Na Isri Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Wakati mashabiki na wadau wa mchezo wa ngumi nchini wakiendelea kushinikiza kutaka pambano kati ya mabondia Twaha Kiduku na Hassan Mwakinyo liandaliwe ili kumaliza utata wa nani ni bingwa wa mwenzake, Kiduku ameibuka na kufichua kuwa kuna promota alijitokeza kutaka kuandaa pambano hilo lakini Mwakinyo ametaka kiasi kikubwa cha kuanzia cha sh. bilioni ili akubali kupigana.

Kiduku amesema promota huyo alikuwa tayari kuwalipa kila mmoja milioni 250 za Kitanzania lakini mwenzake amekataa akitaka kiasi hicho ambacho kimemshinda promota.

Kiduku amesema amechoshwa na vita ya maneno mitandaoni ambayo mpaka sasa Mwakinyo ndiye mshindi hivyo anamtaka akubali kusaini ili wapigane ili apatikane na mshindi wa ulingoni.

“Tunaonekana kama mabondia waimba taarab kurushiana maneno mitandaoni, yeye akubali kusaini tu, pambano likachezwe kwao Tanga, baada ya hili pambano kuna mmoja atashuka na mwingine atapanda, ninachotaka ni tupigane tu, Watanzania wamechoka maneno maneno” amesema Kiduku.

Umekuwa wimbo wa muda mrefu wa kutaka mabondia hawa ambao wanaonekana kuwa mahasimu wapande ulingoni ili kukata kiu ya wadau na mashabiki wao.

By Jamhuri