Na Munir Shemweta, WANMM

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula ameitaka Kamati ya Uteuzi na Nidhamu ya Madalali na Wasambaza Nyaraka wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya kuhakikisha madalali wanaoteuliwa wanapata mafunzo na wenye weledi wanaoweza kufanya kazi kwa staha.

Dkt.Mabula amesema hayo Mei 16,2023 alipokutana na Kamati ya Uteuzi na Nidhamu ya Madalali na Wasambaza Nyaraka wa Mabaraza ya Ardhi, Nyumba na Wilaya ilipokwenda kumtembelea ofisini kwake Mtumba jijini Dodoma.

Kamati hiyo ambayo iko chini ya Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi iliundwa Desemba 27, 2021 kwa mujibu wa wa kifungu cha 2&3 cha sheria ya Mahakama za migogoro ya ardhi sura 216.

“Ni vizuri madalali mtakaowateua waonekane ni wale waliopata mafunzo na wenye weledi na wanaoweza kufanya kazi kwa staha, hilo nalo ni zuri zaidi” amesema Dkt.Mabula.

“Unaenda kutekeleza amri ya mahakama halafu unachukua vitu unarusha huko hiyo hapana, tunatambua ni amri ya mahakama lakini basi ifanyike kwa staha siyo kujivurugia kwa sababu ni dalali, tusingependa kuingia kwenye historia ya kuanza na madalali walioteuliwa kwa kanuni mpya na kupigiwa kelele” àmesema Dkt Mabula.

Aidha, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ametaka madalali walio na leseni za utekelezaji kutoenda moja kwa moja kwenye tukio bila kupita ofisi za utawala wa eneo husika na kutaka madalali   wakati wa utekelezaji kupita kwa Mkuu wa Mkoa. Wilaya wilaya au Afisa Tarafa kutegemeana na utaratibu utakaowekwa ili kazi ifanyike na baraka za utawala.

” Kumekuwa na changamoto hiyo mara  nyingi sana, dalali anapata kazi anaamkia site anaenda kuvunja nyumba mimi nisingependa yatokee kwa style hiyo ni vizuri kupita kwa DC akaona hukumu yenyewe au amri ya mahakama na kujiridhisha ingawa hana namna ya kubadilisha lakini akawa na taarifa nini kinaenda kufanyika” amesema Dkt Mabula.

Akigeukia suala la wito wa mahakama, Waziri Mabula ametaka kujua sheria inasemaje kwa mtu anayepelekewa wito na kukosekana mara moja au mbili nyumbani kwake.

“Nisingependa malalamiko yatokane na madali walioteuliwa halafu mtu akose haki kutokana na kutopata wito au nyaraka iliyotoka mahakamani na taratibu nyingine zikaendelea ni vizuri kuangalia utaratibu mzuri wa kuhakikisha  mhusika amefikiwa na kama hakufikiwa utaratibu upi unatumika ili walau afahamishwe kile kinachoendelea vinginevyo tunatumia madalali badala ya kupunguza changamoto zinakuwa zinaendelea” amesema Mabula.

Majukumu makuu ya Kamati ya Uteuzi na Nidhamu ya Madalali na Wasambaza Nyaraka wa Mabaraza ya ardhi ni kufanya uteuzi wa Madalali na Wasambaza Nyaraka wa Mabaraza ya ardhi, Kusikiliza na kuamua madai ya utovu wa nidhamu dhidi ya madalali na wasambaza nyaraka wa mabaraza ya ardhi  pamoja na kuunda na kusimamia  kamati ndogo za kusimamia Madalali na Wasambaza Nyaraka katika ngazi za mikoa.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Uteuzi na Nidhamu ya Madalali na Wasambaza Nyaraka wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya ilipomtembelea ofisini kwake Mtumba jijini Dodoma tarehe 16 Mei 2023. Kulia ni Katibu Mkuu Eng. Anthony Sanga.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Kamati ya Uteuzi na Nidhamu ya Madalali na Wasambaza Nyaraka wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya wilaya. Wa pili kulia ni Katibu Mkuu Eng. Anthony Sanga. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)

By Jamhuri