Naungana na Watanzania wote kutoa pole kwa familia ya Komredi Kingunge
Ngombale-Mwiru, kutokana na kifo cha mwamba huo wa siasa katika Taifa
letu.
Mzee Kingunge atakumbukwa kwa umahiri wake wa kujenga hoja na weledi
aliojaaliwa na Mwenyezi Mungu, hata akaweza kuwa lulu na moja ya injini
muhimu katika ustawi wa Taifa letu.
Bahati mbaya watu wa aina yake wanapofariki dunia mara moja jamii
huwasahau. Tumeona juhudi nyingi za kuwaenzi waasisi wa Taifa letu kwa
kuyapa majina majengo, madaraja, barabara na kadhalika. Naamini katika
hili mamlaka zinazohusika, kila moja kwa wakati wake, zitaona namna
nzuri ya kumuenzi mzee huyu. Kwa mfano, inaweza kutazamwa barabara
moja yenye hadhi ikapewa jina la shujaa huyu.
Lakini lililo kubwa zaidi ni kwa vyama vya siasa na wanasiasa
kuyarejea maandiko ya nguli huyu ili yawasaidie katika ujenzi wa vyama
imara vyenye maono ya kuwaletea wananchi maendeleo. Kumweleza Mzee
Kingunge kunahitaji kurasa nyingi mno. Itoshe kumwombea pumziko jema
huko alikotangulia.
Wiki iliyopita, kulikuwa na matukio mawili mengine yaliyowagusa
makabwela katika Jiji la Dar es Salaam, na bila shaka na sehemu nyingne
nchini. Tukio la kwanza lilikuwa ni la Wiki ya Sheria, na la pili ni
lile lililotangulia – la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda –
aliyewakaribisha wananchi wenye malalamiko ya kudhulumiwa haki zao.
Hili la Wiki ya Sheria sina mjadala nalo sana kwa sababu limekuwa
tukio la kila mwaka. Wananchi hujitokeza kupata msaada wa kisheria kwa
mashauri yanayowagusa. Kama ilivyo ada, Rais wa Jamhuri ya Muungano
hupata wasaa wa kueleza aliyonayo. Hotuba zake mara kadhaa zimeibua
mijadala. Wapo wanaodai amekuwa akivuka mpaka kwa kuingilia muhimili
mwingine! Lakini wapo wanaoona yuko sahihi.
Rais ndiye kiongozi mkuu wa nchi (dola). Dola inaundwa na mihimili
mitatu – Utawala (Rais), Bunge (Spika) na Mahakama (Jaji Mkuu).
Pengine kwa kuwa Rais anachaguliwa na wananchi, hii inaweza kuwa
sababu ya kumfanya aingilie baadhi ya mambo ambayo wakati mwingine
yanatafsiriwa kuwa ni kuingilia mihimili mingine.
Kufaulu au kufeli kwa dola yoyote kunaweza kusababishwa na kasoro
kwenye muhimili mmoja, miwili, au yote. Lakini lililo kubwa ni kuwa
muhimili wa Utawala ndiyo wenye dhima ya kutekeleza yale ambayo
wananchi wangependa kuona wakitendewa. Rais anachaguliwa na wananchi.
Jaji Mkuu anateuliwa, na Spika anachaguliwa na wabunge. Kwa wote hawa
watatu Rais ndiye aliyeko kwenye kikaango zaidi hata kama udhaifu
utakaoikabili dola unaweza kuwa umesababishwa na ama Bunge, au
Mahakama.
Mathalani, wananchi wakikosa dawa au chakula Mahakama hawawezi
kuilaumu Mahakama. Wanafunzi wakikosa huduma za kuwawezesha kusoma
vizuri hawalishutumu Bunge (labda kama limekataa kuridhia bajeri).
Watumishi wa Bunge, Mahakama au Serikali wanapokosa mishahara wa
kulaumiwa ni Utawala.
Huu mzigo wote wa kuibeba dola nadhani ndiyo unamfanya wakati
