Na Waandishi Wetu, JamhuriMedia

Mwendo wa maisha ya Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, umemalizika baada ya Jumamosi ya wiki iliyopita kuzikwa katika Kijiji cha Mangapwani, Zanzibar.

Mwinyi, maarufu kwa jina la ‘Mzee Rukhsa’ amezikwa katika kijiji hicho kilichopo Mkoa wa Kaskazini Unguja, Wilaya ya Kaskazini ambako ni mahali alikokulia na kupata elimu ya msingi na kati baada ya kuagwa na maelfu ya watu mbalimbali wakiwamo viongozi wa kitaifa kutoka ndani na nje ya nchi kwenye Uwanja wa Amaan Complex, Zanzibar.

Makamu wa Rais, Dk. Isidor Mpango, amewaongoza mamia ya Watanzania kuhifadhi mwili wa Mzee Mwinyi katika makaburi yaliyopo kijijini hapo.
Mazishi yake yalianza saa 10 jioni yakiongozwa na viongozi wa dini kwa kumsomea dua na baadaye taratibu za kijeshi ziliendelea, ikiwamo kupigwa mizinga 21.

Samia awaongoza Watanzania kuaga

Rais Samia Suluhu Hassan amewaongoza Watanzania kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa Mzee Mwinyi.

Akizungumza kabla ya kuaga mwili huo, amesema jambo pekee la kufanya tumkumbuke Mzee Mwinyi ni kuendeleza mema yote aliyoyaishi.

“Mzee Mwinyi aliishi kwa kufuata misingi bora ya maisha katika uhai wake wote, akiwa kijana baba yake alimsihi kuwa mcha Mungu , mnyenyekevu, asiyejiona bora kuliko wengine, mtumishi wa watu kwa shida zao, mkarimu na mtu asiyekata shauri peke yake juu ya masuala muhimu,” amesema.

Pia ameitaka familia ya Mzee Mwinyi kuendelea kuheshimiana na kushikamana, na hawatafurahi kuiona inakinzana kutokana na migogoro.
“Mdogo wangu Hussein, simama kama mbuyu, na mbuyu huu uende ukaheshimike. Mbuyu unapong’oka si shida kupanda mwingine, kati yenu 11 mliobaki mmoja asimame awe mbuyu,” amesema.

Akitoa wasifu wa Mzee Mwinyi, amesema alikuwa mwanamageuzi katika nyanja za kisiasa, kiuchumi, kijamii na aliheshimu haki za watu na utawala bora.

Amesema alikuwa ni maktaba inayotembea na iliyosheheni vitabu vyenye mafunzo ya uadilifu, uzalendo, ustahimilivu, mageuzi, ujasiri, unyenyekevu na ucha-Mungu.

Vilevile amesema alisimamia mageuzi ya kisiasa kwa kurejesha mfumo wa vyama vingi na kuruhusu uwekezaji wa kampuni binafsi.

Katika hatua nyingine, ametaja mafunzo aliyopata kwake kuwa ni kiongozi shupavu, asiyeyumba, kwa sababu licha ya masharti magumu ya sera za kiuchumi za Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na kuwa na uchumi dhaifu lakini Mzee Mwinyi alifanya mageuzi makubwa.

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi akiweka mchanga katika kaburi la baba yake, Rais mstaafu, hayati Ali Hassan Mwinyi.

Atoa wosia kwa familia yake

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema kabla ya kifo cha baba yao aliwaita wote akawaeleza wanatakiwa wawe wamoja na akamchagua asimamie familia hiyo.

Akizungumza juzi wakati wa hitma ya Mzee Mwinyi iliyoandaliwa na Rais Samia katika viwanja vya Maonyesho Nyamanzi Fumba, Unguja, amesema: “Aliniita kwa jina, akaniambia nakuagiza wewe si kwa ukubwa wako, bali kwa nafasi uliyonayo, uwe msimamizi wa familia yangu,” amesema.

Pia amesema alijizuia kuzungumza lakini akahisi ana deni kubwa na asipofanya hivyo ataendelea kubaki nalo.

Katika hatua nyingine, amemshukuru Rais Samia akisema amewafanyia wema tangu Mzee Mwinyi alipopelekwa nchini Uingereza kwa matibabu na alikuwa karibu nao akiwauliza kila hatua inayoendelea.

