Waziri Mkuu (mstaafu), Edward Lowassa, aliyekuwa mgombea wa ushirikiano wa kisiasa wa vyama vya upinzani, maarufu kwa jina la Ukawa, amerejea CCM wiki iliyopita akitokea Chadema, ametoa neno zito.

Wakati watu wengi wakijiuliza imekuwaje Lowassa, mwanasiasa aliyetoa changamoto kubwa kwa Chama tawala  CCM ameamua kuhama upinzani kurejea CCM, majibu sasa yameanza kujitokeza kuwa Lowassa ni mfia nchi.

“Mzee amesema yeye katika vyote, nchi anaitanguliza kwanza katika kila uamuzi anaoufanya. Ndiyo maana amekuwa na siasa za kistaarabu miaka yote. Hataki vurugu, hataki misuguano, bali anataka kila jambo lifanikiwe kwa kujenga hoja na kueleweka,” Abubakar Liongo, ambaye ni Msemaji wa Lowassa ameliambia JAMHURI mwishoni mwa wiki.

JAMHURI limekutana na Lowassa jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki ambaye awali aliihama CCM Juni 29, 2015 akaenda Chadema na kurejea CCM Machi Mosi, 2019. Amesema kwa sasa hataki kuzungumza lolote kuhusu Chadema au upinzani, isipokuwa kama lipo jambo la kusema atalizungumza kupitia taarifa rasmi itakayotolewa na msemaji wake, Liongo.

Liongo alipotafutwa, akasema: “Kwa sasa Rais John Magufuli anajenga reli ya kisasa. Umeme wa uhakika Stiegler’s Gorge, amepambana na rushwa na anajenga misingi imara ya viwanda, hali itakayoinua maisha ya wananchi. Mzee [Lowassa] ameona ni wakati mwafaka kushirikiana na Rais Magufuli kujenga nchi imara kwa kushirikishana mawazo, badala ya kuendeleza mivutano ya kisiasa,” amesema.

Lowassa ambaye akiwa mgombea wa Ukawa alipata kura 6,072,848 sawa na asilimia 39.97 ya kura zilizopigwa katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, ambazo ni nyingi kuliko mgombea yeyote wa upinzani tangu siasa za vyama vingi zianze nchini, inaelezwa kuwa anataka kuona Tanzania inaondoka katika lindi la umaskini.

“Mwacheni mzee apumzike. Mwache akatoe mawazo yake huko CCM alikosema ‘anarudi nyumbani’. Huyu ni mzee wa amani. Idadi ya kura alizopata wangezipata hawa waliomtangulia ‘midomo juu’ wangeita watu kuandamana barabarani wakidai wameporwa ushindi. Lakini yeye alikaa kimya. Ni mzee wa busara. CCM na Rais Magufuli wamefanya vema kumpokea, akiwashauri wakamsikiliza nchi itasonga, maana yeye anafahamika kwa kuwaza na kufanya uamuzi,” amesema mwanasiasa mkongwe ndani ya CCM.

Mtu aliyeko karibu na Lowassa ameliambia JAMHURI: “Kuna watu ndani ya CCM hawakumwelewa mzee Lowassa. Walikuwa wanamwogopa na ndiyo maana wakajaribu kila njia kuchafua jina lake, mara kusema wanajivua gamba, wengine wakampachika majina ya ajabu, lakini nia yao ilikuwa ni kuharibu jina lake.

“Mbaya zaidi walipofika mwaka 2014 wakaanza hofu. Wakadhani Lowassa anataka kugombea urais kulipa kisasi kwa waliyomtendea. Hapo walitumia kila nguvu waliyokuwa nayo. Iwe ni kumchafua mitandaoni au kupitia mlango wa siasa walitenda.

“Hawakutaka kukiri ukweli kwamba wazo la kujenga Chuo Kikuu cha Dodoma lilitokana na yeye. Hawakutaka kukiri ukweli kwamba akiwa Waziri wa Maji alikwenda safari ya kihistoria Misri mwaka 2004 na kukutana na Waziri wa Maji, Dk. Mahmoud Abu Zeid, akajenga hoja Tanzania ikapata haki ya kutumia maji ya Ziwa Victoria yanayotumika Shinyanga na Kahama sasa… mradi wa maji pale Wami – Chalinze na mambo mengine mengi yaliwatia hofu.

