Kampuni ya Usafirishaji wa mizigo ndani na nje ya nchi ya Usangu Logistics ya jijini Dar es Salaam imelalamikiwa kwa kuwanyanyasa wafanyakazi na kujihusisha na ukwepaji wa kodi kwa kutumia namba bandia za magari.

Wafanyakazi wa kampuni hiyo, wanaodai kunyanyaswa mwajiri kwa kukatwa mishahara bila sababu za msingi, kufukuzwa kazi kinyume na sheria za kazi, na wakati mwingine kuchapwa viboko iwapo gari limepata tatizo lolote barabarani.

Katika hali ya kuhitaji faraja ya kufanya kazi, wafanyakazi hao wameiangukia Serikali hususani Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kuifuatilia kampuni hiyo na wamiliki wake kupata ukweli wa madai hayo.

Wakizungumza na JAMHURI kwa sharti la kutotajwa majina gazetini, wanasema Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo, Ibrahim Ismail amekuwa akiwakata mishahara kiasi cha Sh 25,000 kwa kila mfanyakazi (Red payment voucher) ambayo haijulikani yanakopelekwa makato hayo. Wanaamini wanadhulumiwa.

“Kwa upande wa mafundi, akitoa maelekezo ya kutengeneza gari na tukichelewa kukamilisha kwa muda anaoutaka yeye, anatukata mshahara kila mmoja Sh 200,000 na kwa watu watano anachukua milioni moja au zaidi.

“Mishahara yetu ni midogo, wengine tunalipwa Sh 150,000 hadi 250,000 kwa mwezi ambazo anatudhulumu kwa madai ya kutuadhibu kwa kutokamilisha matengenezo ya magari kwa muda aliotupangia na pia kuchapwa viboko kama wanyama, tunateswa mno Watanzania na watu hawa,” ameeleza mmoja wa wafanyakazi.

Wanasema wamekuwa wakipeleka malalamiko kwa muda mrefu kituo cha Polisi cha Buguruni na kwa Maofisa wa Wizara ya Kazi ambao baadhi wamekuwa wakipewa fedha na kutochukua hatua zozote zile na kuwaacha wanaotoa taarifa za manyanyaso hayo wakifukuzwa kazi bila utaratibu.

“Kampuni hii inasafirisha mafuta ya Petrol na bidhaa mbalimbali nchi za Afrika ya Mashariki na Kusini, lakini kinachotushangaza wakati tunapopakia mizigo zinabandikwa namba zingine za magari ambazo inaonesha ni za bandia na ubadilishaji huo wa namba hufanyika wakati wote wa safari ikiwa ni ukwepaji wa kodi za serikali,” anasema.

 

Mmoja aeleza alivyofukuzwa bila utaratibu

Saitoti Oyaya aliyefukuzwa kazi bila utaratibu na mwajiri wake Usangu Logistics,  Machi 14, 2014 alifungua shauri Tume ya Usuluhishi na Uamuzi Kanda ya Dar es Salaam lililopewa Na. CMA/DSM/ILA/239/14/1281 na kushinda.

Saitoti anasema awali shauri hilo, halikupata suluhu katika hatua ya usuluhishi hivyo akaamua kulipeleka katika hatua ya uamuzi Agosti 13, 2014 akiwakilishwa na mwakilishi binafsi Zakaria Jorojig na upande wa mlalamikiwa uliwakilishwa na Tulianus Mtafungwa ambaye ni Meneja Usalama wa kampuni hiyo.

Katika shauri hilo hoja zilizokuwa zikibishaniwa ni endapo kulikuwa na sababu halali za mlalamikaji kuachishwa kazi; endapo mlalamikiwa alifuata taratibu halali wakati wa kumwachisha kazi mlalamikaji na nafuu zipi kila upande unastahili.

Mwakilishi wa mlalamikaji akitoa ushahidi mbele ya tume hiyo, anasema mlalamikaji (Saitoti Oyaya) alikuwa mfanyakazi wa mlalamikiwa kama mlinzi Aprili, 2012 kwa ujira wa Sh 155,000 kwa mwezi.

Julai, 2012 alibadilishwa kitengo na kuwa mkaguzi wa mgari hata hivyo hakukuwa na badiliko la ujira akiwa chini ya Mkuu wake wa Idara ambaye ni ofisa usafirishaji. Agosti alibadilishwa kazi na Mkurugenzi wa Kampuni hiyo kwenda kwenye kitengo cha ununuzi wa vipuri vya magari ambako mlalamikaji aliwajibika kwa ofisa ununuzi wa spea, Taji Mohamed Abasi.

Katika kitengo hicho alifanya kazi mbili, ununuzi wa spea na huduma ya chakula kwa viongozi wake wa kazi na ujira wake kwa mwezi ulikuwa Sh 270,000 kwa mwezi.

