Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linamshikiria Omari Mlopa (28),
mkazi wa Mlandizi na wenzake wawili wakiwa na pikipiki 32 zilizoibwa na baadae kuzifanya zao kwa kuzikodisha kwa mikataba kwa watu mbalimbali na kujipatia pesa kila siku.

Aidha Jeshi hilo limesema katika kipindi cha Januari hadi Februari, 2024 makosa ya pikipiki yaliyokamatwa ni 36,775, walioandikiwa faini za papo kwa hapo ni 36,754, waliofikishwa mahakamani ni 14, na mashauri 7 yapo kwenye ofisi ya
Mashitaka ya Taifa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 5, 2024 Kamanda Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema jeshi hilo linaendelea na operesheni kali maalum ya kuzuia vitendo vya kihalifu na kukamata watuhumiwa mbalimbali wakiwemo wezi wa pikikipi na kukamata pikipiki zilizoibwa maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam na mikoa ya jirani.

“Operesheni hii ilianza Februari 6, 2024 na inaendelea mpaka sasa imemkamata Omari Mlopa (28) mkazi wa Mlandizi na wenzake wawili wakiwa na pikipiki 32 zilizoibwa na baadae kuzifanya zao kwa kuzikodisha kwa mikataba kwa watu mbalimbali na kujipatia pesa kila siku.

“Uchunguzi wa awali uliofanywa na Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam umebaini kuwa watuhuhumiwa hao walibadilisha namba za usajili za pikipiki hizo na kuweka namba bandia ili zisitambulike,” amesema.

Amebainisha kuwa pikipiki 13 tayari zimetambuliwa na wamiliki.

Wakati huo huo, amesema Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linaendelea na operesheni maalum ya
ukamataji wa watu wanaokiuka sheria kwa kutenda makosa ya usalama barabarani hasa kwa waendesha pikipiki (Bodaboda) na Bajaji.

“Katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2023 makosa ya pikipiki yaliyokamatwa ni 179,174, walioandikiwa faini za papo kwa hapo ni 178,937, waliofikishwa Mahakamani ni 237, waliohukumiwa adhabu ya kulipa faini 236, na mmoja alihukumiwa kifungo jela.

“Katika Operesheni hii baadhi ya makosa ambayo yamekuwa yakijirudia mara kwa mara kwa waendesha pikipiki na bajaji ni kutovaa kofia ngumu, kupita taa nyekundu, ulevi, kuzidisha abiria, kupita barabara za
mabasi yaendayo haraka pamoja na kupakia abiria kwenye taa za kuongozea magari,” amesema.

Ameongeza kuwa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam licha ya kuendelea kutoa elimu juu ya uzuiaji wa makosa, ukamataji umelenga pia watu ambao wamekuwa wakikaidi na kutotii sheria kwa kuendesha vyombo vya moto
bila kujali na baadae kujikuta wakisababisha ajali.

By Jamhuri