Mheshimiwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa. Mimi ni miongoni mwa Watanzania wengi waliokupongeza kwa kuteuliwa kwa mara nyingine kuwa waziri mkuu baada ya msiba mzito wa Rais wetu mpendwa, Dk. John Magufuli, Machi mwaka jana.

 Hii haikuwa bahati tu kuendelea kuwa kiongozi mkuu katika utendaji wa serikali, bali historia yako ya utendaji  ndiyo iliyokubeba.

 Watanzania wengi, kama si wote wanaupenda utendaji wako bora na uliotukuka na kwa sababu hiyo sitapoteza muda kueleza kuhusu usimamizi wako mwema. 

Ila leo naomba uchukue muda mfupi kupokea ushauri wangu kwa serikali yetu ambayo wewe na Rais Samia Suluhu Hassan mnaisimamia vema, na kwa sababu wewe ni miongozi wa viongozi wachache wanaopenda michezo, hasa mpira wa miguu, naomba uniruhusu niifananishe serikali yako na timu ya mpira wa miguu.

Mheshimiwa Waziri Mkuu, timu yoyote bora lazima iwe na sifa  katika vitengo vifuatavyo: Iwe na kocha bora; benchi bora la ufundi na wachezaji bora.

Wachezaji hawa hugawanywa katika sehemu tatu; mabeki bora, viungo bora na washambuliaji bora.

Mheshimwa Waziri Mkuu, kocha tuliyenaye, Mama Samia, ni bora na Watanzania wote tunamjua vema anavyo ‘upiga mwingi’ katika kutuletea maendeleo ya haraka. 

Wewe na yeye pia ndio washambuliaji katika serikali yetu. Nikiri kuwa kazi yenu tunaiona vema, tunawatia moyo msonge mbele kwa kuwa sisi tupo nyuma yenu. 

Viungo wa serikali ni mawaziri, wabunge, wakuu wa mikoa na makatibu tawala, ambao baadhi yao wapo vizuri kwenye kazi japokuwa si wote. Kiuhalisia hawa ndio viungo kati ya ninyi washambualiaji na mabeki.

Ninaona uhusiano bora kutoka kwa viungo kwenda kwa washambuliaji.

Mheshimiwa Waziri Mkuu, mabeki wa nchi hii ni wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa vitengo mbalimbali vya wilaya, madiwani na viongozi wengine wa serikali ya wilaya kurudi chini hadi kwa mwenyekiti wa kitongoji. 

Ni hapa ndipo pana shida kubwa ama ni ya makusudi au ya bahati mbaya. 

Mheshimiwa Waziri Mkuu, pamoja na kuwa mnafanya vizuri kufunga mabao, lakini mabeki wenu wanafungisha mabao mengi sana. 

Hii ni sawa na washambuliaji kufunga mabao matano ilhali mabeki wanaruhusu mabao 10! 

Hapo kama timu tunakuwa tumepoteza mchezo na pointi pia. 

Mheshimiwa Waziri Mkuu, uongozi wa wilaya zetu ni shida tupu, na nitatoa mfano wa Wilaya ya Korogwe. 

Serikali yako inafanya kazi kubwa ya kuunganisha nguvu kati ya sekta binafsi na sekta ya umma ili kwa pamoja tuweze kuleta maendeleo ya haraka. 

Watanzania tumeweka mazao ya kimkakati ili tuweze kupata fedha za kigeni na kuboresha kipato kwa wananchi. Miongoni mwa mazao hayo ni mkonge. 

Sote tunafahamu kwamba Tanzania ilikuwa inaongoza katika soko la dunia kuanzia enzi za mkoloni hadi  mwanzoni mwa uongozi wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.

Na sasa tumekusudia kurudisha heshima hii tena. Ili hili liwezekane, tunahitaji sekta binafsi; yaani wananchi kulima zao hili kwa wingi, kitendo kitakachoongeza kipato na ukusanyaji wakodi pia. 

Mheshimiwa Waziri Mkuu, miongozi mwa mikoa ambayo imepokea suala hili kwa mtazamo chanya ni Tanga,  hasa Wilaya ya Korogwe, lakini viongozi wa Korogwe wanalikwamisha na kuwaacha wananchi wasijue nini cha kufanya. 

Mimi ni mwananchi wa Korogwe, ninatoka Kijiji cha Gemai, Mkumbara; kijiji kilichoandikishwa Desemba 21, 1975 na kupata usajili Na 482 mwaka 1977.

Hapa pamezuka mgogoro mkubwa wa ardhi kati ya kijiji hiki na Kijiji cha Goha, Kata ya Mkumbara, Mji Mdogo wa Mombo, Wilaya ya Korogwe.

Mheshimiwa Waziri Mkuu, Kijiji cha Goha kilitengwa kutoka Gemai. Ninafahamu kwamba vijiji hivi viwili vimepewa ramani za vijiji ila kiuhalisia wasomaji wazuri wa ramani hizi ni wataalamu kutoka Halmashauri ya Korogwe Vijijini. 

Mheshimiwa Waziri Mkuu, mgogoro huu ulifikia pabaya kiasi ambacho watu walikaribia kuuana wakiwa mashambani. 

