Na William Bhoke

Kwa uhalisia wake, bado Watanzania
hatujajitambua, Watanzania tumekuwa
kama mbuzi wa kiangazi. Mbuzi wa kiangazi
wanazunguka kutwa nzima pasipo kuelewa
wanaelekea wapi.
Imepita takriban miaka 54 tangu taifa hili
kupata uhuru, lakini cha ajabu ni kwamba
bado taifa linachechemea katika huduma za
kimaendeleo. Nchi yetu inahitaji mabadiliko
kama vile mtu aliyekabwa koo anavyohitaji
hewa ya oksijeni.
Huyu mtu akicheleweshwa kwa muda mrefu
atakufa, akicheleweshwa sana lakini si kiasi
cha kumuua, anaweza kuibuka akiwa na
ubongo ulioumizwa, hataweza kufikiri vema
kama awali.
Tumekuwa taifa gonjwa lisilokuwa na akili
za ubunifu wa kugundua na kuendeleza
tulivyo navyo.

Mtanzania ukimwambia hii ni rangi nyeusi,
anakubali ndiyo ni rangi nyeusi pasipo
kuhoji kwa nini ni rangi nyeusi, nini
kimeifanya kuwa rangi nyeusi.
Mtanzania ukiambiwa Taifa la Marekani
limeendelea kiuchumi, kidemokrasia na
kielimu unakubali; “Ndiyo Marekani wako
juu kuliko sisi.” Haujiulizi, kwa nini Marekani
wako juu kuliko sisi?
Leo hii Mtume Paulo angekuwa nasi
Watanzania angeweza kutuuliza lile swali
alilowauliza Wagalatia: “Enyi Walagatia ni
nani aliyewaroga?” Nasi twaweza kujiuliza:
“Watanzania nani ameturoga?’’
Ni hakika, Watanzania hakuna aliyeturoga,
tumejiroga wenyewe. Watanzania tunaishi
maisha yasiyo na utafiti, huo ni msalaba wa
kujitengenezea. Tunapenda majibu mepesi
kwa maswali magumu, huo ni msalaba wa
kujitengenezea. Hii ni misalaba. Tuitue.
Ni Tanzania, kiongozi akiwa anawania
nafasi ya uongozi anakwenda kwa waganga
wa kienyeji kutafuta nyota ya mvuto,
anaona elimu aliyopata haijampa uwezo wa
kujieleza na kujenga hoja na jamii
ikakubaliana na hoja yake.

Tumefika mahali tunaamini kupata utajiri
mpaka kuiba au kujiunga na mtandao wa
kishetani (Freemason). Hii ni dhana kuntu
inayohitaji kuondolewa kutoka kwenye
bongo za Watanzania.
Ni ajabu sana, kwa upande mwingine
mantiki ya kifalsafa inaninong’onezea ukweli
kwamba, umaskini wa Watanzania ni
chaguo la Watanzania wenyewe. Adui wa
Tanzania yupo Tanzania.
Adui huyu binafsi ninamfahamu kwa majina
ya “Fikra zisizofikiri kwa usahihi, fikra zilizo
lala, fikra zilizokosa mbolea.”
Watanzania tuko huru, lakini hatuko huru
kwa upande wa kifikra. Ni katika mazingira
haya tunaendelea kuzalisha kizazi
kisichokuwa na maono ya kulijenga taifa.
Utafiti uliofanywa mwaka 2010 na asasi ya
Marekani inayoitwa PEW Research Centre
ulibaini na kuonyesha kwamba asilimia 93
ya Watanzania wanaamini katika ushirikina.
Yaani miongoni mwa nchi 19 za Afrika
ambako utafiti huo ulifanyika, Tanzania
ilishika nafasi ya kwanza ikifuatiwa na
Cameron yenye asilimia 78. Hii ni aibu
kubwa.

Watanzania watakuwa mashuhuda kwa kile
kilichotokea kwa ‘Babu’ wa Loliondo,
alijizolea umaarufu kwa kile alichodai
kwamba ameoteshwa na Mwenyezi Mungu
dawa inayotibu ukimwi.
Wasomi wetu na wasiosoma waliibukia kwa
babu kupata kikombe na viongozi wetu pia
waliibukia kwa babu kupata kikombe.
Tunao madaktari waliosoma, lakini
hawakutoa tamko lolote kuhusu kikombe
cha babu. Haishangazi sana kila kona
tunakopita tunakutana na vibao barabarani
vya waganga wa kienyeji.
Matangazo yao utaona yanasomeka hivi:
Dk. bingwa kutoka Congo anatoa huduma
zifuatazo:
Kumrudisha mpenzi wa zamani.
Kuongeza nguvu za kiume.
Kuongeza akili za darasani.
Kumsahaulisha mdai wako.
Kuongeza mvuto kwa warembo.
Kupandishwa cheo kazini.
Kama kuna taifa lenye visa na mikasa, basi
Tanzania tunaongoza kwa visa na mikasa.
Tanzania tumekuwa taifa la kishirikina.
Dunia ya leo haina lelemama kwa binadamu

yeyote. Yeyote anayeonyesha hana nguvu
na akili ya kustahimili vishindo ndani ya
dunia hii, dunia itamtupilia mbali.

<<<<<< Itaendelea>>>>

Please follow and like us:
Pin Share