“Kabla ya kurejea CCM ameniambia ameona Rais Magufuli ana mwelekeo wa kusaidia nchi hii kutoka katika umaskini. Ameniambia haoni sababu ya kuwa mbinafsi, hivyo ni bora ashirikiane na Rais Magufuli kutoa mawazo yatakayoimarisha elimu, afya, maji, miundombinu, viwanda nchini… unakumbuka alivyopambana kuhakikisha shule za sekondari za kata zinajengwa? Shule hizi mwanzo walizibeza, lakini sasa ndizo mkombozi,” amesema mtu aliyeko karibu na Lowassa aliyeomba asitajwe jina.

Januari 9, mwaka jana Lowassa alikutana na Rais Magufuli Ikulu, Dar es Salaam na akampongeza kwa kazi nzuri anayoifanya, akisema: “Nimepata faraja sana kuja hapa Ikulu kuonana na Mhe. Rais, tumezungumza naye na nimempongeza kwa kazi nzuri anayoifanya, lazima tukiri anafanya kazi nzuri na anahitaji kutiwa moyo.”

Lowassa aliongeza: “Moja kubwa ambalo ni la msingi sana ni la kujenga ajira, katika kuanza ujenzi wa reli ya kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro hapo anajenga ajira.

“Na kwenye nchi yoyote inayoendelea suala muhimu ni kujenga ajira, Stiegler’s Gorge ni kujenga ajira na miradi mingine ya aina hiyo, lazima kuwepo na kipaumbele cha kusema kwamba tunajenga ajira, jingine ni la elimu, ni muhimu sana, huwezi kuacha elimu katika mambo yako unayofanya, hili nalo lazima lisemwe vya kutosha, kwa kweli nakushukuru Mhe. Rais, you made my day.”

Kwa upande wake, Rais Magufuli alisema Lowassa ni mwanasiasa mzuri kwani hata wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu uliopita ambao naye aligombea kiti cha urais, hakuwahi kumtukana.

Amemshukuru “…kwa kutambua kazi kubwa inayofanywa na serikali… tumezungumza mambo mengi, ameniambia ya kwake na mimi nimemwambia ya kwangu, kwa ujumla Lowassa ni mwanasiasa mzuri na tuendelee kuwaenzi wazee hawa ambao kwa nyakati fulani walifanya mambo mazuri, na mimi napenda kumpongeza Lowassa ambaye kama alivyosema hapa kuwa tumefanya mambo mazuri mengi.”

Gwajima, Membe wanena

Akizungumza na Gazeti la JAMHURI, Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, anasema kimsingi jambo alilolifanya aliyekuwa mgombea wa Ukawa, Edward Lowassa, ni sawa na kusema kila kizazi na muziki wake.

Gwajima anasema, mwanasiasa yeyote huangalia zaidi fursa na akiona mahala ambapo masilahi yake yanatimizwa huko ni sahihi kwake kuhamia.

Wakati Lowassa anahama kutoka CCM kwenda Chadema, Gwajima alitajwa kuwa mtu muhimu ambaye alishawishi mawazo ya mwanasiasa huyo kutimkia upinzani. Gwajima ameliambia JAMHURI kwamba Lowassa alimwambia kwamba anarudi CCM.

“Lowassa ni rafiki yangu ila hilo la kuniarifu… aliniambia. Niliongea naye nikamwambia kwamba yeye ni mwanasiasa na mimi ni mtumishi wa Mungu… Siasa zinabadilika kulingana na mazingira,” anasema Gwajima.

Wakati Lowassa akihama na kurudi kwenye Chama Cha Mapinduzi, uchunguzi wa JAMHURI umebaini kwamba atafuatwa na baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu ya Chadema.

“Unajua hapa ni suala la muda tu, ila nakuhakikishia kwamba kuna vigogo kutoka Kamati Kuu ya Chadema wapatao watano watamfuata Lowassa CCM,” kimesema chanzo chetu.

Akizungumza na Gazeti la JAMHURI, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa mstaafu, Bernard Membe, anasema suala la Edward Lowassa kurejea CCM lilitarajiwa.