“Rais Samia alipokuja kumtembelea nyumbani Mikocheni, Mzee wetu alilia kwa furaha kumuona Rais wetu,” amesema.

Amewashukuru madaktari wa Hospitali ya Mzena alikokuwa amelazwa Mzee Mwinyi akisema walimhudumia kwa saa 24 kwa upendo mkubwa.

“Mimi ni daktari, nimefanya kazi nje ya nchi na hapa nchini, katika maisha yangu sijawahi kuona watu waliojitolea kumsaidia mzee wetu kama madaktari wa Mzena, walikuwa hawabanduki. Mara nyingi mzee wetu hali yake ilikuwa ikibadilika, lakini tulikuwa nao wakati wote,” amesema.

Pia amewashukuru watu wote walivyojitoa kabla na wakati wa kifo cha baba yake na alikuwa akipokea simu nyingi kutoka kila upande wakimueleza jinsi wanavyomuombea dua mzee wao.

Wakati wa hitma hiyo, Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omar Kabi, amesema kulingana na wema aliofanya Mzee Mwinyi inawezekana amekwenda peponi moja kwa moja.

“Huyu mzee alikuwa ni mtu mwema na amefanya mengi mazuri na inaweza akawa ameepushwa motoni, wasiwasi upo kwetu sisi, tufuate matendo yake, alikuwa mtu wa vitendo na alikuwa ni mtu wa kusamehe na muadilifu,” amesema na kuongeza:

“Uadilifu wake umetajwa mara nyingi lakini alikuwa na huruma kwa watu anaowaongoza, alijishusha na kuwaheshimu masheikh wenzake. Wakati wa uhai wake alifanya mambo mengi, ikiwamo ujenzi wa misikiti na nyumba za ibada.
“Aliufungua uchumi na Zanzibar, watu walianza kwenda kisiwani hapo kutoka nchi mbalimbali kufanya biashara.”

Naye Katibu wa Mufti, Khalid Ali Mfaume, amesema wazee wenye hekima wanaondoka, lakini ni lazima kuendeleza waliyoyatenda.

“Machi 2, mwaka huu tumezika elimu, busara na hekima. Huyu alikuwa sheikh, alikuwa mwalimu, alipomaliza kazi ya urais alikuwa akisalisha misikiti mbalimbali, katika sifa zake zote, basi alikuwa mpenzi wa Mtume Muhamad (S.A.W).

“Maisha ya binadamu ni hadithi, kila mmoja anatamani azungumzwe hivihivi kama anavyozungumzwa mzee wetu, na hapa ndipo tunaposema waandaliwe watoto wetu katika malezi mema. Kila mmoja ana nafasi ya kubadilisha hadithi yake ili akiondoka azungumzwe vizuri,” amesema.

Kwa upande wake, Sheikh Othman Maalim, amesema mtu mwenye hekima anajua azungumze vipi na wakati gani na sifa hizo alikuwa nazo Mzee Mwinyi.
“Aliikuta Tanzania katika hali ngumu, kulikuwa na uchumi mgumu, anatajwa kwa mengi, ametengeneza historia na hatumtaji kwa sababu alikuwa Rais wetu.

“Bali kutokana na busara zake na hiyo ni mifano mizuri inayotakiwa kuzungumzwa na kufahamika kwa kila mmoja na watoto wadogo wajue, kwa sababu tunajua kuvaa viatu vya mzee itakuwa vigumu, lakini japo kwa kujifananisha naye kwa uchache,” amesema.

Wasifu wake

Mwinyi, maarufu kwa jina la Mzee Rukhsa amekutwa na mauti Februari 29, mwaka huu wakati akipatiwa matibabu ya ugonjwa wa saratani ya mapafu katika Hospitali ya Mzena iliyopo jijini Dar es Salaam.

Akitangaza kifo hicho, Rais Samia, amesema: “Kwa majonzi makubwa nasikitika kutangaza kifo cha Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, aliyefariki dunia saa 11:30 jioni alipokuwa akipatiwa matibabu.

“Mzee Mwinyi amekuwa akipatiwa matibabu tangu Novemba, mwaka jana jijini London, Uingereza na baadaye akarejea nchini na kuendelea na matibabu katika Hospitali ya Mzena,” amesema na kutangaza siku saba za maombolezo na bendera zitapepea nusu mlingoti kisha alitoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki.

