Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania (6)

Wiki iliyopita tulikuletea sehemu ya tano ya mtiririko wa maandiko ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere juu ya Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania. Katika kitabu alichokiandika mwaka 1994, Mwalimu alisema: “Ati Chama hakiwezi kupinga Bunge lake, lakini kwa mantiki ya ajabu ajabu wabunge wanaweza kupinga chama chao! Hiyo ndiyo demokrasia halisi ya mageuzi. Nilirudi Butiama nikalipa ada yangu ya CCM na nikaandika utenzi wa Tanzania Tanzania!” Endelea…

Jukumu la kueleza taarifa hii ya Serikali katika Halmashauri Kuu ya Taifa aliachiwa Waziri wa Sheria na Mambo ya Katiba, Mheshimiwa Samuel Sitta. Baadaye, baada ya kikao nilimtafuta Ndugu Sitta, nikampa pole kwa kupewa jukumu la kueleza jambo ambalo halielezeki.

Mapema nilikuwa nimeambiwa kwamba alikuwa ametamka bungeni hapo kwamba hoja ya kudai Serikali Tatu itakapoanza kujadiliwa yeye ataipinga, maana jimbo lake la uchaguzi, Urambo, halikuwa limemtuma kwenda bungeni kudai Serikali ya Tanganyika.

 

Wabunge wote wakweli wangeweza kusema hivyo hivyo. Hata Waziri Mkuu na Katibu Mkuu wangeweza kusema hivyo hivyo. Wao ni wateuliwa na Rais, ambaye alikwishakwenda bungeni siku chache tu zilizopita, na kupinga hoja ya Serikali Tatu. Katika kikao cha usiku wa jana yake nilikuwa nimewakumbusha hivyo viongozi wetu waheshimiwa.


Kutokana na mazungumzo yaliyofuatia niliona kuwa bado tulikuwa tunayo nafasi ya kumaliza mgogoro huu bila madhara makubwa. Niliamini kabisa kwamba Serikali ikiondoa mapendekezo yake kukitaka chama kikubali Serikali Tatu, Halmashauri Kuu ya Taifa itaridhika na wajumbe wake wengi watapumua pumzi za faraja. Na la maana zaidi, nchi yetu itakuwa imeondolewa kwenye ukingo wa shimo la giza.


Nilihisi kuwa tatizo ambalo Rais atapata litatokana na washauri wake, maana wao ndiyo wenye hoja, lakini kwa kuwa yeye ndiye mteuzi wao sikuona kwa nini wawe mgogoro mkubwa. Nilimwambia hivyo na kuahidi kuwa mimi nitakuwa tayari kumsaidia maeneo yale atakayoona kuwa anahitaji msaada wangu.


Naamini kuwa Rais alijaribu, lakini kama nilivyotazamia washauri wake walikataa. Jitihada na hila za kushawishi wajumbe wa Halmashauri Kuu wakubali hoja ya kuwa na Serikali tatu ziliendelea. Hazikufaulu. Halmashauri Kuu ya Taifa ilikataa kubadili sera yake ya Muungano wenye Serikali mbili; jambo ambalo ndilo lililokuwa shabaha ya viongozi wetu waheshimiwa.


Lakini, hata hivyo, walifaulu kuibabaisha Halmashauri Kuu hata ikakubali kupitisha azimio la kutafuta maoni ya wananchi kuhusu suala la Serikali tatu. Mimi niliamini kwamba hili ni kosa. Hivi kila wakati CCM itakapotaka kubadili sera yake itatafuta kwanza maoni ya wananchi? Halmashauri Kuu iliketi Unguja ikabadili Azimio la Arusha bila kwanza kutafuta maoni ya wananchi.


Na walikuwa na haki ya kufanya hivyo maana ni sera yao. Ubaya wao ni kwamba jambo lenyewe walilifanya kwa nia na “janja janja” na mpaka sasa wanaendelea kudanganya wananchi kwamba Sera ya CCM bado ni ya Ujamaa na Kujitegemea. Ndivyo viongozi wetu waheshimiwa wanavyojaribu kufanya hata katika suala hili la Muungano.


Wanataka kuvunja Tanzania maana “wamechoka na Wazanzibari”, lakini hawataki kusema hivyo wazi wazi. Wanachosema ni kwamba wanataka Serikali ya Tanganyika “ndani ya Muungano”, ingawa wanafahamu, maana si watu wapumbavu, kwamba ukifufua Tanganyika utaua Tanzania.


