Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Mwanza

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt.Angeline Mabula ametoa wito kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) kuweka mpango wa matumizi ya ardhi katika eneo la Mradi wa wa Chanzo na Kituo cha Tiba ya Maji cha Butimba mkoani Mwanza.

Dkt Mabula ametoa wito huo tarehe 14 Sept 2022 wakati wa uwekaji jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa chanzo na kituo cha tiba ya Maji Butimba jijini Mwanza uliofanywa na Makamu wa Rais Dkt Phillip Isdori Mpango.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (wa pili kushoto) akifurahia jambo na Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) Christopher Gachuma wakati wa uwekaji jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa chanzo na kituo cha tiba ya maji Butimba uliofanywa na Makamu wa Rais Dkt Phillip Mpango mkoani Mwanza

Ameishukuru MWAUWASA kwa kuweka uzio katika eneo linalozunguka mradi huo na kueleza kuwa, eneo hilo likiachwa wazi watu wataingia na ndipo migogoro ya ardhi inapoanza na kusisitiza kuwa mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza imefanya jambo zuri la kuweka uzio.

Hata hivyo, amesema pamoja na hatua ya kuwekwa uzio iliyofanywa na mamlaka hiyo lakini mpango wa matumizi bora ya ardhi kwenye eneo hilo ni muhimu ili kujua mahitaji ya huduma mbalimbali.

“Chanzo tunakiona kipo lakini wakiweka mpango wa matumizi mazuri kwenye eneo walilozungushia uzio tutajua tuna uhaba wa nyumba za watumishi zinazoweza kuwepo katika eneo hili na wakazi wake wakawa ni sehemu ya walinzi wa mradi. Uwepo wao utakuwa siyo tu utakuwa umeboresha maeneo lakini tutakuwa tumewapa makazi bora watumishi” amesema Dkt Mabula.

Akigeukia utunzaji mazingira, Waziri wa Ardhi Dkt Mabula alieleza kuwa, wizara yake imeelekeza kwamba, kwa sasa kila hati inapotoka basi iwe na masharti ya upandaji miti kwa lengo la kutunza mazingira.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza wakati wa uwekaji jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa chanzo na kituo cha tiba ya maji Butimba uliofanywa na Makamu wa Rais Dkt Phillip Mpango mkoani Mwanza

Mradi wa ujenzi wa chanzo na kituo cha tiba ya maji Butimba umewekwa jiwe la msingi na Makamu wa Rais Mhe. Dkt Phillip Mpango ambapo katika hotuba yake aliagiza mradi huo kukamilika mapema Desemba 2022 ili iwe zawadi ya Krismas kwa wakazi wa jiji la Mwanza na kusisitiza wananchi wanaoishi eneo linalozunguka mradi ni lazima wapewe kipaumbele katika kupatiwa huduma ya maji.

By Jamhuri