Na Mwandishi Maalumu, JamhuriMedia

SERIKALI kupitia Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), imeendelea na juhudi za kuwafungulia fursa mabaharia wa Tanzania kimataifa.

Juzi, kwa niaba ya Serikali TASAC ilisaini Hati ya Makubaliano (MOU) na nchi ya Barbados ili nchi hizo mbili ziweze kutambua vyeti vya mabaharia wa kila upande. Tanzania kwa sasa imesajili vyeti 17,689 vya mabaharia.

Akizungumza mara baada ya kusainiwa kwa makubaliano hayo juzi jijini London, Uingereza, Mkurugenzi Mkuu wa TASAC ambaye pia ni Msajili wa Mabaharia na Meli nchini, Bw. Kaimu Abdi Mkeyenge amesema hadi sasa Tanzania imeanzisha mawasiliano na majadiliano na Nchi 34 kwa ajili ya kuingia katika makubaliano ya kutambulika kwa vyeti vya Mabaharia wa pande hizo.

Mkurugenzi Mkuu na Msajili wa Mabaharia na Meli wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Bw. Kaimu Abdi Mkeyenge (kushoto) akiwa na Msajili Mwandamizi Mkuu wa Mabaharia na Meli wa Barbados, Bw. Giovanni Ciniglio mara baada ya wawili hao kusaini Hati ya Makubaliano (MOU) kwa niaba ya nchi zao ili kuruhusu kutambuliwa vyeti vya mabaharia katika nchi hizo. Hafla hiyo ilifanyika juzi katkka ubalozi wa Barbados jijini London, Uingereza.

Amesema hatua hiyo ni fursa nzuri ya ajira za kimataifa kwa mabaharia wa Tanzania, lakini pia itasaidia kuondoa usumbufu wa kushushwa kwa mabaharia wa kitanzania katika meli mbalimbali ambazo zimesajiliwa na nchi ambazo Tanzania haina mkataba nazo.

Barbados ni nchi ya Kisiwani katika Bahari ya Karibi takriban kilomita 430 Kaskazini-Mashariki mwa Venezuela, mpaka sasa ina usajili wa wazi na masharti nafuu (open registry) wa meli 400.

Nchi jirani za karibu kuvukia bahari ni Saint Lucia na Saint Vincent upande wa Magharibi, Trinidad na Tobago upande wa Kusini na Grenada upande wa Kusini-Magharibi.

“Barbados ni moja ya nchi ambazo tulikuwa tumeanzisha mazungumzo kuhusu kutambuliana vyeti na tunashukuru leo hii tumefanikiwa kusaini Hati ya Makubaliano ya kutambuliana vyeti vya mabaharia, hivyo basi, ni dhahiri kuwa sisi tunatambua mabaharia wa Barbados na wao wanatambua mabaharia wetu”, amesema Mkeyenge.

Nchi nyingine ambazo Tanzania imeshaanzisha mawasiliano na majadiliano ni pamoja na Bahamas, Algeria, Korea ya Kusini, China, Comoros, Cyprus, Misri, Ufaransa, Ghana, India, Iran, Kenya, Liberia, Malta, Marshall Islands, Mongolia, Oman, Palau, Panama, Peru, Qatar, Saudi Arabia, Singapore, Africa Kusini, Shelisheli, Uturuki, Umoja wa Falme za Kiarabu, Vanuatu, Vietnam na nchi za Umoja wa Ulaya.

Mkurugenzi Mkuu na Msajili wa Mabaharia na Meli wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Bw. Kaimu Abdi Mkeyenge (kushoto) na Msajili Mwandamizi Mkuu wa Mabaharia na Meli wa Barbados, Bw. Giovanni Ciniglio wakitia saini Hati ya Makubaliano (MOU) ya kutambuliana vyeti vya mabaharia kati ya nchi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Barbados jijini London, Uingereza katika ofisi za Ubalozi wa Barbados.

By Jamhuri