Muundo wa Muungano, pamoja na kwamba hatutaki uwe ukitibuliwa-tibuliwa mara kwa mara, ni suala la sera, si amri ya Mungu. Vyama vya siasa mbalimbali vinaweza vikawa na maoni mbalimbali kuhusu muundo unaofaa kwa Katiba ya Nchi yetu. Muundo utakaokubaliwa na wananchi walio wengi ndiyo utakaokuwa sehemu ya Katiba ya nchi.


Muundo wa Serikali mbili unakubaliwa na wananchi, lakini unatokana na sera ya TANU na ASP, na kwa sasa CCM. Chama Cha Mapinduzi kikipenda kinaweza kubadili sera hiyo ya muundo wa Serikali mbili bila kuuliza wananchi kwanza. Kinaweza kufanya hivyo kwa kuhisi kuwa hivyo ndivyo wananchi wengi watakavyo; lakini pia kinaweza kufanya hivyo kwa sababu kinaamini kuwa inafaa kufanya hivyo, hata kama Wananchi wengi hawakudai au hawapendi mabadiliko.


Pendekezo hili la kutaka Serikali ya Tanganyika lilizushwa kwanza na Tume ya Nyalali, bila madai ya Wananchi. Chama Cha Mapinduzi kikalikataa, kwa sababu nzuri kabisa; lakini kingeweza kulikubali, kama kilivyokubali kuacha Mfumo wa chama kimoja na kuleta mfumo wa vyama vingi, pamoja na kwamba wananchi walio wengi walipenda tuendelee na mfumo wa chama kimoja.


Maoni ya Wananchi yanaweza kukifanya Chama kibadili sera zake; lakini si lazima. Chama chochote kinaweza kubadili sera zake bila kutafuta kwanza maoni ya Wananchi. Siku ya Uchaguzi Mkuu maoni ya Wananchi yatajulikana!


Nasema niliamini kuwa ni kosa kwa Halmashauri kuu ya Taifa kukubali Chama kiulize Wananchi kama inafaa tuwe na Serikali tatu. Kwanza, kwa sababu hiyo niliyoeleza; na pili hata kama CCM ingependa kukubali sera yake, kwa nini turukie Serikali tatu? Kwa nini tusitake maoni ya wananchi kuhusu Serikali moja? Au hata kuhusu Serikali za Majimbo?


Tumejadili katika vikao gani tukakubaliana kuwa miundo mingine yote haifai, ila muundo unaofaa ni ule wa Serikali tatu? Au hata Bunge lenyewe, limejadili miundo mbalimbali ya Muungano katika kikao gani, hata Wabunge waheshimiwa, pamoja na Waheshimiwa Mawaziri wetu, wakafikia uamuzi, baada ya mjadala, kwamba muundo peke yake unaofaa ni huu wanaopendekeza, wa kuwa na Serikali tatu?


Hizi zote ni mbinu tu za viongozi wetu waheshimiwa, kutaka kukiingiza Chama katika njia moja nyembamba, na kutuburura kama vipofu tuitumbukize nchi yetu shimoni. Ni jitihada za kukifanya Chama, na sisi wengine wote, tuukubali msimamo wao wa kutaka kuigawa nchi yetu.


Lakini kwa bahati njema, pamoja na kubabaishwa na viongozi wetu, Halmashauri Kuu ya Taifa katika uamuzi wake wa kikao hicho ilirudia tena kusisitiza sera yake ya Muungano wa Serikali mbili. Sehemu inayohusika na Azimio la Halmashauri Kuu ya Taifa inasema:


“Chama kifuatilie mjadala wa wananchi juu ya Azimio hilo na kujipa nafasi ya kujenga mtazamo wake kuhusu Muundo wa Muungano kabla ya maamuzi ya mwisho. Wakati huu CCM italinda sera yake ya Serikali mbili.”


Ukizingatia jitihada na hila zilizotumiwa na viongozi wetu kuitaka Halmashauri Kuu ikubali hoja ya Serikali tatu, na pia ukizingatia msimamo wa Kamati Kuu yenyewe, niliona kuwa hata kule kubaki tu na sera ya Serikali mbili ni ushindi, ambao bado unaweza kutumiwa kuiokoa nchi yetu kutoka kwenye shimo la maangamizi.


Lakini nilitambua kuwa hali ni ngumu; maana waheshimiwa hawa walikuwa wametufikisha mahala ambapo Serikali ya Muungano ina sera moja, na Chama Cha Mapinduzi kina Sera nyingine. Na kwa hila na ujanja wa viongozi wetu wabunge wa Tanzania wamefanywa waonekane kama kwamba, katika suala hili, wote kabisa, wako upande wa Serikali. Hawa si watu wajinga wanajua watendalo.


