Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Katavi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Katavi imehukumu Titus Malambwa (28), mkazi wa Kijiji cha Ntibili Mpimbwe Wilaya ya Mlele, Mkoa wa Katavi kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mke wake kwa makusudi wakati wakiwa wamelala baada ya kukasirika kunyimwa na mkewe tendo la ndoa.

Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi Gway Sumaye, baada ya Mahakama kuridhika pasipo shaka yoyote ile kuwa mshitakiwa huyo alitenda kosa hilo ukiwepo ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na mama mzazi wa mshitakiwa pamoja na shangazi yake .

Mshitakiwa Titus amehukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kifungu cha sheria Namba 196 na 197 cha kanuni ya adhabu .

Awali katika kesi hiyo Mwendesha Mashitaka mwanasheria kutoka Ofisi ya Mashitaka Mkoa wa Katavi, Hongera Malifimbo, aliiambia Mahakama kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo mnamo Novemba 3,2019 katika Kijiji cha Ntibili Wilaya ya Mlele mkoani hapa .

Siku hiyo ya tukio mshitakiwa Titus alikuwa amelala na marehemu mkewe Noelia Costa na baada ya kushiriki naye tendo hilo hakuridhika na marehemu alimueleza kuwa alikuwa amechoka.

Mwendesha Mashitaka alieleza kuwa kauli hiyo marehemu ilimkasilisha mshitakiwa na ndipo aliposubiri marehemu mke wake apitiwe na usingizi kisha alitoka nje na kuchukua shoka na kumkata nalo kichwani ,tumboni na shingoni na kumsababishia majeraha makubwa yaliyomfanya atoke damu nyingi na kumsababisha kifo.

Baada ya mshtakiwa kutekeleza mauaji hayo alitoroka hadi alipokamatwa akiwa kwenye Kijiji cha Kakese kufuatia jitihada kubwa zilizofanywa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi .

Akisoma hukumu hiyo Hakimu Mkazi Mfawidhi mwenye Mamlaka ya kusikiliza kesi za Mahakama Kuu aliiambia mahakama kuwa pasipo shaka yoyote ile kutokana na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo mshitakiwa ametiwa hatiani pasipo shaka yoyote ile .

Hivyo alitoa nafasi kwa wanasheria wa upande wa mashitaka na utetezi kama wana maelezo yoyote ya kuieleza Mahakama kabla ya hukumu .

Mwanasheria wa Serikali Hongera Malifombo aliiomba Mahakama itoe adhabu kwa mujibu wa sheria inavyoelekeza licha ya kuwa mshitakiwa huyo hakuwa na historia yoyote ya kufanya kosa mengine .

Kwa upande wa mwanasheria wa mstakiwa Hamad Arfi alisema kuwa hana cha kuiomba Mahakama kwa kuwa kosa alilopatikana nalo mshitakiwa adhabu yake kwa mujibu wa sheria ni moja tu.

Hakimu Mkazi Mfawidhi alisoma hukumu na kuiambia mahakama kuwa mshitakiwa amepatikana na hatia kinyume na kifungu cha sheria namba 196 na 197 cha kanuni ya adhabu hivyo mshtakiwa mahakama imemuhukumu kunyongwa hadi kufa Titus Malabwa na kama atahitaji kukata rufaa nafasi hiyo ipo wazi.

By Jamhuri