Membe anasema baada ya Lowassa kurejea CCM kinachosubiriwa ni kumezwa kwa CCM mpya, baada ya muda mfupi haitakuwepo. Anasema Chama Cha Mapinduzi kimekuwa na ajenda nyingi kwa wakati mmoja.

“Kote duniani lengo la kila chama cha siasa ni kushinda uchaguzi na kushika dola, si kuua ama kudhoofisha vyama vya upinzani. Kinachoendelea kwa sasa ni kuua vyama vya upinzani,” anasema Membe.

Katika hatua nyingine, akizungumzia ujio huo wa Lowassa CCM, Mkuu wa Mkoa wa Njombe ambaye amewahi kuwa Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka, ambaye awali akikwaruzana na Lowassa ndani ya CCM akijinasibu na kundi la mitume 12, amesema: “Tunamkaribisha kushirikiana nasi katika kuijenga nchi.”

Kwa mujibu wa Sendeka, ujio wa Lowassa tena katika CCM ni fursa nzuri ya kuimarisha sauti ya chama hicho tawala mbele ya wananchi.

“Kwa wanasiasa makini hakuna namna isipokuwa kumuunga mkono Rais Dk. John Magufuli kwa kuwa anafanya kazi nzuri kwa manufaa ya taifa hili, sisi wasaidizi wa Rais Magufuli tunajua uchungu alionao katika kuwatumikia Watanzania, naamini Lowassa amefanya uamuzi mzuri sana,” amesema Sendeka.

Mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Kasheku, maarufu kama ‘King Msukuma’, amezungumza na JAMHURI akasema amefurahishwa na ujio wa mzee Lowassa ndani ya CCM.

Kasheku ambaye miaka michache iliyopita alimtolea Lowassa maneno makali yaliyokuwa na sura ya kudhalilisha, amesema mchezo wa siasa unanoga kadiri wakati unavyopita.

“Tena nakwenda Bukoba kwenye mazishi ya Ruge, niko safarini hivi sasa. Nakuhakikishia mzee Lowassa akifika nitamkumbatia na kumbusu. Huyu kwake ni huku CCM, kama walimkosea wakamuudhi kwa hasira akapotea njia, sasa ameipata njia sahihi kwa kurejea nyumbani,” amesema Kasheku.

Baadhi ya viongozi waliohojiwa akiwamo Frederick Sumaye, James Mbatia, Dk. Vincent Mashinji na wengine wamesema kuondoka kwa Lowassa hakuwezi kuua upinzani, japo wamesema alistahili kuondoka baada ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, kuachiwa kutoka gerezani.

Nguvu za Lowassa Ukawa

Kati ya mambo yanayodhihirisha nguvu za kisiasa za Lowassa ni pamoja na kufanikisha Ukawa kuweka rekodi ya aina yake kwa wingi wa idadi ya wabunge tangu kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa vyama vingi mwaka 1995.

Katika uchaguzi wa 1995 ambao Lowassa alikuwa mgombea urais anayeungwa mkono na Ukawa, alifanikisha upinzani kupata jumla ya wabunge 116 kuingia katika Bunge la 11 lililoanza kazi Novemba 17 mwaka 2015.

Kwenye uchaguzi huo mkuu majimbo 258 kati ya 262 yalifanya uchaguzi na matokeo yalionesha kuwa CCM ilishinda ubunge katika majimbo 188, Chama cha Wananchi (CUF) 35, Chadema 34, NCCR–Mageuzi kiti kimoja – vyama hivi vilikuwa sehemu vya vyama vilivyomuunga mkono Lowassa kwenye urais na hivyo kufaidika na nguvu zake za kisiasa.

Hata katika idadi ya wabunge wa viti maalumu, upinzani ulifaidika kwa wingi wa idadi, Chadema ikipata viti 36, CUF 10 na CCM viti maalumu 64.

Kwa hesabu hizo, Chadema ilikusanya jumla ya wabunge 70  kutoka 48 wa mwaka 2010, CUF wabunge 45 kutoka 36 wa mwaka 2010 lakini NCCR-Mageuzi ikishuka kutoka wabunge wanne wa 2010 hadi mmoja na kufanya idadi ya wabunge wa Ukawa kuwa jumla 116.

By Jamhuri