mwingine, Rais, ama kwa kukusudia, au kwa kutokusudia, ajikute anatoa
maelekezo yanayotafsiriwa tofauti. Kama alivyowahi kusema yeye
mwenyewe, yote inaweza kuwa mihimili, lakini upo wenye mzizi mrefu
zaidi.
Hatua hii inanipeleka moja kwa moja kujadili uamuzi wa Makonda wa
kuwakaribisha makabwela wanaolia na kutaabika kwa kudhulumiwa haki
zao.
Yamekuwapo mambo kadhaa ambayo nimekuwa sikubaliani na Makonda, lakini
imeniwia vigumu kumpinga katika hili alilolifanya kwa wanyonge wa Mkoa
wa Dar es Salaam.
Kwenye hili tunapaswa kuweka pembeni lawama za kuhoji kuwa yeye ni
nani hata aweze kuwaita watu wamweleze kilio chao cha kudhulumiwa.
Tunaweza kusema hana mamlaka ya kubadili uamuzi uliotolewa na Mahakama
au mamlaka nyingine. Tunaweza kuhoji kama kweli ana nguvu au mamlaka
ya kutengua adhabu zilizozipendelea benki, na kadhalika.
Vyovyote iwavyo, hatua ya Makonda kuwakaribisha maskini waliodhulumiwa
ni ya kupigiwa mfano. Inatusaidia kwenda mbali zaidi kutambua ukubwa
wa tatizo la upatikanaji haki katika nchi yetu.
Kwenye shughuli hii ya Makonda, lawama nyingine zimeelekezwa kwa
Mahakama, Polisi na wanasheria (mawakili). Wananchi wengi wameonesha
vielelezo kuthibitisha namna walivyodhulumiwa kwa msaada wa Mahakama,
wanasheria au Polisi.
Ninachotaka kusema hapa ni kwamba tunaweza kumpuuza Makonda kwa hatua yake ya kuwaita maskini hao waliodhulumiwa, lakini hatuna budi kukiri
kuwa tukio hili limetusaidia kujua ukubwa wa tatizo la dhuluma katika
Mkoa wa Dar es Salaam na kwa hakika kwa nchi nzima.
Sisi tunaofanya kazi katika vyumba vya habari tunaletewa malalamiko
mengi mno na wananchi waliodhulumiwa nyumba, mashamba, magari au mali
nyingine. Yapo matukio mengi mno. Nakumbuka tukio moja niliwahi
kuwapeleka wananchi kwa Jaji Mkuu wa wakati huo, Augustino Ramadhani.
Huyu ni mmoja wa majaji wanyenyekevu. Wananchi walionifuata, walikuwa wamehangaika kwa miaka minne kumfikia Jaji Mkuu bila mafanikio.
Walikuwa na fedha zao – milioni kadhaa – zilizokuwa zimekaliwa katika
Ofisi ya Msajili. Nilipowasikiliza, nikaona ile si habari ya
kuiandika, bali ya kuwawezesha wamwone Jaji Mkuu. Nikampigia simu.
Akapokea. Nikamweleza kisa cha maskini hao. Akaagiza wamwone ofisini
kwake baada ya siku moja. Nikawaeleza. Hawakuamini. Mmoja akasema,
“Tumehangaika miaka minne bila mafanikio wewe leo unasema tumwone
keshokutwa? Sidhani kama tutafanikiwa, tutaenda tu lakini siamini kama
kuna lolote la maana tutakalopata.”
Haya maneno yalionesha namna walivyokata tamaa, na kwao walichoamini
ni habari hiyo iandikwe ili Rais aisome na kisha awasaidie. Kweli,
siku ilipowadia walifika ofisini kwa Jaji Mkuu. Akawapokea na
kuwasikiliza. Hapo hapo akawafurusha hao waliokalia haki ya
wananchi hao kwa miaka zaidi ya mitano! Akawahakikishia kuwa watapata
haki yao. Wale watu wakarejea ofisini kwangu siku hiyo hiyo. Mmoja
alipofika akanipa mkono, lakini hakujibu kitu. Akawa ameufunika uso
wake. Alikuwa akilia (kwa furaha).