BUNGE NA CHAMA:

Kabla ya kwenda Dodoma, na wakati tukiwa Dodoma, niliambiwa, kwa niaba ya waheshimiwa hao, kwamba Chama Cha Mapinduzi hakiwezi kupinga hoja ya Serikali tatu, maana hiyo sasa ni sera rasmi ya Bunge. Ati Chama hakiwezi kupinga Bunge lake, lakini kwa mantiki ya ajabu ajabu wabunge wanaweza kupinga Chama chao! Hiyo ndiyo demokrasia halisi ya mageuzi. Nilirudi Butiama nikalipa ada yangu ya CCM na nikaandika utenzi wa Tanzania Tanzania!

 

“Sasa wana hoja nyemi,

Ya kutaka kujihami,

Ni hoja ya kudanganya,

Na kutaka kujiponya.

Wanasema viongozi,

Ati Chama hakiwezi,

Kukataa sera hino,

Ya kuvunja Muungano.

Ati Serikali mbili,

Sasa ni sera batili;

Maana Bunge la watu,

Limetaka ziwe tatu.

Chama kisipobadili,

Hiyono sera batili,

Kitapinga Bunge lake

Pia Serikali yake.

Na hilo, wanatwambia,

Ni kinyume cha sharia,

Siyo halali kwa chama,

Kupinga Bunge la Umma!

Kale twali tukiimba,

Wimbo huu wa kasumba;

Furaha kuu, furaha kuu!

Mikono chini, miguu juu!

Twaenda machi, twaenda machi!

Twaenda machi, furaha kuu!

Hizo ni hoja za wakuu,

Za miguu kuwa juu,

Na vichwa vikawa chini,

Wabunge tahadharini.

Siyo zenu hoja hizi,

Ni hoja za viongozi,

Msizipe uhalali,

Kwani ni hoja batili

Wabunge wote wa umma,

Asili yao ni chama,

wale wa kuchaguliwa,

Na walioteuliwa

Sera zao Bungeni,

Zatokana na Ilani,

Ya uchaguzi wa nyuma,

Ulofanywa na kauma.

Na wala si sera zao.

Ni sera za chama chao,

Na sababu ya Ilani,

Ni kutafuta idhini,

Ya wananchi wenzenu,

Wakubali sera zenu.

Mkisha pata kibali,

Mtaunda Serikali.

Mtekeleze bungeni,

Sera zenu, kwa idhini;

Na wale walowatuma,

Ni chama pamwe na umma.

Ndiyo ma’na ikasemwa,

Wabunge wakishatumwa,

Wana kauli ya mwisho,

Wasikubali vitisho.

Wameshatumwa na chama,

Kwa idhini ya kauma,

Atowapinga ni nani,

Ila chama kipinzani?

Na kwa chama kipinzani,

Kiloshindwa uwanjani,

Kupitisha sera zake,

Kupinga ni haki yake.

Bali kwa ambalo katu,

Hamkutumwa na watu,

Wala si chama chenu,

Ila ni mawazo yenu.


Hamuwezi mkasema,

Kukataliwa na chama,

Si halali, ni haramu,

Na ni kupinga kaumu.

Wanaweza viongozi,

Baada ya uchaguzi,

Wakawa wanalo wazo,

Au wana pendekezo,

Wasotumwa na kauma,

Wala si sera ya chama.

Viongozi bila shaka,

Chama chao watataka,

Kijadili jambo hili,

Kipate kulikubali.

Likifanywa sera yao,

Kwa uchaguzi ujao,

Wataandika Ilani,

Waliombee idhini,

Endapo wapiga kura,

Wataikubali sera.

Ndipo tena Bunge lao,

La umma na Chama chao,

Litakwenda kutimiza,

Sera waliyoiagiza.

Serikali haiwezi,

Kwa hila za viongozi,

Ikapitisha Bungeni,

Sera iso na idhini.

Ya chama wala ya umma,

Kisha ianze kusema,

Chama kikichachamaa,

Sera kikaikataa,

Ati hiyo ni haramu,

Chama cha kupinga kaumu!

Ni nani alowatuma

Kwa uchaguzi wa nyuma?

Jambo hili ni lao tu,

Hawakutumwa na watu.

Kama wanalo haraka,

Kusubiri wamechoka,

Basi wasiwe ajizi,

Waitishe uchaguzi,

Ufanywe hata mwakani,

Waliombee idhini.

Wanasema linapendwa,

Hawawezi kushindwa,

Wanachohofu ni nini,

Kuliombea idhini?

 

Itaendelea wiki ijayo

 

By Jamhuri