Anasema kwa muda wake wote amefanya kazi kwa uaminifu wake wote na kuzingatia taratibu zote. Hata hivyo siku moja alipewa maelekezo na mwajiri wake kwamba atafute spea ambayo ni skrubu (screw) yenye urefu wa inchi nne na asipoipata asifike kazini na kazi hiyo aliifanya kwa siku mbili bila mafanikio.

Jumanne Februari 18, 2014 anasema aliitwa na Ofisa Rasilimali Watu, Grace Charles alimweleza kwamba hatakiwi kufanya kazi ya aina yoyote kutokana na maelekezo aliyopewa kwa njia simu na mkurugenzi.

Aliporudi kutoka katika majukumu yake nje ya ofisi, siku hiyohiyo ambayo ilikuwa ni ya tatu ya utafutaji wa kipuri hicho bila mafanikio, alizuiwa na mlinzi kuingia ndani ya ofisi yakiwa ni maelekezo kutoka kwa mwajiri wake.

“Sikupewa barua yoyote zaidi ya kukabidhiwa kwa mlinzi wa getini na kuelezwa kuwa sitakiwi tena kuingia eneo la kazi la mwajiri na kwamba nimefukuzwa kazi.

“Pamoja na kuachishwa kazi bila utaratibu, nililipwa Sh 930,000 mbele ya tume ikiwa ni makato ya mshahara Sh 500,000, likizo 270,000 na mshahara nusu kwa mwezi wa pili wa siku 18,” anasema.

Mlalamikaji anapinga kuachishwa kazi na mlalamikiwa kinyume na Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, sheria   namba 6 ya mwaka 2004 ambayo inaeleza bayana juu ya sababu na taratibu halali wakati wa kusitisha ajira kifungu cha 37 (1), (2) a na b (i),(ii),(c).

Saitoti ameshinda shauri hilo na mlalamikiwa kuamuriwa kumlipa fidia ya mshahara wa miezi 12, hati ya utumishi na kiinua mgongo na vyote vikifikia jumla ya Sh 3,385,385 na uamuzi huo umetolewa kwa mujibu wa kifungu cha 88 (8) cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini namba 6 ya 2004.

“Uamuzi huu utekelezwe ndani ya siku 14 tangu utolewe, aidha nafasi ya marejeo ipo wazi kwa upande wowote usioridhika na uamuzi huu,” imeeleza nakala hiyo ya uamuzi iliyotolewa na Tume Desemba 30, 2015 na kusainiwa  na Mwamuzi wa shauri hilo, Fungo E.J.

Hata hivyo mlalamikiwa hajatekeleza maelekezo aliyopewa na tume hiyo hadi sasa na badala yake amekata rufaa Mahakama Kuu.

 

Usangu wafunguka 

JAMHURI lilimtafuta Mkurugenzi Mtendaji wa Usangu Logistics, Ibrahim Ismail bila mafanikio na baada ya jitihada hizo kushindikana, lilifanya mahojiano na Mkurugenzi wa Fedha, Saad Ismail ambaye pia ni miongoni mwa wamiliki wa kampuni hiyo kuhusu unyanyasaji wafanyakazi na ukwepaji wa kodi za serikali kwa kutumia namba bandia katika magari.

Saad anasema hashangazwi na suala la malalamiko ya wafanyakazi kwani mara kadhaa wanaweza kusema lolote lile wanaloona linafaa. Anasema Maofisa wa Wizara ya Kazi wamefanya ukaguzi katika kampuni hiyo kwa kipindi cha miezi miwili iliyopita na kugundua kwamba wako sahihi.

Hata hivyo, Saad hakutaka kuzungumza zaidi kwa madai kwamba yeye sio msemaji wa kampuni hivyo, atafutwe Mkurugenzi, Ibrahim.

Naye, Meneja Mahusiano wa Kampuni hiyo, Grace Charles alipohojiwa na JAMHURI, alikanusha wafanyakazi hao kuajiriwa bila kuwa na mikataba na kwamba hawabadilishi namba za magari ambayo wafanyakazi wanadai wanafanya hivyo kwa muda mrefu kwa kukwepa kulipa kodi za serikali.

Meneja huyo anasema wana jumla ya wafanyakazi 202 kati yao madereva ni 180 na kwamba wote wana mikataba ya kazi na kumwomba mwandishi wa JAMHURI kufika ofisini kwake kuiona mikataba hiyo.

Lakini alipofuatwa ofisini kwake hakuweza kupatikana kwa madai kwamba alikuwa kwenye kikao na wamiliki wa kampuni hiyo na alipopigiwa simu na kutumiwa ujumbe mfupi wa maneno hakuweza kupokea wala kujibu hadi mwandishi anaondoka katika ofisi za kampuni hiyo saa saba mchana Ijumaa iliyopita.

Hata hivyo JAMHURI, imeelezwa na vyanzo vyake vya habari kwamba wafanyakazi walioituhumu kampuni hiyo kuwanyanyasa wanasakwa na uongozi kwa lengo la kuchukuliwa hatua.

By Jamhuri