Na Mwandishi Maalumu – Dar es Salaam

Madaktari 22 wanaotoa huduma kwa watoto kutoka Tanzania na nje ya nchi wanashiriki mafunzo maalumu ya awali ya namna ya kufanya kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiograph – ECHO) kwa watoto.

Mafunzo hayo ya siku tano yanafanyika kwa mara ya sita tangu yalipoanzishwa mwaka 2018 yakiratibiwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Shirika la Madaktari bingwa wa magonjwa ya watoto kutoka Ujerumani (GTP) na chama cha madaktari wa watoto Tanzania (PAT).

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Stela Mongela  alisema mafunzo hayo yamewalenga madaktari wanaotoa huduma kwa watoto ili waweze kubaini magonjwa ya moyo kwa watoto mapema na watoto waweze kupatiwa matibabu wanayostahili kwa wakati.

“Kati ya madaktari 22 wa watoto wanaoshiriki katika mafunzo ya mwaka huu watano wametoka nchini Uholanzi na Ujerumani na wengine 17 wametoka katika mikoa ya Mtwara, Morogoro, Dodoma na Dar es Salaam”, alisema Dkt. Stella.

Dkt. Stella alisema wanatarajia baada ya mafunzo hayo kumalizika wataalamu wa afya walioshiriki watakuwa wamepata maarifa yakuweza kufanya kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiograph – ECHO) kwa watoto na kuchukuwa maamuzi stahiki pale watakapokutana na watoto wenye shida za moyo.

Naye mshiriki wa mafunzo hayo Daktari bingwa wa magonjwa ya watoto kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili Nsajigwa Misidai alisema mafunzo hayo yatawasaidia kuwa wafanisi zaidi katika kugundua magonjwa ya moyo kwa watoto mapema.

Dkt. Nsajigwa ambaye ni daktari katika wodi ya watoto wachanga (Neonatal) alisema kwasababu yeye anafanya kazi katika wodi ya watoto wenye umri wa kuanzia siku moja hadi siku 28 ataweza kuwafuatilia kwa karibu na pale atakapoona dalili za magonjwa ya moyo kwa mtoto atachukua hatua za haraka kuhakikisha mtoto anapata matibabu kwa wakati.

“Nimefurahi sana kushiriki katika mafunzo haya ambayo yanaenda kunirahisishia majukumu yangu ya kazi kwani nitakuwa na uwezo wa kuwagundua watoto wenye shida za moyo mapema na kuwapa matibabu stahiki mapema”, amesema Dkt. Nsajingwa

Tangu mafunzo hayo yalipoanza kutolewa mwaka 2018 madaktari wanaotoa huduma kwa watoto 100 kutoka Tanzania na nchi za nje wameweza kushiriki mafunzo hayo.

Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Stella Mongela akiwaonyesha namna ya kufanya kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiograph – ECHO) wataalamu wa afya kutoka nchini Ujerumani, Uholanzi na Tanzania wakati wa mafunzo maalumu ya siku 5 ya awali ya jinsi ya kufanya ultrasound ya moyo yanayofanyika katika Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya wataalamu wa afya kutoka nchini Ujerumani, Uholanzi na Tanzania wakimpima mtoto kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiograph – ECHO) wakati wa mafunzo maalumu ya siku 5 ya awali ya jinsi ya kufanya ultrasound ya moyo yanayofanyika katika Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.