Februari 13, 2021 kulifanyika mkutano wa vijiji hivi viwili, lakini muafaka haukupatikana. Ilipofika Machi 25, 2021 walikuja wataalamu wa halmashauri na kusimamisha watu wasifanye kazi yoyote katika eneo lenye mgogoro, wakisema mwezi mmoja baadaye watakuwa wametatua tatizo hilo. 

Mheshimiwa Waziri Mkuu, hadi sasa wataalamu hawa wapo kimya, hakuna chochote kinachofanyika. Mei 21, 2022 tuliandika barua kwa mkurugenzi, lakini  cha kushangaza alituambia suala hili lipo Ardhi na kwamba yeye hahusiani nalo. 

Ndipo tulipomtuma mjumbe kwenda Ardhi na wataalamu wakatujibu kuwa bado hawajawezeshwa gari kuja Gemai na vifaa, hatujui ni vifaa gani. 

Mheshimiwa Waziri Mkuu, kama suala hili lingemalizwa kwa wakati, sasa hivi wananchi wa vijiji hivi viwili wangekuwa na mkonge ambao miaka miwili ijayo wangetokomeza umaskini! 

Maswali ya kujiuliza ni; Je, ni kweli halmashauri haina gari au mafuta ya kwenda Gemai kwa zaidi ya mwaka sasa?Je, halmashauri haina GPS (Global Position System)ya kuonyesha mpaka? 

Je, hivi ni kweli wataalamu wa halmashauri hawana hata ‘Total station’ kwa ajili ya kufanya ‘survey’? Hivi, Mheshimiwa Waziri Mkuu, halmashauri haina vifaa kweli? Walichoraje ramani za vijiji hivyo? 

Kwa hakika mlifanya vema kuondoa wafanyakazi hewa, sasa kama tuna wataalamu katika halmashauri ambao hawawezi kumaliza migogoro ya ardhi katika maeneo yao, tunawalipa mshahara wa nini?

Hawa si wafanya kazi hewa! Kuna minong’ono eti hawawezi kutoka ofisini bila posho. Hivi wao mnawalipa kwa kazi gani ambazo haziwaruhusu kwenda ‘site’? 

Mheshimiwa Waziri Mkuu, mimi nashauri vitengo hivi tuvifute kabisa kwenye halmashauri zetu ili ikitokea mgogoro kampuni za watu binafsi zitaumaliza haraka, kwa kuwa hawa ndugu zetu wanachonganisha serikali na wananchi, kwa sababu si Watanzania wote wanajua kuwa ni baadhi tu ya wafanyakazi wa serikali wanaofanya vibaya kiutendaji. 

Lawama zinapelekwa serikalini kwa kufuata msemo wa Kiswahili: “Samaki mmoja akioza, wote wameoza.”

Mheshimiwa Waziri Mkuu, piga hesabu ya wafanyakazi wa vitengo hivi wa halmashauri za Tanzania nzima tunawalipa kila mwezi mamilioni ya fedha za walipa kodi ila hata wakienda kukipima kijiji au mji mdogo lazima walipwe fedha kama kampuni binafsi na wakati mwingine wana gharama kuliko hata kampuni binafsi. 

Hivi hawa ndugu zetu wanataka wananchi wauane ndipo waende kumaliza migogoro? 

Mheshimiwa, nimeamua kukuandikia kwa kuwa hata Waziri wa Ardhi sasa hivi simjui. Nilikuwa namfahamu William Lukuvi kwa kuwa tulikuwa tunamuona kiutendaji. 

Sasa hivi Kijiji cha Gemai kimo katika wakati mgumu. Watu wamelima maharage ila mvua zimekatika mapema hata mbegu hatutapata na kiangazi cha mwaka huu kinaonyesha kitakuwa kikubwa kuliko mwaka jana. 

Aidha, tumelima viazi, navyo vimekauka kwa jua, kwa sababu ya uhaba wa mvua. 

Tegemeo  letu kubwa ni kuwekeza kwenye zao letu la kimkakati; mkonge, ambalo linakwenda sambamba na mabadiliko ya tabia nchi, ila tunakwamishwa na viongozi wachache wasio waaminifu na wasio na hata chembe ya huruma kwa Watanzania wanyonge. 

Mheshimiwa Waziri Mkuu, tunakuomba utusaidie kwa hili. Wapigie simu tu. Au mtume huyo Waziri wa Ardhi atusaidie. 

Hali yetu ni ngumu na hatuna pa kwenda. Sisi wananchi tunawaogopa viongozi wa halmashauri kwa kuwa wanatutishia kuwa kama tunawasumbua, watatuhamishia Lushoto na ardhi yetu iporwe.

Mheshimiwa Waziri Mkuu, tuna imani kubwa na serikali yako chini cha Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Tusaidie sisi wanyonge. Tunatanguliza shukurani zetu za dhati.

Mungu ibariki Tanzania. Mungu inusuru Halmashauri ya Korogwe Vijijini.

Wako katika ujenzi wa taifa.

Richard Mcharo

Simu: 0766-267 160 / 0656-455 873

Please follow and like us:
Pin Share