NA AGUSTINO CLEMENT, TUDARCO
DAR ES SALAAM

Chama cha Kutetea Abiria Tanzania
(Chakua) kimesema kimekuwa na wakati
mgumu wa kutimiza majukumu yake ya
kutetea haki za abiria kutokana na kukosa
ruzuku kutoka serikalini.
Chakua imekuwa ikiahidiwa na serikali
kupata ruzuku hiyo kupitia Mamlaka ya
Usimamizi wa Usafiri wa Nchi Kavu na
Majini (Sumatra) kwa muda mrefu lakini
utekelezaji huo umekuwa ukilegalega, hivyo
kuathiri mikakati ya chama hicho.
Akizungumza na Gazeti la JAMHURI,
Mwenyekiti wa Chakua Taifa, Hassan
Mchanjama, anasema moja ya majukumu
ya chama hicho ni kuhakikisha abiria
wanapewa haki zao za msingi wanapokuwa

safarini.
Mchanjama anasema pamoja na ukosefu
wa fedha na vifaa vya kufanyia kazi ikiwemo
magari ambayo yatawawezesha kuwahi
sehemu ambazo abiria wamepatwa na
matatizo ni baadhi ya changamoto
wanazokabiliana nazo.
Mwenyekiti huyo anasema Sumatra
wamekuwa wakiwasaidia katika utekelezaji
wa baadhi ya majukumu ambayo
yanahusisha utoaji wa elimu kwa wananchi
ambao ndio abiria wanaotumia vyombo
mbalimbali vya usafiri na kuandaa
machapisho lakini bado msaada huo
hautoshelezi.
Mchanjama anasema haki zinazopaswa
kuzingatiwa na wamiliki wa vyombo vya
usafiri nchini ni pamoja na abiria kulipa nauli
halali iliyotangazwa na serikali, kulipwa fidia
baada ya kupata madhara katika ajali na
kusafiri na mzigo wenye uzito wa kilo 20
bure.
Anasema haki nyingine za abiria ni kupata
mahitaji muhimu pindi chombo cha usafiri
kinapoharibika au kuchelewesha abiria, na

abiria kuchagua chombo cha usafiri
anachokitaka yeye mwenyewe.
Mwenyekiti wa Chakua anasema ni haki ya
abiria kupewa tiketi baada ya kulipa nauli
ikiwa ni mkataba kati ya abiria na mmiliki wa
chombo cha usafiri, ikiwa ni pamoja na
kupewa elimu na ratiba ya safari mpaka
mwisho wa safari.
Akifafanua kuhusu haki za abiria kupata
mahitaji muhimu pindi chombo cha usafiri
kinapoharibika au kuwachelewesha abiria,
anasema abiria wana haki ya kupewa
chakula na sehemu ya kulala.
“Ikitokea chombo cha usafiri kikaharibika,
usipite muda wa saa mbili kabla abiria
hawajaanza safari na kama chombo hicho
kikishindwa kuendelea na safari abiria
wabadilishiwe chombo kingine
kitakachokuwa na ubora na hadhi sawa na
usafiri waliokuwa nao tangu mwanzo.
“Wamiliki wa vyombo vya usafiri wana
wajibu wa kuwapa fidia majeruhi kama
ikitokea ajali na kusababisha vifo vya abiria,
ndugu wa marehemu wanalipwa fidia,

anasema Mchanjama.
Ametoa wito kwa abiria wanaokwenda

katika ofisi za Chakua kutoa taarifa za
madhara ya ajali walizopata kwamba
waende na fomu za PF 3, PF 90, nakala za
hukumu za kesi zinazohusu ajali, mchoro
wa ajali, taarifa ya ajali na leseni ya dereva.
Mchanjama ameliambia Gazeti la JAMHURI
kuwa malalamiko ambayo wamekuwa
wakipokea kutoka kwa abiria ni
upandishwaji wa nauli hasa vipindi vya likizo
kwa wanafunzi, sikukuu za mwisho wa
mwaka na kuchelewa kwa safari kutokana
na sababu mbalimbali ikiwemo ubovu wa
chombo cha usafiri na abiria kupewa tiketi
feki.
Anasema Chakua inahakikisha haki za
abiria nchini zinatekelezwa kwa kuwa ofisi
za chama hicho zipo katika mikoa yote
nchini kuanzia ngazi ya taifa, kanda, mkoa
na wilaya.
Chakua imegawanyika katika kanda kuu
tano, ambazo ni Kanda ya Mashariki
ambayo makao makuu yake ni Dar es
Salaam na mikoa ya Lindi, Mtwara,
Morogoro na Pwani; Kanda ya Kaskazini
inayojumuisha mikoa ya Arusha, Manyara,
Kilimanjaro na Tanga, ambapo makao

makuu yake ni Arusha.
Vilevile kuna Kanda ya Ziwa inayojumuisha
mikoa ya Mwanza, Kagera, Simiyu, Geita,
Katavi, Shinyanga na Mara, huku makao
makuu yakiwa ni Mwanza. Pia kuna Kanda
ya Nyanda za Juu yenye mikoa ya Mbeya,
Iringa, Njombe, Rukwa na Songwe ambapo
makao makuu ni Mbeya.

Mwisho

Please follow and like us:
Pin Share