Dar es Salaam

Na Mwalimu Samson Sombi

Maendeleo makubwa ya nchi pamoja na mambo mengine hutokana na maono na msimamo wa kiongozi mkuu wa nchi. 

Aidha, maendeleo ya nchi huwa na hatua kuu nne ambazo ni mipango, mikakati ya utekelezaji wa mipango, usimamizi na upimaji wa utekelezaji wa mipango hiyo.

Kiongozi ni lazima awe na maono mapana yanayoakisi malengo  na dira  ya nchi  anayoiongoza, awe na ujasiri wa kuthubutu kufanya uamuzi wenye masilahi mapana ya taifa.

Mshahiri na mwandishi wa riwaya wa Marekani, Marge Piercy, aliwahi kusema: “Mwanamke shupavu ni yule anayetaka kufanya yale ambayo  wengine wanadhani hayawezekani.”

Rais Samia Suluhu Hassan tangu aingie madarakani Machi 19, 2021 amekuwa na msisitizo mkubwa sana juu ya nchi kujitegemea kiuchumi huku akiweka bayana nia yake ya kuboresha mazingira ya biashara  na uwekezaji kama hatua pekee ya kukuza uchumi wa nchi.

Aprili, 2021, Rais Samia alihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa mara ya kwanza tangu aingie madarakani na kueleza mikakati na dira ya serikali yake.

Pamoja na mikakati mingine alieleza mwelekeo kwamba utakuwa ni kurudisha imani na kutoa  vivutio kwa wawekezaji na wafanyabiashara, ikiwamo kuwezesha uwekezaji kufanyika kwa haraka na kwa mazingira tulivu na salama.

“Nchi yetu imekuwa na changamoto ya kutokuwapo kwa mazingira  mazuri ya biashara na uwekezaji, ikiwamo kutokuwa na sera zinazotabirika, urasimu unaokwamisha ustawi wa biashara na uwekezaji. Serikali ya Awamu ya Sita inakusudia kufanya marekebisho makubwa,” anasema Rais Samia.

Katika hatua nyingine, Aprili 6, mwaka 2021 Rais Samia alieleza  umuhimu wa uwazi na mazingira bora kwa uwekezaji na biashara  hapa nchini, huku akiwataka viongozi  wahusika kufanya kazi kwa weledi na uzalendo mkubwa.

“Anakuja mwekezaji anawekeza pesa zake, anafungua  Insurance Company (Kampuni ya Bima) kubwa, anakuja  na wataalamu wake pengine wawili.

“Wataalamu wamefika, miaka mitatu anaomba tena kibali  cha kazi. Ahaa! Weka Watanzania! Huu ni mradi wake mwenyewe, anatia Sh 1 akijua itazaa 1.5. Kwa nini umlazimishe aweke  mtu ambaye hamtaki?”anahoji Rais.

Rais anawataka wanaosimamia uwekezaji  wajenge  mazingira bora ya uwekezaji.

“Makampuni yanafungwa ndugu zangu si uongo, yanafungwa na wanaondoka, yakiondoka uchumi wetu unapungua, ajira zinapungua, na hicho ndicho kilio chetu Watanzania, mifuko inabaki mitupu,” anasema Rais.

Akikumbushia  hotuba yake bungeni, Rais anasema: “Juzi tu nilitoa kauli ya kodi,  wawekezaji  wengi wanampigia katibu wangu na wasaidizi wangu – mwambie Rais tunataka kumwona aje atuhakikishie, tunataka kuja Tanzania. Kwa hiyo  watu wanataka kuja Tanzania. Naomba tuvute wawekezaji, tupate ajira, fedha izunguke, uchumi ukue.”

Akiwa katika ziara ya kikazi nchini Kenya  Mei, 2021, Rais Samia alimweleza Rais wa nchi hiyo  Uhuru Kenyatta kwamba Kenya ni mdau mkubwa  wa biashara na uwekezaji Tanzania, na kwamba  wanapaswa kuboresha  mazingira kwa ufanisi zaidi.

“Kwa mfano wakati  wa mazungumzo  yetu nimemwarifu Rais Kenyatta  kuwa Kenya inashika nafasi ya tano kwa uwekezaji nchini Tanzania kiulimwengu lakini kwa nchi za Afrika Mashariki inashika nafasi ya kwanza,” anaeleza Rais Samia.

Katika hatua nyingine, Rais Samia anasema  kwa lengo  la kukuza  biashara  na uwekezaji “tumekubaliana kuendelea kufanyia kazi changamoto hususan vikwazo visivyo vya kodi, hivyo sasa viondoke  na tumekubaliana kuwa tume yetu ya ushirikiano iwe inakaa kutoa suluhu  ya vikwazo vinavyojitokeza.”

Moja ya maeneo ambayo ni lango kuu  la biashara na uchumi wa nchi ni bandari. Nchi yetu ni miongoni  mwa nchi za Afrika Mashariki zenye bandari nyingi, kubwa na bora ambazo ni mtaji mkubwa sana katika  kukuza  uchumi  na kuongeza pato la taifa.

Akizungumza na wajumbe wa Baraza Kuu la Taifa la Biashara (TENC) jijini Dar es Salaam Juni 26, 2021,

Rais Samia Suluhu Hassan anasema wameanza mazungumzo ya kufufua mradi wa Bandari ya Bagamoyo pamoja na ule wa chuma na makaa ya mawe wa Mchuchuma na Liganga.

Akizungumzia mradi huo wa Bandari ya Bagamoyo, Balozi wa China  hapa nchini, Chen Mingjian, anaipongeza  serikali ya Tanzania kwa kuboresha mazingira ya uwekezaji.