Taarifa ya kifo hicho imekuja baada ya Februari 2, mwaka huu mtoto wake, Abdullah Ali Mwinyi, kutangaza baba yao kupelekwa hospitalini kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Mzee Mwinyi aliingia madarakani kuiongoza nchi Novemba 5, 1985 akipokea kijiti cha uongozi kutoka kwa Rais wa Awamu ya Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere.

Alizaliwa Mei 5, 1925 eneo la Kivule, Mkuranga mkoani Pwani akiwa ni mtoto wa Mzee Hassan na Asha Sheikh Mwinyi, huku maisha yake ya utotoni aliyatumia akiwa Unguja alikopelekwa na baba yake kujifunza masomo ya dini ya Kiislamu.

Kisha alipata elimu yake ya msingi katika Shule ya Mangapwani, Mjini Magharibi na akajiunga na Shule ya Sekondari ya Mikindani, Dole Mkoa wa Mjini Magharibi na baadaye alipata Stashahada ya Elimu ya Watu Wazima jijini Dublin, Ireland kuanzia mwaka 1954 hadi mwaka 1956.

Mwaka 1960 alipata Astashahada ya Umahiri katika Kiingereza kutoka Taasisi ya Regent, Uingereza na mwaka 1972 hadi mwaka 1974 alipata nyingine katika Lugha ya Kiarabu katika Jiji la Cairo, Misri.

Amewahi kuwa mwalimu wa shule za msingi za Mangapwani na Bumbwini, Zanzibar.

Kisiasa, mwaka 1964 alijiunga na Chama cha Afro Shiraz (ASP) na mwaka 1963 alishika nyadhifa mbalimbali katika Serikali ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Zanzibar.

Pia mwaka 1970 alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kati ya mwaka 1982 hadi mwaka 1983 alikuwa Waziri wa Afya, Waziri wa Mambo ya Ndani, Waziri wa Maliasili na Utalii na Balozi wa Tanzania nchini Misri.

Mwaka 1984 alichaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Amejaliwa kupata watoto 12 kutoka kwa wake zake wawili; Mama Khadija na Mama Siti Mwinyi. Majina ya watoto hao kwa mpangilio wa kuanzia wa kwanza hadi wa mwisho ni:-Asha, Hassan (marehemu), Njuma, Fatma, ⁠Abbas, ⁠Hussein, ⁠Mohammed ama Eddy, Abdullah, ⁠Salama, Dk. Amour, ⁠Halima na Asma.

Pamoja na mambo mengine, Mzee Mwinyi alikuwa ana tabia njema na moyo wa huruma kwa kuchukua watoto wa kuwalea na jumla aliwalea 55, yeye akiwa ndiye baba na wake zake ndio mama. Miongoni mwa hao 55 ni Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Dk. Abdulla Hasnu Makame na Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mahmoud Thabit Jecha, walioishi miaka kadhaa nyumbani kwake baada ya kuondokewa na wazazi wao.

Wamzungumzia Mzee Mwinyi

Akizungumza alipowaongoza maelfu ya Watanzania kuaga mwili huo katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, Dk. Mpango, amesema Mzee Mwinyi alikuwa kisima cha hekima, chemchemi ya elimu, shule ya uzalendo, uadilifu na uongozi.

Amesema alitoa mchango katika maeneo tofauti, ikiwamo katika kukuza na kufanya Kiswahili kutumika katika anga za kimataifa.

Pia amesema alikuwa mfano wa hali ya juu wa uwajibikaji baada ya kujiuzulu nafasi ya Waziri wa Mambo ya Ndani kutokana na mauaji asiyohusika nayo ya vikongwe waliotuhumiwa ni ‘wachawi’ mkoani Shinyanga na Mwanza.

“Mzee Mwinyi alikuwa ni kielelezo cha kutetea umoja wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nadhani ilikuwa ni baraka kwamba Mungu alipenda azaliwe Bara lakini akulie na kulelewa Unguja, alikuwa mzalendo asiyetiliwa shaka na alihamasisha kilimo,” amesema.

Kwa upande wake, Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, amesema Mzee Mwinyi alikuwa ni mpole lakini ni mkali na mwenye uamuzi mgumu.

