Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Zikiwa zimebaki siku 10 ifike terehe ya mwisho kwa viongozi wa umma kuwasilisha tamko la rasilimali na madeni kwa Kamishna wa Maadili, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imewataka viongozi wote wa umma kuzingatia matakwa ya katiba na sheria ya maadili kwa kuwasilisha tamko lao ifikapo Desemba 31, mwaka huu.

Hayo yameelezwa jijini hapa na Katibu, Ukuzaji wa Maadili,Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Waziri Kipacha wakati akizungumza na vyombo vya habari kuhusu hali ya urejeshaji wa tamko la rasilimali, madeni na mfumo wa ujazaji fomu za tamko kwa njia ya mtandao.

Kipacha amesema mwenendo wa uwasilishaji taarifa hizo hauridhishi na kufafanua kuwa hadi kufikia Desemba 20,2023 ni Viongozi 2,475 pekee ndio wameweza kuwasilisha tamko lao kwa Kamishna wa Maadili kati ya Viongozi 15,762 sawa na asilimia 16 ya viongozi wote.

“Idadi hii ni sawa na asilimia 16 ya viongozi wote wanaopaswa kuwasilisha tamko la Rasilimali na madeni kwa mujibu wa sheria, napenda kuchukua nafasi hii kuwaomba ambapo bado watimize wajibu wao ili kuungana na Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hasan, Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango na Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa ambao tayari wametimiza wajibu huo, “amesema.

Ametumia nafasi hiyo pia kuwasihi viongozi wengine ambao bado hawajawasilisha matamko yao wakiwemo waliotamkwa katika tangazo la serikali Na. 857 la Novemba 24,2023 kuwa tangu siku ya tangazo hilo wanawajibika kutimiza masharti yote ya sheria ya Maadili ya viongozi wa Umma.

Amefafanua kuwa taarifa hizo zinazotakiwa kutumwa na viongozi ni pamoja na majina matatu, simu ya mkononi, barua pepe binafsi ya kiongozi husika, yaasisi anayofanyia kazi wadhifa wa kiongozi na tarehe ya uteuzi .

“Kuhusu viongozi wapya wao watatatikiwa kuwasilisha taarifa zao ndani ya siku 14 baada ya kuteuliwa au kupandishwa cheo ambapo watatumiwa taarifa za siri kwa ujumbe mfupi kupitia simu zao kuwezesha kuingia kwenye mfumo wa ODS, ” amesema.

Akizungumzia kuhusu ujazaji fomu za tamko la Maadili kwa njia ya mtandao, Kipacha amesema Ofisi hiyo pia imeanza kutumia mfumo huo kuendana na mabadiliko ya sayansi na Teknolojia (ODS)kuwezesha viongozi ambao hawatapata muda wa kufika kwenye ofisi hizo kujaza kwa njia ya mtandao.

Amesema mfumo huo utaondoa uwezekano wa kupokea matamko kutoka kwa watumishi ambao sio viongozi kwa mujibu wa sheria na kwamba kila kiongozi atakayejaza tamko atakuwa ametengenezewa akaunti kutoa nafasi ya kupokea matamko ya viongozi wanaowajibika na sheria ya Maadili na si vinginevyo.

Pamoja na mambo mengine ameeleza kuwa ikiwa ni idara ya Umma inayojitegemea lengo lake ni kuhakikisha masharti ya sheria ya Maadili ya viongozi wa Umma inazingatiwa ipasavyo kwa mujibu wa sheria Na. 13 ya mwaka 1995 kupitia kifungu cha 19 cha sheria inayoipa wajibu wa kupokea taarifa na tuhuma za ukiukwaji wa Maadili ya viongozi hao.

Majukumu mengine ni pamoja na kuchunguza tuhuma za ukiukwaji wa Maadili ya viongozi wa Umma,kupokea matamko ya Rasilimali na madeni yanayotakiwa kutolea na viongozi, kufanya uhakiki wa matamko kwa mujibu wa sheria, kuanzisha na kufanya uchunguzi wowote wa tuhuma za ukiukwaji wa Maadili yaliyo bainishwa na sheria, kutoa elimu ya Maadili kwa viongozi na kufanya tafiti za hali ya Maadili nchini.

By Jamhuri