Kwa Magufuli haponi mtu

maguJuzi Jumapili, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli alifanya mabadiliko ya ghafla kwa kumteua Balozi Mhandisi John William Kijazi kuwa Katibu Mkuu Kiongozi.

Taarifa hizo zilithibitishwa na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, Ikulu, Gerson Msigwa.

Kabla ya uteuzi huo Mhandisi Kijazi alikuwa Balozi wa Tanzania nchini India na anachukua nafasi ya Balozi Ombeni Sefue ameelezwa kuwa atapangiwa kazi nyingine.

Hata hivyo, kabla ya Rais Dk. Magufuli kutangaza hatua hiyo, katikati ya wiki iliyopita alisema kuna baadhi ya watu wamejipanga kufifisha nguvu zake za kuchukua hatua dhidi ya viongozi mbalimbali wa serikali na mashirika ya umma waliofanya makosa hasa ya ubadhirifu.

Japo Rais Dk. Magufuli hakuwataja, lakini akaonya watu wanajitokeza kutetea watuhumiwa mbalimbali wa ufisadi hasa wale waliochukuliwa hatua za awali, ikiwamo ya kusimamishwa kazi kwamba wamwache afanye kazi.

Rais Dk. Magufuli ameomba Watanzania kuendelea kumuunga mkono ili aendelee kupambana watuhumiwa hao wa ufisadi kwa kuwa ni wachache na kwa kipindi kirefu waliharibu maisha ya Watanzania wanaokadiriwa kufikia milioni 50.

Rais Dk. Magufuli anasema ataendelea kupambana na watuhumiwa hao na wengine na uchunguzi ukikamilika wale watakaostahili kupelekwa mahakamani, watapelekwa.

Lakini onyo ambalo mwenyewe alisema: “Nimelichomekea” limo kwenye sehemu ya hotuba ya neno kwa neno aliyoitoa wiki iliyopita kwa baadhi ya wakazi wa Arusha, katika hafla ya uwekaji jiwe la msingi katika sehemu ya barabara ya Sakina hadi Tengeru yenye urefu wa kilomita 14.1, itakayokuwa na njia nne.

Alisema: “Ndiyo maana nawaomba ndugu zangu wa Afrika Mashariki. Ninyi wananchi mkiamua sisi viongozi tutaweza. Mkitupa sapoti tutaweza. Mkituombea yale tunayotakiwa kuyafanya, tutaweza, msipotusaidia hatutaweza.

“Na ndio maana hapa Watanzania wenzangu, tumekuwa na hatua ndogondogo ambazo tumeanza kuzichukua. Za kuwashughulikia watu ambao walianza kuneemeka kwa wakati wao, wakawatesa Watanzania wengi.

“Na wala hawajafika kuwa wengi…kwa sababu idadi yangu mimi hata wakifika 2,000, sawa tu. Ili kusudi Watanzania milioni 50 wafaidike. Lakini tumenza kusikia wale ambao walikuwa wanafaidi nao hao, wameanza kulalamikalalamika. Wakashindwe wakalegee. Watuache tufanye kazi kwa ajili ya Watanzania waliokuwa wanyonge.

“Tanzania hii, ilikuwa shamba la bibi, watu walikuwa wanafanya ya ovyo. Ninaposema ya ovyo ni ya ovyo kweli, mimi nipo serikalini, lakini nimekuwa waziri kwa miaka 20, ninayajua. Ninaposema ya ovyo, ndugu zangu naomba mniamini.

“Mambo ya mateso kwa wananchi hayana chama. Ukikosa madawa hospitalini hata ukiwa Chadema utakosa tu, hata ukiwa CCM unaimba kila siku CCM oyeee, utakosa tu madawa. Kwa hiyo hatua tunazotaka kuzichukua ni kwa wananchi wote bila kujali itikadi zao.

“Tumefika katika wakati huu, ni lazima patokee mmoja wa kuyafanya. Na ndiyo maana siku zote nimekuwa nikiwaeleza. Ndugu zangu mimi nimeamua kuwa sadaka ya Watanzania. Kazi hii ni ngumu, ni ya ajabu. Kila mmoja anajitahidi haya tunayoyafanya tusiyafanye, lakini nawashukurui mnaendelea kuniombea. Ndiyo maana niko hapa. Endeleeni kutuombea  lengo letu ni la kuwasaidia ninyi. Ni lazima tufanye.

“Tusipofanya hakuna sababu ya mimi kuwa rais. Hakuna sababu ya mimi kuwa Rais. Hakuna sababu ya mimi kuitwa rais. Ni vema niende nyumbani nikakae, nilale. Hakuna sababu ya mimi kuitwa Rais. Nasema kwa dhati kutoka moyoni. Hakuna sababu ya mimi kuitwa rais.

“Kwa hiyo ninawaomba ndugu zangu Watanzania. Mtusapoti. Tufanye haya tunayoyafanya. Mambo ya ovyo!, juzi tumeshindwa sisi kuingia kwenye mambo ya roaming ndani ya East Africa Community kwa sababu sisi, hatutasafisha nyumba yetu. Kwenye TCRA kule, kulikuwa na mambo ya ovyo yanafanyika. Juzi Profesa Mbarawa yuko hapa, waziri wa miundombinu amefukuza baadhi ya wafanyakazi pale. Tumepoteza zaidi ya Sh bilioni 400.

“Bilioni 400 zilikuwa zinatosha kununua sijui ndege ngapi… tatu hivi za airbus. Tungeweza kutengeneza barabara lolote hata tukapasua hapa la kilometa zote. Lakini watu wamechezea pale na wako pale wengine wanajiita wasomi.

“Ndiyo maana tunaamua sisi kufukuza. Na tunafukuza baadaye watapelekwa mahakamani. Ili ikiwezekana wakafungwe wakapate machungu ya wananchi ambayo wameyatengeneza kwa miaka mingi.

“Na kwenye hili ndugu zangu mimi sitaangalia sura. Uwe Chadema, uwe CCM, uwe CUF, uwe huna chama…Ni Kazi Tu…utapelekwa. Ni tufike mahali tuache kuvumiliana, tuache kuonenaa aibu. Haiwezekani nchi zetu zikaendelea kuwa masikini.”

Rais Dk. Magufuli alihutubia hayo mbele ya viongozi wa nchi zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), wakiwamo Rais Yoweri Museveni wa Uganda, Uhuru Kenyatta wa Kenya, Makamu wa Pili wa Rais wa Burundi, Dk. Joseph Butore, Makamu wa Pili wa Rais wa Sudan Kusini na James Wani Igga.