Ukitaka kufanikiwa jifanye kama mti. Refuka uwezavyo. Usiangalie miti mingine ilivyo mifupi ama ilivyo mirefu. Nisikilize kwa umakini hapa; Iko hivi, unalo jambo la kujifunza kutoka kwa walioshindwa kufanikiwa. Jifunze. Ukifahamu kilichowafanya wasifanikiwe, utajifunza namna ya kukabiliana nacho. Lakini pia, unalo jambo kubwa la kujifunza kutoka kwa waliofanikiwa ili na wewe ufanikiwe kama wao au zaidi ya wao. Walioshindwa kufanikiwa wana jambo la kukufundisha na waliofanikiwa wana jambo pia la kukufundisha. Kuwa tayari kujifunza somo zuri kutoka kwa watu hao wawili.

Mwandishi Enock Maregesi anasema: “Kuwa teja wa mafanikio.” Usikate tamaa, wewe ni mwana-mafanikio. Ota ndoto za mafanikio. Tembea na ndoto za mafanikio. Ongea ndoto za mafanikio. Fikiria ndoto za mafanikio. Simamia ndoto zako. Teseka kwa ajili ya ndoto yako. Teseka kwa ajili ya kipaji chako. Ndoto ni tunda bichi la unabii. Ndoto ni picha ya kesho. Ndoto ni mbegu za uhalisia wa yajayo.

Tumeumbwa kufanikiwa. Tumeumbwa kushinda. Tazama huu ushuhuda wa John Paul DeJoria. John Paul DeJoria akiwa katika shule ya upili [kidato cha tano na sita] mwalimu wake alimwambia: “Wewe John huwezi kufika popote kwa sababu huna akili za kimasomo.”

John Paul hakukatishwa tamaa na maneno ya mwalimu wake. Aliendelea kuhangaika kutafuta maisha  yake. John Paul alioa lakini kuna wakati maisha yalimwendea kombo. Akayumba sana kiuchumi. Mke wake John alipoona maisha yamekuwa magumu alimkimbia John na kumwachia mtoto mmoja wa miaka miwili.

John alianza kuokota chupa tupu zilizotumika na kuziuza ili amtunze mwanae. Siku zote John alimwambia mwanaye: “Tutatoka kimaisha pamoja.” John alianza pia kufanya biashara ya kuuza magazeti mlango mmoja baada ya mwingine. Ilifika hatua akaamua kuanzisha kampuni. Watu walimbeza na wakamwambia kwamba hana elimu yoyote ya biashara na hana pesa za kutosha za kuendesha biashara. John aliendelea kukomaa. Mwaka 2015, jarida maarufu la Forbes lilimtaja kama tajiri namba 234 kati ya matajiri 400 kutoka Marekani akiwa na utajiri wa dola bilioni 2.8 za Marekani. John Paul pia ni mwanzilishi wa bidhaa za nywele zinazojulikana kama Paul Mitchel.

Mafanikio ni nchi ya juhudi. Ili uishi kwenye nchi hii ya juhudi ni lazima ujifunze kuwa na nidhamu ya pesa. Mikono yenye nidhamu ya pesa ni mikono mizuri. Mwandishi Idow Koyenikan anasema: “Pesa inapotambua kuwa ipo kwenye mikono salama inataka kukaa na kuongezeka.” Pesa ina macho, inaona namna unavyoitumia. Pesa ina masikio, inasikia namna unavyoizungumzia. Desturi ya pesa ni kwamba inawapenda wanaoitumia vizuri na inawakimbia wale wanaoitumia vibaya.

Mwandishi wa vitabu vya ujasiriamali, Brian Tracy, anasema: “Ni vigumu kuipata pesa na rahisi kuipoteza. Ilinde kwa uangalifu.” Itafute pesa lakini ukiipata itumie kwa busara. Mwandishi Clement Stone anasema: “Kama huwezi kuweka akiba ya pesa, mbegu za kuwa mtu mkubwa haziko ndani mwako.” Jifunze kuweka akiba pesa na jifunze kuwa na nidhamu pesa.

