Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia

Edward Lowassa ni Waziri Mkuu wa zamani wa Tanzania aliyehudumu katika nafasi hiyo kati ya Desemba 30, 2005 na Februari 7, 2008 wakati wa uongozi wa awamu ya nne wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete.

Lowassa alizaliwa Agosti 26, 1953 Wilayani Monduli mkoni Arusha akiwa mtoto wa nne wa mfugaji Ngoyai Lowassa ambaye alifanya kazi kwa muda wa ziada akiwa tarishi katika serikali ya kikoloni.

Edward Lowassa alipata elimu ya msingi katika shule ya msingi Monduli ambayo baadaye ilibadilishwa jina na kuitwa Moringe kati ya mwaka 1961 na 1967.

Baada ya elimu ya msingi alijiunga na masomo ya sekondari katika shule ya sekondari Arusha kuanzia mwaka 1968 alikohitimu kidato cha nne mwaka 1971.

Hakuishia hapo kielimu, kwani alijiunga na shule ya sekondari Milambo mkoani Tabora kwa ajili ya masomo ya kidato cha 5 na 6 kati ya mwaka 1972 na 1973 alipohitimu.

Mwaka 1977, Lowassa alifuzu na kutunukiwa shahada ya awali ya Sanaa za Maonesho kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Akiwa UDSM, ndipo alikutana na Jakaya Kikwete akisoma Uchumi, na miaka zaidi ya 20 baadaye kuwa Rais wa nne wa Tanzania.

Mnamo mwaka 1978, Lowassa alijiunga na jeshi la ulinzi wa wananchi wa Tanzania (JWTZ) na kwenda vitani wakati wa vita vya Kagera, kati ya Tanzania na Uganda vilivyodumu kwa miezi 6 na kumalizika April.1979.

Baadaye mwaka 1984 Lowassa alitunukiwa Shahada ya pili ya Maendeleo kutoka Chuo Kikuu cha Bath cha Uingereza.

Jina la Lowassa lilianza kufahamika zaidi kwa umma baada ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha kimataifa cha mikutano Arusha, (AICC) na baadaye kuteuliwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu wakati wa Uongozi wa Rais wa pili, Ali Hassan Mwinyi.

Alitia nia kuwania kuteuliwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) kugombea urais mwaka 1995, lakini jina lake lilichujwa katika hatua za awali katika mchakato ulimpa ushindi Benjamin Mkapa ndani ya chama na katika uchaguzi mkuu.

Mwaka huo huo 1995 Lowassa alishinda Ubunge wa Monduli kisha mwaka 1998 aliteuliwa na Rais Mkapa kuwa Waziri wa nchi Ofisi ya Mkamu wa Rais akihusika na Mazingira na kupambana na Umaskini.

Baada ya uchaguzi wa mwaka 2000 aliteuliwa Waziri wa Maji. Mwaka 2005 aliamua kumuunga mkono rafiki yake wa miaka mingi, Jakaya Kikwete katika kuwania kuteuliwa na CCM kuwania Urais dhidi ya wagombea wa upinzani. Baada ya Kikwete kupata ushindi mkubwa wa zaidi ya asilimi 80, Lowassa aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa 9 wa Tanzania. Alijipatia sifa kubwa ya uchapakazi hususan ufuatiliaji wa utedaji serikalini.

Hata hivyo, Lowassa alidumu kwenye nafasi ya uwaziri mkuu kwa miaka miwili na mwezi mmoja hivi, pale alipolazimika kujiuzulu kutokana kashfa ya kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Richmond, ambayo kupitia uchunguzi wa Kamati teule ya Bunge iliyoongozwa na mbunge Dkt. Harrison Mwakyembe ilibainika kuwa ililipwa fedha nyingi licha ya utendaji duni uliolenga kuikwamua nchi kutoka kizani.

Hii ilikuwa baada ya ripoti ya Kamati ya uchunguzi ya Bunge kuwasilishwa bungeni, huku Lowassa akilalamika kabla ya kujiuzulu kuwa alikuwa ameonewa na kudhalilishwa sana kwa kutosikilizwa na Kamati hiyo ya Dkt. Makyembe.

Baada ya miaka 7 kupita yaani mwaka 2015, Lowassa alirejea tena katika nia yake ya kuongoza taifa la Tanzania kwa kuomba ridhaa ya CCM, Licha ya umaarufu wake, alichujwa bila kuingia hata tano bora. Uamuzi huo ulisababisha ajitoe CCM na kujiunga na chama cha Upinzani Chadema, kilichomteua kugombea urais wa Tanzania akieleza kuwa ajenda yake kuu ilikuwa kuimarisha elimu. Kila mara wakati wa kampeni za uchaguzi alikuwa akisema vipaumbele vyake vitatu ni elimu, elimu, elimu.

Hata hivyo, alishindwa na mgombea wa CCM John Magufuli, aliyechaguliwa kuwa rais wa 5 wa Tanzania.

Machi 1, mwaka 2019 Lowassa aliachana na CHADEMA na kurejea CCM akipokewa na aliyekuwa mwenyekiti wa CCM wakati huo, John Magufuli.

Tangu Machi 2023, afya ya Lowassa ilielezwa kuteteleka pale ilipotangazwa alikuwa amelazwa huspitalini nchini Afrika Kusini. Tangu wakati huo hapakuwepo taarifa za mara kwa mara juu ya hali ya afya yake hadi kutangazwa kifo chake jana Februari 10, 2024 na Makamu wa Rais Dk Philip Mpango.