Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Samweli Rweyemamu akimfanyia upasuaji wa tundu dogo kuondoa maji yaliyopo katika mfuko wa kutunza moyo mgonjwa ambaye moyo wake umejaa maji hivi karibuni katika Hospitali hiyo.

……………………

Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia

Kwa mara ya kwanza Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group imefanya upasuaji wa tundu dogo kuondoa maji yaliyokuwa yameuzunguka moyo kwa wagonjwa ambao walikuwa na tatizo la maji kujaa kwenye mfuko unaotunza moyo (pericardia effusion).

Upasuaji huo umefanyika kwa wagonjwa wawili ambao wameonekana kuwa na dalili za magonjwa mengine yaliyopelekea mfuko unaotunza moyo kujaa maji kwa kiwango kikubwa.

Akizungumza kuhusu matibabu hayo Daktari Bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete tawi la JKCI Hospitali ya Dar Group Samweli Rweyemamu amesema wagonjwa hao maji yamekuwa yakijaa pole pole kwenye mfuko unaotunza moyo ambapo mgonjwa mmoja maji yaliyotolewa yalifika kiasi cha lita moja na nusu na mwingine mills 750.

Dkt. Rweyemamu ambaye pia ni Mkuu wa Sehemu ya Huduma za Tiba JKCI Hospitali ya Dar Group alisema kwa kawaida maji yaliyopo kwenye mfuko unaotunza moyo huwa mills 50 hadi 100 lakini ikitokea yakaongezeka ghafla hadi kufukia mills 200 na kuendelea mtu huanza kupata hali za tofauti katika mwili wake ikiwemo kuchoka, mapigo ya moyo kwenda mbio na moyo kushindwa kufanya kazi vizuri.

“Tiba ya tatizo la kujaa maji kwenye mfuko unaotunza moyo ni kuyaondoa maji hayo ambapo kwa wagonjwa hawa tumeweza kuwatoa maji yaliyokuwa yamezunguka mioyo yao na kuusababishia moyo kutaka kusimama”,

“Kiashiria kikubwa anachokuwa nacho mgonjwa ambaye maji yamejaa kwenye mfuko unaotunza moyo anaweza kuwa na magonjwa mengine ambayo yanaashiria ugonjwa wa kifua kikuu (TB) hivyo kupelekea mfuko unaolinda moyo kujaa maji”, amesema Dkt. Rweyemamu.

Dkt. Rweyemamu alisema maji yaliyotolewa kwa wagonjwa hao yamepelekwa katika Maabara za juu kwaajili ya kuchunguza tatizo lililosababisha maji kujaa lakini pia kuangalia kama kuna tatizo zaidi kutokana na maji hayo kuwa na mchanganyiko wa damu.

“Mgonjwa mmoja tuliyemtolea maji alikuwa anapata changamoto ya kupumua kutokana na maji kujaa eneo linalouzunguka moyo wake, pia oksijeni kwenye mwili wake ilikuwa inashuka, na mapigo yake ya moyo yalikuwa juu sana”, amesema Dkt. Rweyemamu.

Dkt. Rweyemamu alisema kutokana na tatizo walilokuwa nalo wagonjwa hao la kujaa maji na mioyo yao kushindwa kufanya kazi vizuri kama wasingepatiwa matibabu mapema wangeweza kupoteza maisha ghafla.

Naye mgonjwa aliyefanyiwa upasuaji mdogo wa moyo kuondoa maji katika mfuko unaotunza moyo Hussein Mamboleo alisema kwa muda wa wiki mbili zilizopita amekuwa akikosa nguvu na kusikia mapigo ya moyo kwenda kwa haraka hivyo kufika JKCI Hospitali ya Dar group kwa ajili ya kuchunguza.

Hussein alisema baada ya uchunguzi na kugundulika kuwa moyo wake umezungukwa na maji alipatiwa matibabu ya kuondoa maji hayo ambapo baada ya matibabu amekuwa akifanya mazoezi ya kutembea na kutokujisikia tena kuchoka kama ilivyokuwa hapo awali.

“Kwasasa nipo vizuri naweza kutembea umbali mrefu bila ya kuchoka, nawapongeza Taasisi ya Moyo kuweza kusogeza huduma za matibabu ya moyo karibu na wananchi kwani sisi watu wa Temeke sasa hatuna haja ya kwenda JKCI upanga kwaaliji ya matibabu ya moyo”, amesema Hussein.

Hussein alisema kupatiwa matibabu JKCI Hospitali ya Dar Group kumeirahisishia familia yake kupata urahisi wa kumhudumia mgonjwa umbali mfupi kutoka nyumbani.

JKCI Hospitali ya Dar Group imekuwa ikipokea wagonjwa wa moyo kutoka maeneo mbalimbali ya Temeke na maeneo ya jirani hivyo sasa kuanza kutoa huduma za upasuaji mdogo wa moyo kwa wagonjwa wanaohitaji matibabu hayo kurahisisha upatikanaji wa huduma na kusogeza huduma karibu

By Jamhuri