Ili uishi kwenye nchi ya juhudi ni lazima uwapende wateja wako. Jeff Bezoe, mwanzilishi wa Amazon anasema: “Tunawaona wateja wetu kama wageni waalikwa kwenye sherehe na sisi ni wenyeji wa sherehe.” Mteja ni mtu muhimu sana katika mafanikio yako. Anachangia kuupanua mfuko wako. Anasaidia kukutangaza. Tumia lugha nzuri kumpokea na kumkaribisha mteja.

Onyesha uso wa tabasamu na furaha unapokuwa unamkaribisha mteja. Mwambie karibu kaka, karibu mama, karibu baba. Mteja ni mfalme. Methali ya watu wa China inasema: “Mtu asiye na uso wa tabasamu asifungue duka.” Kama una tabia ya kumpokea mteja kwa kujisikia sahau kufanikiwa. Mpokee mteja kama unavyompokea mgeni wako wa muhimu. Mteja ni mgeni. Amekuletea pesa. Amekuletea mafanikio unayoyatafuta. Amekuletea mawazo mapya. Kuna baadhi ya wateja wakifika ukawapokea kwa furaha, wanakuachia ushauri wa namna ya kuimarisha huduma yako. Furahi kumpokea. Onyesha kujali. James Cash Penney, mwanzilishi wa J.C. Penney Store anasema: “Kumtendea kwa heshima mteja kutamfanya awe tangazo la biashara yako.”

Naomba kukutia hamasa! Ni kweli, safari ya kuyafikia mafanikio halali ni ndefu. Ukianguka, tafadhali inuka. Njiani utakutana na changamoto za kila aina. Utatukanwa, utabezwa, utadharauliwa, utafyonzwa sana lakini vaa viatu vya uvumilivu. Usikate tamaa.

Endelea kupambana mpaka kieleweke. Hakuna aliyewahi kufanikiwa bila kushindwa. Usiogope kushindwa. Mchezaji wa mpira wa kikapu, Michael Jordan, anasema: “Nimeshindwa mara nyingi maishani ndiyo sababu ninafanikiwa.” Mwandishi mashuhuri wa vitabu, Gilbert Chesterton, hakuweza kusoma mpaka  darasa la tatu. Alipoanza shule hakuwa anafanya vizuri darasani. Siku moja mwalimu wake alimwambia: “Tukifungua kichwa chako hatutakuta ubongo lakini tutakuta rundo la mafuta  meupe.”

Baadaye Gilbert alijiandaa na akaandika vitabu vingi sana. Mwanasayansi maarufu duniani, Charles Darwin, alikuwa anafanya vibaya  sana darasani, siku moja  mwalimu wake alimwambia: “Utakuwa aibu kwa  familia yako.” Leo hii dunia nzima inafahamu mchango wa Charles Darwin.

Usiogope kushindwa. Endelea kupambana. Kesho yako inakuja, tena kesho yako ni ya matumaini na mafanikio makubwa. Mwandishi Henrieta C. Mears anasema:  “Mungu anatuacha tushindwe katika jambo ambalo si la msingi ili tuweze kufanikiwa katika jambo ambalo ni la msingi.”

Kuna nyakati fulani mtu anahisi kuwa hawezi kuona njia kwa urahisi. Anawahi kuhitimisha kwa kusema: “Hapa siwezi.” Kumbuka pale unaposema hapa nimefika mwisho, Mungu anasema: “Huu ni mwanzo mpya.” Mwandishi na mshairi wa Marekani, Albert Laighton, anatutia moyo kwa ujumbe huu: “Pale mwanadamu anapoona majani yamekauka. Mungu anaona maua mazuri yamechanua.”

Nahitimisha sura hii kwa kukuomba ujiandae kuzaliwa mbinguni. Maisha yetu ya hapa duniani yana ukomo! Tena yana ukomo. Unapojiandaa kufanikiwa hapa duniani, kumbuka pia kujiandaa kufanikiwa mbinguni. Tafakuri hii ya Mt. Camillus de Lellis itukumbushe umuhimu wa kujiandaa kuzaliwa mbinguni. Mt. Camillus de Lellis alipokuwa akipita katika makaburi ya ndugu zetu waliotangulia mbele ya haki alikuwa anajiuliza: “Ikiwa watu hawa wangeliweza kuishi tena wangefanya nini ili  waingie  mbinguni?’’

Please follow and like us:
Pin Share