Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

KATIBU wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Paul Makonda amesema katika ziara yake aliyoifanya hivi karibuni katika mikoa 23 amebaini mambo makubwa matatu ikiwemo kukithiri kwa dhulma.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 5, 2024 a jijini Dar es Salaam, Makonda amesema mambo waliyoyabaini ni pamoja na kuwepo kwa kiwango kikubwa cha dhulma kukithiri hususani katika sekta ya ardhi.

“Dhulma hii imegawanyika katika maeneo mengi ikiwemo kilio cha watu wengi kunyang’anywa ardhi zao na walio na haki na wenye nguvu ya fedha ..kilio cha watu kupewa nyaraka na hati feki. Hata hivyo nilimuagiza Waziri wa Ardhi kushughulikia jambo hili na tayari hatua mbalimbali zimechukuliwa ili kutoa funzo kwa watu wanaotumia pesa kutapeli ardhi za wanyonge.

“Lakini pia Waziri anapaswa kufanya mapitio kwa watendaji wote ambao wameweka minyororo ya utapeli wa ardhi waweze kuchukuliwa hatua kwani utapeli wa ardhi umeonekana kuwa na mtandao mpana na si wa mtu mmoja pekee. Kila mtendaji ambae amekuwa katika mnyororo wa kuwaonea wananchi wabainishwe na lazima wachukuliwe hatua stahiki ili kuleta mabadiliko chanya, ” amesema.

Aidha ameongeza kuwa zipo dhulma nyingi zilizofanyika hasa za watu kujipatia mali kiudanganyifu hivyo mamlaka husika zinapaswa kuchukua hatua ili kukomesha dhuruma hizo.

Aidha amesema tatizo lingine ni viongozi kutokutatua kero za wananchi ambazo huwa wanazisikiliza hivyo chama kinaelekeza kila alie na nafasi anapaswa kutatua kero za wananchi kwani ofisi aliyopo ni ya umma hivyo kutokutatua kero zao ni kinyume na utumishi.

“Viongozi tusitatue changamoto za wananchi kwa sababu ya kujuana bali tutatue changamoto kwani wanahaki ndani ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano

“Changamoto nyingine ni ukatili wa kijinsia ambao umejitokeza kwenye baadhi ya mikoa hivyo changamoto hiyo inashughulikiwa ili kuja na mkakati thabiti wa kuzuia ukatili huo.

Sambamba na hayo amesema ziara hiyo imekuwa na mafanikio makubwa sana na kuwapongeza viongozi wote wa chama walioshirikiana katika ziara hiyo kwenye mikoa yao.

Katika hatua nyingine Makonda amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassani ameamua kutenga siku moja katika kila mwezi kwa ajili ya kusikiliza kero za wananchi .

Amesema ameamua kufanya hivyo kumuezi Hayati Rais wa Awamu ya Pili, Ally Hassan Mwinyi kutokana na kuwa na utaratibu huo enzi za uhai wake.

“Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ameamua kutenga siku moja kwa mwezi kuwasikiliza wananchi wa kipato cha chini na atafanya utaratibu huo aidha akiwa Dodoma, Zanzibar au hapa Dar es Salaam,” amesema.

By Jamhuri