Mwishoni mwa mwaka jana Mpita Njia (MN) alisoma kwenye vyombo vya habari ahadi aliyopewa Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Rais John Magufuli.

MN anakumbuka vema kuwa ahadi hiyo ilitolewa na ‘wakubwa’ waliokuwa kwenye ziara mkoani Mara, na kituo kilichohusika kilikuwa cha Wilaya ya Butiama.

Kwenye Uwanja wa Mwenge kijijini Butiama, watendaji wa Wizara ya Ujenzi, kwa mbwembwe nyingi wakamhakikishia kiongozi mkuu wa nchi kwamba ile Barabara ya Makutano – Butiama – Nyamuswa hadi Fort Ikoma ujenzi wake ulikuwa ukiendelea vizuri sana.

Akahakikishiwa kuwa kile kipande cha Makutano – Butiama – Nyamuswa kingekuwa kimeshawekwa lami ifikapo Februari, 2019!

MN aliposikia tambo hizo akajiinamia; maana aliamini ni miujiza pekee ambayo ingewawezesha makandarasi kumaliza kazi hiyo ngumu kwa muda huo.

Kweli, juzi MN amepita eneo hilo kuona maendeleo ya kazi. Alichokiona ni sifuri kabisa. Acha lami, lakini hata kujaza udongo tu (tuta) kwenye barabara hiyo kuanzia Butiama, Busegwe, Butuguri hadi Makutano – hakuna kitu. MN anadhani huu ni mwaka kama wa saba barabara hii inaimbwa. Imedumaa. Hakuna kinachoendelea.

Ndiyo maana anauliza, ujasiri huu wa kumhadaa mkuu wa nchi hawa viongozi wetu wanautoa wapi? Kulikuwa na shida gani kumweleza kuwa barabara ile haitakamilika labda hadi mwaka 2025?

Kama kuna kitu kilichojitokeza hapo katikati hata barabara hiyo ikawa imekwama kwa kiasi hicho, kwanini waliomdanganya mkuu wa nchi hawajitokezi kueleza sababu za huo mkwamo? Na je, yale magema waliyoyachonga na kuziba kabisa njia za mchepuko kijijini Butiama lini yatasawazishwa?

MN hapendi kuchuria watu, lakini anadhani kama yule mama aliyemdanganya mkubwa kuhusu kutokuwapo watumishi hewa mkoani kwake alitumbuliwa, hawa wengine waliomdanganya hadharani mchana kweupe nini kinawanusuru?

Mpita Njia anahoji, kama watendaji wanaweza kumweleza mkuu wa nchi maneno  yasiyo ya kweli, tena mita chache kutoka kwenye kaburi la ‘mwenyeheri’, itakuwaje wakiwa maeneo ya mbali? Kwa kuwa mkuu wa nchi anavyo vyombo vya kumpatia taarifa sahihi, ebu avitumie vimpe maneno na picha ya hali ilivyo kwenye barabara ile. Wakimfikishia yaliyo ya kweli, MN anaamini bosi ‘atakufa na mtu’, maana huwa hapendi kudanganywa – na ndiyo maana hupenda kurejea “msema kweli ni mpenzi wa Mungu.”

Please follow and like us:
Pin Share