NA MICHAEL SARUNGI,
DAR ES SALAAM

Serikali imetangaza kuanza kutumika kwa
sheria mpya ya udhibiti wa uzito wa magari
ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (East Africa
Vehicle Load Control Act, 2016) kuanzia
Januari mwakani ili kukabiliana na uharibifu
wa barabara pamoja na majanga mengine.
Akizungumza na wadau wa sekta ya ujenzi
katika mkutano uliofanyika mjini Dodoma
hivi karibuni, Katibu Mkuu wa Wizara ya
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,
anayeshughulikia sekta ya ujenzi, Mhandisi
Joseph Nyamhanga, anasema sheria
hiyo ina masharti na adhabu kali kwa
makosa ya kuzidisha uzito wa magari na
makosa mengine ya usafirishaji.
Anasema baadhi ya mambo mapya
yaliyomo kwenye sheria hiyo mpya ni
ukomo wa uzito wa mtaimbo (axle) wenye

matairi mapana (Super Single Tyres)
utakuwa tani 8.5 badala ya tani 10 za sasa.
Mhandisi Nyamhanga anasema kutakuwa
na mfumo wa kuweka kumbukumbu za
makosa ya msafirishaji kwa anayezidisha
uzito (Demerits Point System) ambao
hatimaye unaweza kusababisha gari
kufungiwa kufanya usafirishaji kwa muda au
moja kwa moja.
“Kutakuwa na adhabu kwa makosa ya
usafirishaji hadi ukomo wa dola za Marekani
15,000 (sawa na Sh milioni 34) au kifungo
kisichozidi miaka mitatu (3) au vyote kwa
pamoja, adhabu hizo zitawahusu watumishi
wa mizani wanaokula njama na wasafirishaji
kwa kukwepa kulipa tozo ya kuzidisha
uzito,

” anasema Mhandisi Nyamhanga.

Anasema gharama za kutunza (detention)
gari lililokuwa na makosa katika maeneo ya
mizani baada ya siku tatu kupita ni dola za
Marekani 50 kwa siku badala ya dola 20
kwa siku kwenye sheria ya sasa.
Gharama ya kuegesha gari (Parking Fee)
ndani ya eneo la mizani baada ya kulipa
tozo ya kuzidisha uzito (overloading fees) ni
dola za Marekani 50 kwa siku na kuongeza
kuwa kwa kiasi kikubwa sheria hiyo
inafanana na sheria iliyopo sasa.

Kuanza kutumika kwa sheria hiyo kwa nchi
wanachama wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki (EAC) kumefanyika kupitia
tangazo lililochapishwa kwenye Gazeti la
Jumuiya ya Afrika Mashariki Novemba 18,
mwaka juzi na kupitishwa kwa kanuni zake
mwaka jana.
Nyamhanga anasema moja ya sababu za
kuharibika kwa barabara ni matumizi ya
mitaimbo (axle) yenye matairi mapana
(Super Single Tyres) kubeba uzito sawa na
matairi mawili ya kawaida (Dual Tyres).
Anasema kutokana na hali hiyo serikali
imeona umuhimu mkubwa wa wadau
kushirikiana kwa pamoja kuzilinda barabara
zilizojengwa kwa gharama kubwa kwa
kudhibiti uzito wa magari ili ziweze kudumu
kwa muda mrefu.

Mwisho

Please follow and like us:
Pin Share