama umejiandaa inaweza kutupwa na muda huo huo hata kabla watu hawajatoka mahakamani au wakingali bado wanashangilia ukairudisha kwa kufungua nyingine hapo hapo! 

Ni kurekebisha tu makosa na kuanza upya.

Isipokuwa yale mazuio unayokuwa umepata yanakufa na ile iliyotupwa, hivyo huu muda wa katikati ambao haujafungua nyingine unakuwa haupo salama, kwa kuwa hauna zuio lolote linalokulinda, hivyo lolote linaweza kufanyika dhidi yako.

Lakufanya ni kufungua upya haraka na uombe zuio jingine jipya haraka kabla haujapata madhara ya kutokuwa na zuio.

Kwa msingi huu si ajabu kusikia kesi hii iko mahakamani upya hata kesho asubuhi kabla ya ‘swalaa’.

Basi waandishi watusaidie kuwa wanaripoti ilivyo fasaha.