“Nimejifunza kuwa Serkali ya Tanzania  imefanya  marekebisho  ya sheria  ya uwekezaji na kukuza uwekezaji, mamlaka hizo zinawezesha  kupunguzwa kwa gharama za kufanya biashara ikiwamo kupunguza kodi na mchakato wa kufanya kazi,” anasema Mingjian.

Katika hatua za kuimarisha  diplomasia ya uchumi, Aprili 22, mwaka huu Tanzania imesaini mikataba saba  ya biashara na kampuni za marekani  yenye thamani ya  Sh trilioni 11.7 inayotarajiwa kuzalisha  ajira 301,110 katika sekta  ya kilimo, utalii na biashara.

Mbali na mikataba hiyo, Rais Samia  alishuhudia utiaji saini wa hati  za makubaliano kwa ajili ya  kuanza  mazungumzo  ya uwekezaji na biashara kati ya kampuni za Marekani na Tanzania.

Katika hatua nyingine, Rais Samia aliyaomba  mashirika ya kimataifa kuzisaidia nchi zinazoendelea  kutumia nishati ya kijani.

Aliomba hayo alipozungumza na Rais wa Benki ya Dunia, David Malpass, kwamba hilo litasaidia kuepuka uharibifu wa mazingira.

“Mashirika ya kimataifa yanakuja na teknolojia mpya kila siku yanatuambia tutumie nishati ya kijani, yanapaswa kuangalia hali tulizonazo. Afrika tunaweza katika gesi, umemejua na upepo, lakini  tunahitaji msaada  kukusanya nishati kutoka vyanzo hivyo,” anasema Rais Samia.

Rais Samia  ameendelea kuimarisha  uhusiano mwema  na nchi  wanachama wa Afrika Mashariki  na kukaribisha wawekezaji wa nchi hizo kuja kuwekeza Tanzania kwa masilahi mapana ya Tanzania na nchi hizo.

Mei 10, mwaka huu Rais Samia alifanya  ziara ya siku mbili ya kitaifa  nchini Uganda, ikiwa ni  ziara yake ya kwanza tangu  alipoingia madarakani.

Katika ziara hiyo Tanzania  na Uganda zimesaini  mikataba miwili ya makubaliano kuhusu ulinzi wa nishati, huku  Rais  Samia akiwakaribisha wawekezaji  kutoka Uganda  kuwekeza nchini.

Rais Samia alisema wamefanya  majadiliano na mwenyeji  wake Rais Museveni  katika  masuala  mbalimbali ikiwamo nishati, biashara, usafiri, maendeleo ya miundombinu, afya, utulivu wa kisiasa  na  usalama, lengo  likiwa ni kuimarisha uchumi wa nchi hizo.

Rais amewaalika  pia wafanyabiashara wa Oman  kuja kuwekeza nchini Tanzania  huku akiwahakikishia mazingira mazuri ya uwekezaji na uwepo wa nguvukazi ya  kutosha.

Katika ziara  yake ya siku  tatu  nchini  Oman Juni 12, mwaka huu Rais Samia alisema hayo  wakati  akishiriki  kongamano  la wafanyabiashara  nchini  Oman na kwamba endapo Oman itatumia fursa ya kuwekeza  nchini itanufaika na soko  kubwa ambalo Tanzania  inaweza kulifikia.

“Sisi ni wanachama  wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Pia ni  wanachama wa SADC ambao kwa pamoja  tunatengeneza idadi  ya watu karibu milioni  500, ambalo ni soko kubwa.

“Pia wanachama wa  soko huru la Afrika (ACFTA). Hili linaongeza idadi  ya watu na kufanya soko la watu  kuwa bilioni 1.3,” anasema Rais Samia.

Rais Samia alieleza kuhusu fursa za uwekezaji Tanzania  ikiwamo kilimo, mifugo, uvuvi, madini, utalii, uzalishaji, teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) na maendeleo ya miundombinu.

Kwa upande wake Waziri wa Biashara, Viwanda na Uwekezaji wa Oman, Qais bin Mohammed Al-Yousef, anasema wako tayari kujadili ni kwa namna gani wanaweza kushirikiana na kuendeleza  fursa hizo ambazo Tanzania imezitaja.

“Pia tuko tayari  kuangalia  namna tunavyoweza  kuimarisha biashara, uwekezaj  na kuongeza ushirikiano  wa kiuchumi kwa manufaa ya watu wa nchi zote  mbili, hususan katika  maeneo  ya kilimo, uvuvi, viwanda, madini na utalii kama yalivyotajwa na Rais Samia,” anasema Al-Yousef.

Ofisa Uvuvi Mwandamizi Mkoa wa Geita, Tito Mlelwa, anasema Rais Samia amefanikiwa  kujenga diplomasia ya kiuchumi na kuvuta wawekezaji wengi kuja kuwekeza Tanzania kwa kipindi kifupi.

“Ziara za Rais Samia kimataifa zinajenga diplomasia ya kiuchumi na kuwahakikishia wawekezaji hali ya usalama  na amani iliyopo Tanzania. Wawekezaji wanahitaji mazingira  mazuri, usalama wao pamoja na fedha zao,” anabainisha Mlelwa.

Kwa upande wake mfuatiliaji wa masuala ya siasa na kijamii, Hashini Yahya wa Masika, Manispaa ya Morogoro, anasema vijana wanapaswa kuchangamkia fursa zinazopatikana katika uwekezaji na kumpongeza Rais Samia kwa jitihada za kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.

Na Mwalimu Samson Sombi.

0755-985966

Please follow and like us:
Pin Share