“Nilikuwa namsoma akiwa waziri baadaye akajiuzulu akawa balozi, akarudi akawa Waziri kwenye Ofisi ya Makamu wa Rais, alikuwa ‘low profile’, hakuwa kimbelembele kuonekana sana,” amesema na kuongeza:

“Nilimfahamu mwaka 1984 wakati wa machafuko ya kisiasa Zanzibar, kulikuwa na mkutano wa NEC ulifanyika Dodoma na mimi nilikuwa mjumbe ndiyo nilikuwa nimeingia miaka miwili tu.

“Wajumbe wote tulipangiwa kulala kwenye hosteli za Chuo cha Biashara (CBE), si kawaida, maana tunapewa posho yetu tunakwenda kulala unapojua, baadaye tukaenda kusimuliwa kujua kwa nini ilikuwa vile.

“Mawaziri walikuwa wanalala nyumbani kwao, tulikuwa na mmoja aliyekuja kukaa na sisi. Waziri huyo ni Ali Hassan Mwinyi, tukafanya udadisi kwa nini? Tukajua ile ‘rest house’ chumba cha mapumziko alikopangiwa kukaa, waziri mwenzake aliamua kumuweka mtu mwingine.

“Kwa hiyo alijua ndiyo chumba chake cha siku zote akakuta mgeni mwingine, akaamua kutokugombana na kuja kujiunga na sisi wajumbe wa kawaida wa NEC. Alitupa mapenzi makubwa, hakuwa anadai ‘treatment’ tofauti na sisi.

“Tulijifunza kwamba alikuwa hapendi makuu, anaishi maisha ya kawaida kama watu wengine, ana mapenzi kwa watu, mchakato ulivyokuwa unakwenda baada ya Mzee Jumbe kujiuzulu yeye akapendekezwa, mpendekezaji ni Thabiti Kombo. Sisi tuliokaa naye hosteli tulifurahi maana tulikuwa tumeshamfahamu na tukasema Zanzibar watakuwa wamepata kiongozi thabiti.

“Pengine yule aliyemkataa kule Mwenyezi Mungu alimuongoza Mwinyi aje kukaa na sisi ili wajumbe wa NEC tumfahamu, atufahamu.”

Pia amesema alimfahamu alipomteua kuwa Mbunge na Naibu Waziri wa Nishati na Madini mwaka 1988.

“Nilikuwa jeshini, nikateuliwa kuwa Katibu wa CCM Nachingwea, baadaye wa Masasi mkoani Mtwara,” amesema na kuongeza:

“Nilipokwenda kumuona nikamwambia hii ya ubunge ni nzuri, nitakuwa natoka Masasi mara nne kwenda vikao vya Bunge lakini hili la Naibu Waziri silijui, akaniambia: ‘You are young, bright, best of luck’ akaniacha, hakuwa na interest ya kuendelea kunisikiliza, na mie nikatoka nikarudi kwa Katibu wa Rais, Mahamoud Jabir, akaniambia ‘mbona unaonekana umeloa sana’, ndiyo nikajitizama kumbe nilitokwa jasho kipindi kile nilichokuwa na mzee, nikamwambia kukaa na Rais sio jambo dogo.

“Baadaye nikaja kuwa Waziri wa Maji, Nishati na Madini, baadaye nikawa Waziri wake wa Fedha. Rais Mwinyi alikuwa msikivu sana, alikuwa anapokea ushauri, ukiwa mzuri.

“Watanzania tumkumbuke ndiye baba wa mageuzi ya kiuchumi na kisiasa. Haikuwa rahisi mjadala wa kuyapokea maelekezo ya IFM na World Bank, ya kufanya mageuzi ya kiuchumi kwenye NEC haikuwa rahisi, yalikuwa magumu, akasema ‘jamani ee kama ni mkuki unanichoma mie, mbele mkuki, nyuma mkuki’.”

Katika hatua nyingine, amesema Mzee Mwinyi alivunja Baraza la Mawaziri mara mbili na mara ya kwanza aliwaita mawaziri wote na manaibu mawaziri na hakuonyesha bashasha, akasema: “Nawashukuruni kwa mlivyonisaidia ila wenzangu naomba muende mkajiuzulu.”

“Tunatazamana wote tukajiuzulu eee! Akanyanyuka akaondoka, basi na sisi tukaondoka, kutoka nje hakuna magari madereva wameshaondoka, kwa sababu tuliamini ni mkutano na ungechelewa kwisha, tuliwaruhusu madereva waondoke na magari.

