LINI WATATHAMINIKA

1: Japo wao ndo walezi, thamani yao ni ndogo,
Hufanyishwa ngumu kazi, kuzidi punda mdogo,
Wengi hutokwa machozi, ya kulemewa mizigo,
Mama zetu vijijini, lini watathaminika?

2: Masaa kumi na mbili, mama anachapa kazi,
Lile jua lote kali, lamuishia mzazi,
Uko wapi uhalali, baba kutofanya kazi?
Mama huzalisha mali, lakini hanufaiki.

3: Kweli wanasulubika, kwa hizi adhabu kali,
Muda mwingi hutumika, kutuzalishia mali,
Tena hata wakichoka, maji huyafwata mbali,
Yao mengi maumivu, nani wa kuyapooza?

4: Masika ye ni shambani, mazao kupalilia,
Akisha rudi nyumbani, analea familia,
Ataingia jikoni, chakula kuipikia,
Hapo huanza safari, kwenda kutafuta maji.

5: Mbaya zaidi ni hii, yakisha vunwa mazao,
Yeye hatumsikii, akiwa kwenye mgao,
Japo ni yake bidii, ndiyo imekuwa ngao,
Mavuno mali ya mume, mila zimehalalisha.
6: Pia kwenye uongozi, wanaume wamejaa,
Kwenye mbalimbali ngazi, huu ni unyanyapaa,
Ni wa wazi ubaguzi, na tena usiofaa,

Ukweli mama ni nguzo, iko wapi thamaniye?

7: Maswali najiuliza, kwani amekosa nini?
.Nani wa kumliwaza, mwanamke kijijini?
Mbona tunampuuza, ni kama hana thamani?
Mama yangu kijijini, mbona anadharirishwa?

8: Mama anavyoonewa, jama yatia uchungu,
Ni lini atatetewa, huyu mkombozi wangu?
Aache kudhulumiwa, iwe tamu ilo chungu,
Ninamtetea mama, kwani yeye ndiye nguzo.

9: Nimefikia ukomo, kalamu chini naweka,
Na kwenu yawe ni somo, yote niloyaandika,
Usijekuja mgomo, jamii ikaanguka,
Mwanamke kijijini, tumfikirie upya.
Mwalimu Tobias Siwingwa (Msakatonge)

0755721609

Mwisho

By Jamhuri