Na Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo amesema kuwa uamuzi wa Serikali wa kufuta Taasisi ya Chakula na Lishe unalenga kuongeza wigo wa kusogeza karibu zaidi huduma za chakula na lishe kwa jamii.

Prof. Mkumbo amesema hayo leo Desemba 21, 2023 wakati akishiriki kwa njia ya simu katika kipindi cha Malumbano ya Hoja kinachorushwa na kituo cha televisheni cha ITV.

“Kufutwa kwa Taasisi si adhabu wala Serikali haijafuta programu za lishe nchini. Taasisi ya Chakula na Lishe ipo jijini Dar es salaam na ina wafanyakazi 121 pekee haipo katika kanda wala mikoa, nchi hii ina mikoa 31 na halmashauri 184 hivyo lengo ni kusogeza huduma karibu zaidi na jamii”, amesema Prof. Mkumbo.

Amefafanua “Programu za lishe zinafanyika katika ngazi za halmashauri hadi shule za msingi. Aidha, Serikali imefikia uamuzi huu baada ya kuangalia mwingiliano wa majukumu na malengo ya taasisi kwa kuwa tayari zipo taasisi nyingine nyingi zinazohusika na masuala ya lishe nchini, pia halmashauri zimeelekezwa kuwa na programu za lishe, na tunapoelekea ni kuwa na Idara za Lishe katika ngazi za halmashauri”.

Ameongeza kuwa lishe ni suala la kipaumbele kwa miaka mingi ndio maana Serikali imefanikiwa kupunguza kiwango cha udumavu kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano kutoka asilimia 48 mwaka 2000 hadi kufikia asilimia 30 mwaka 2022 na lengo ni kufikia asilimia 20 mwaka 2025.

Aidha, Prof. Mkumbo amesisitiza kuwa programu za lishe zitaendelea kutekelezwa nchini na wataalamu wote wa lishe watapelekwa sehemu husika.