“Kwa vile wakati huo hakukuwa hata na simu za mkononi, haikuwezekana hata kuwaita madereva ili watupe usafiri wa kuondoka Ikulu, ikabidi tutoke na kuanza kutembea kwa miguu, tukiwa tumeongozana.

“Namshukuru Mzee Msuya (Cleopa) alikuwa Waziri wa Fedha, tukatembea hadi ofisini kwake akatupa magari yakatupeleka, tukawa tunafikiria hivi tunaandikaje barua ya kujiuzulu?

“Baada ya muda tukapata barua tusijiuzulu, baadaye tukapata barua wote tumefukuzwa, ondokeni ofisini kakaeni nyumbani hadi mtakapoitwa tena, basi akaunda tena Baraza ndiyo nikawa waziri kamili,” amesema.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa zamani, Jaji mstaafu, Joseph Sinde Warioba, amesema ni majonzi kuondokewa na Mzee Mwinyi lakini tunatakiwa kusherehekea maisha yake.

Amesema Mzee Mwinyi alilitumikia taifa hili kwa muda mrefu na alisaidia katika juhudi zake za kuleta maendeleo.

Wakati wa utawala wake, amesema tulikuwa na matatizo makubwa upande wa uchumi na matatizo ya kisiasa kwa sababu kabla ya kushika uongozi huko nyuma kulikuwa na matukio yaliyoathiri juhudi zetu za maendeleo.

“Ikiwamo kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Vita ya Uganda na kupanda kwa bei ya mafuta kulifanya uchumi wetu ukadorora,” amesema na kuongeza:

“Aliposhika uongozi wakati huo hali ilikuwa ni mbaya, sasa hivi tuna matatizo ya upungufu wa sukari, tuna matatizo ya umeme, changamoto ya maji, lakini matatizo tuliyo nayo sasa hivi ni madogo ukilinganisha na wakati aliposhika uongozi wa nchi hii.

“Alikuta nchi ikiwa na upungufu wa mafuta na shughuli za kiuchumi na kijamii zilikuwa zinakwama, alikuta nchi ilikuwa haina bidhaa madukani, wakati huo tulikuwa tunasema bidhaa adimu. Alikuta ina upungufu wa chakula na katika mazingira ambayo hatukuwa na rasilimali za kutosha, aliunda timu ya kumsaidia kupambana na matatizo ya uchumi, mimi nilikuwa mmoja wao kama msaidizi namba moja.”

Warioba aliyekuwa waziri mkuu wakati wa utawala wa Mzee Mwinyi, amesema kwa kipindi cha miaka mitatu walifanikiwa kufanya kazi usiku na mchana na matunda yake chini ya uongozi wake hali ya mafuta ilirejea kawaida na bidhaa zilikuwa zinapatikana, ikiwa ni matokeo ya rukhsa aliyoitoa.

Pia amesema baada ya miaka mitatu aliongoza taifa likatulia na tukaanza safari ya maendeleo.

“Lakini kulikuwa na matatizo ya kisiasa, wote mtakumbuka mwaka 1984 tulikuwa na matatizo Zanzibar na alipewa mzigo wa kwenda kuyatuliza alipokuwa Rais wa Zanzibar na kwa miaka miwili aliituliza, hata hivyo bado yalikuwa kwa nchi nzima,” amesema na kuongeza:

“Nakumbuka ilipofika mwaka 1988 kulikuwa na mpasuko wa uongozi katika nchi yetu, hata baadhi ya watu wakajiondoa kwenye chama kilichokuwa kinatawala. Wakati huo huo kulikuwa na vuguvugu la kuleta mabadiliko ya kisisa, si hapa ndani tu, dunia nzima.

“Mzee Mwinyi aliunda Tume ya Nyalali ikaleta mapendekezo. Alikuwa ni kiongozi mkubwa lakini maisha yake yalibaki kuwa ya mtu wa kawaida. Sisi wasaidizi wake tulikuwa tunamwona kama kaka yetu, baba, tunamheshimu lakini anatupa uhuru, ukiwa na wazo hata ukijua mzee ana wazo tofauti, hauogopi kumshauri, alikuwa anasikiliza ushauri lakini mwisho anafanya uamuzi mgumu.”