 

Hoja ikawa kwamba mimi ni nani hata nimewawezesha wamwone Jaji Mkuu ndani ya muda mfupi? Nikawajibu kuwa tunao viongozi wazuri wasiopenda kuona watu wakitaabika, lakini shida inaletwa na wachache walio kwenye nafasi nyeti!  Baadaye wananchi wale wakalipwa fedha zao. Hawakurudi kwangu, lakini nikawa nimefarijika kwa kuona kuwa nimetekeleza wajibu wangu. Maskini wamepata haki yao.
Ofisini kwetu tuna mwandishi mmoja mahsusi kwa ajili ya kupokea na
kufanyia kazi malalamiko ya wananchi waliodhulumiwa ardhi, nyumba,
mashamba na kadhalika. Malalamiko ni mengi sana. Tunawashukuru baadhi
ya viongozi na watendaji kwenye mamlaka za utoaji haki ambao mara
kadhaa tumewapelekea vilio vya maskini hawa na wakawasaidia.
Moja ya vitu vinavyowaumiza sana maskini katika nchi yetu ni huu mfumo
wa kisheria wa kufuta kesi kwa njia za ‘ujanja ujanja’ (technicalities).

 

Kwa mfano, mwananchi aliyedhulumiwa shamba anamfuata
wakili. Yule wakili anaandaa maelezo ya kesi ya mlalamikaji, lakini
badala ya kutumia kwa mfano kifungu 12, anaweza kuandika 22.
Wanapokwenda kwa hakimu au kwa jaji, wakili wa upande wa pili
anawasilisha hoja ya kutupwa kwa kesi kwa sababu kifungu kilichotumiwa
na upande wa mlalamikaji si kilichopo kwenye sheria. Kesi nyingine
zimetupwa kwa njia hii. Kuna madai kwamba baadhi ya mawakili huwa
‘wana-conspire’ na upande wa pili ili kuvuruga kesi.
Tufanye nini? Hili suala baadhi ya Mahakimu na Majaji wameliona.
Wamelilalamikia lakini wamefungwa mikono kwa sababu wao kazi yao ni
kutafsiri sheria. Tunapofika hapo ndipo tunapowageukia wabunge wetu na
kuwaomba watazame upya hii kitu ‘technicalities’ ili warekebishe
sheria. Kwa kufanya hivyo, pale inapokuwa kifungu kimekosea, basi
hakimu au jaji awe na mamlaka kisheria ya kuutaka upande husika
kufanya marekebisho na hivyo kuendelea na kesi. Huu ni wajibu wa
wabunge. Kufuta kesi kwa njia hizi za ‘ujanja-ujanja’ kunawaumiza mno
maskini wengi katika nchi yetu.
Itoshe tu kusema Makonda ametukumbusha namna mfumo wetu wa utoaji haki katika Taifa letu ulivyo na mushkeli. Tunaweza kuilaumu Mahakama,
lakini ukweli ni kuwa mnyororo wa chanzo cha shida hii ni mrefu. Upo
kwa wanasheria, Polisi na mamlaka nyingine za usimamizi na utoaji wa
haki.

 

Tukilikiri hilo tutajua ni kwanini Rais Magufuli wakat mwingine anazungumza kwa hisia kali na kuonekana kama vile anaingilia mihimili mingine. Atakuwa kiongozi wa ajabu kuona watu wake wakitaabika kwa dhuluma, na yeye kama kiongozi mkuu wa dola akakaa kimya. Nchi inapojaa dhuluma lawama nyingi humwendea kiongozi mkuu maana wananchi wanamjua yeye kwa kuwa wamemchagua awaondolee kero.

Please follow and like us:
Pin Share