Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimeitaka serikali kuchukua hatua za haraka kuhakikisha umeme wa uhakika unapatikana ndani ya muda mfupi.

Pia kimetoa wito kwa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kupanga ratiba ya matengenezo ya mitambo ya kuzalisha umeme kwa kuzingatia sayansi ya mabadiliko ya tabianchi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 19, 2024, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk Anna Henga amesema tangu mwaka 2022 kumekuwa na changamoto ya kukatika katika kwa umeme bila taarifa rasmi kutoka Tanesco.

Amesema pamoja na jitihada za serikali za kutatua changamoto za upungufu wa umeme nchini ni muhimu kuweka mikakati madhubuti ya kutafuta utatuzi wa kudumu wa upungufu wa umeme.

“LHRC inatoa tamko hili kwa lengo la kuikumbusha serikali kuwa tatizo la kukatika kwa umeme linaathiri haki mbalimbali za kikatiba ikiwemo Ibara ya 22 na 23 inayobainisha haki ya kufanya kazi na kujipatia ujira, Ibara ya 14 haki ya uhai kwa kupata afya bora, na Ibara ya 18 haki ya kupokea na kutoa taarifa.

“Tatizo la kukatika kwa umeme Tanzania limekuwa ni suala linalojirudia mara kwa mara mbali ya kuwepo kwa utajiri wa vyanzo mbalimbali vya uzalishaji ikiwemo gesi asilia inayozalishwa Mtwara na Lindi katika maeneo mbalimbali ikiwemo Songo Songo, Mnazibay, Msimbazi na Madima,” amesema Dk Henga.

Amefafanua kuwa, Tanzania ina utajiri mkubwa wa vyanzo mbalimbali vya kuzalisha umeme, hivyo kuendelea kwa mgao wa umeme kumesababisha usumbufu kwa wananchi hususani katika shughuli za kila siku za maisha kama vile uzalishaji, biashara, huduma za afya na elimu.

“Mbali na changamoto zote hizi wanazopitia watanzania hakuna mtu aliyewajibika kwa ukosefu wa umeme, wakati serikali ilishatoa ahadi ya kuhakikisha umeme unapatikana 2024. Jambo hili limeendelea kuleta hali ya sintofahamu ikilingalishwa na utajiri wa rasilimali na maliasili za vyanzo vya kuzalisha nishati ya umeme,” ameongeza Dk Henga.