Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis amesema kuwa hadi sasa hakuna changamoto mpya za Muungano zilizojitokeza. 

Amesema hayo leo Mei 17, 2023 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Angelina Adam Malembeka aliyetaka kufahamu changamoto gani mpya za Muungano zimejitokeza.

Khamis amesema kuwa Muungano umeendelea kuimarika ambapo wananchi wa pande zote mbili wameendelea kunufaika kutokana na mafanikio makubwa yaliyopatikana kiuchumi, kijamii na kisiasa. 

Akiendelea kujibu swali hilo amesema mafanikio ya kutokuwa na changamoto mpya ni kutokana na jitihada za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SJMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kuweka Muongozo mzuri wa kushughulikia changamoto kwa haraka zinapojitokeza katika hatua za awali.

”Lengo la Serikali zote mbili ni kuhakikisha changamoto za Muungano zinazojitokeza zinapatiwa ufumbuzi na kuendelea kuimarisha Muungano ili kuepusha changamoto mpya kujitokeza,” amesisitiza Naibu Waziri Khamis.

Ameongeza kuwa Serikali zote mbili kuanzia wataalamu, makatibu wakuu, mawaziri na Kamati ya Pamoja ya viongozi wakuu inakutana kufanya majadiliano ili kuhakikisha changamoto zote zilizosalia zinaisha.

Aidha, amesema kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais hutumia vyombo vya habari na tovuti yake pamoja na makongamano kwa lengo la kuelimisha wananchi kuhusu faida za Muungano.

Wakati huo akijibu swali la Mbunge wa Mwera Zahor Mohamed Haji aliyeuliza kwanini Halmashauri ya Magharibi ‘A’ imeweka Sheria ya Kodi na VAT kwenye Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo, Mhe. Khamis amesema Serikali ya SMT itashirikiana na serikali ya SMZ kufuatilia utaratibu unaotumika.

Amesema Fedha za Mfuko wa Jimbo hutolewa mujibu wa Sheria ya Mfuko wa Jimbo, Sura 96 ya mwaka 2009 na zinatumika kwa kuzingatia Miongozo, Kanuni na Taratibu za usimamizi wa fedha za umma.

Hata hivyo, Naibu Waziri huyo amebainisha kuwa kila upande wa Serikali zote mbili una utaratibu wa usimamizi wa matumizi ya fedha za uma huku akisisitiza kuwa dhamira ya Serikali ni kuendelea kutoa fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo kwa pande zote mbili kwa ajili ya kuboresha huduma za jamii na kuwaletea wananchi maendeleo

By Jamhuri