January, Mwamvita wamjia juu Mzungu

January Makamba1Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, (Mazingira na Muungano), January Makamba, ameibuka na kuzungumzia kwa undani kutohusika kwake na kashfa ya ‘udalali’ wa kutafuta wawekezaji wanaotafuta zabuni serikalini ikiwamo ya ujenzi wa Bandari mpya ya Bagamoyo.

January amesema juzi jijini Dar es Salaam kwamba suala la raia wa nje, anayedai kuwa ametapeliwa zaidi dola 25,000 halina ukweli wowote, hoja inayoungwa mkono na Dada yake, Mwamvita Makamba.

Akizungumza kwenye mahojiano maalumu juzi, January ambaye aliingia kwenye rekodi ya kuingia Tano Bora ya makada watano wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwania urais mwaka jana, anasema: “Kwanza, hii habari nadhani inamhusu dada yangu.”

January ambaye hakufanikiwa kusonga mbele na makada wengine watatu waliompisha Rais Dk. John Magufuli amrithi Jakaya Kikwete, anasema: “Habari hii inamhusu sana dada yangu, kwa hiyo, nadhani yeye atakuwa ni mtu mwafaka wa kuongea naye, na kama hamna simu yake, nitawapa.”

Mwanasiasa huyo, miongoni mwa viongozi wanaotazamwa kimaadili kwa ‘jicho la tatu’,  anafafanua zaidi akisema: “Lakini ngoja nieleze tu, ninavyolijua jambo lenyewe. Kwa sababu naona linawekwa zaidi kisiasa na kiuchochezi. Eeh huyu bwana mimi nimemfahamu… huyu anayezungumzwa huyo, raia wa kigeni, nimemfahamu mwaka 2010, nadhani mwaka 2010 kabla ya sijaingia bungeni.

“Na nimemfahamu kwa sababu alikuwa na uhusiano na sister yangu. Na wakati huo, sister yangu alikuwa ananiambia bwana kuna bwana mmoja, anapenda sana kuonana na wewe, kila siku ananisumbua anataka nikukutanishe naye. Halafu sasa mimi nikawa nasita, nasema mtu huyu ndiyo una uhusiano naye, kwanini ang’ang’anie kuonana na mimi? nini?.

“Kila siku ya Mungu nikikutana na sister yangu, mara ananipigia simu…basi njoo bwana anaomba sana. Basi, sasa mimi nikawa nasita. Lakini baadaye nadhani ilikuwa mwaka mpya 2010 kuingia 2011 nilikuwa nasafiri napita Dubai ndio nikaonana naye. Alikuwa pale na sister yangu alikuwa hapo.

“Ndio nikakutana naye kwa mara ya kwanza, basi tukasalimiana, tukajuana na kubadilishana namba. Sasa nini tatizo?, nilikuwa sijui alikuwa ana shida gani, na kidogo wenyewe wakaendelea na mahusiano yao na dada yangu.

“Baadaye nikawa simsikii tena sister anamzungumzia au anamtaja, wala siwaoni pamoja, nikauliza nini kimetokea? Akaniambia yule bwana tumegombana… Tumegombana kwa mambo mawili, kwanza nimegundua… sasa sister ananiambia, nimegundua kwamba kumbe alikuwa uhusiano wetu alitaka mimi nimsaidie kumuunganisha na viongozi.

“Kwa hiyo, kila siku alitaka nimuunganishe na huyu nimkutanishe na yule. Kwa hiyo sister yangu akasema uhusiano huu ni kama tu, wa kutumiwa. Kwa hiyo akamua kuachana naye.

“Lakini pili, eeeh ikiwamo kwa kukutana na maanake alimwomba, ananiambia sister yangu…huyu bwana alimuomba amkutanishe na Chambo, wakati huo Chambo ni Katibu Mkuu wa mambo ya uchukuzi. Sasa nadhani alimpa namba tu, akaenda huko, akakutana naye nadhani hawakufanikiwa mambo yao. Ilikuwa ni 2011.

“Haya mambo yote yanayozungumzwa yalikuwa ni 2011. Huyu bwana sijamtia machoni kwa miaka mitano sasa hivi. Kwa hiyo eeh eeh… Kwa hiyo eeh baadaye akaniambia tena kwamba wamegombana kuhusu biashara. Kwamba wakati huo wakaamua kufanya biashara nadhani ya kuagiza mashine ya kutengeneza kahawa kwenye maofisi.

“Wakakubaliana kila mtu aweke dola 50,000, lakini dada yangu yeye akawa na shaka na biashara ile, kwa hiyo akaamua aweke 25 kwanza, halafu baadaye akapata uhamisho wa kwenda South Africa kikazi.

“Na huyu bwana akawa anaendesha hii biashara. Baadaye biashara ikafa. Eeh biashara ilivyokufa, sasa huyu bwana akawa bado anadai ile nusu ya mtaji ambao alipaswa kuutoa dada yangu. Kwamba bwana biashara imekufa, lakini eeeh nipe hela yangu.

“Sasa hapo ndipo kwenye ubishi na madaiano ya pesa na baadaye sasa wakawa wanatumiana meseji huko za kuchafuana kwenye… sijui nini baadaye waka… nadhani mwaka huu mape… nadhani mwaka jana mwishoni. Huyu bwana akawa anaomba kukutana na mimi baadaye. Mimi sina cha kuongea naye kuhusu hela yake anayodai. Nikamuuliza sister hili jambo utali-handle vipi. Akaniambia mimi bwana naona usumbufu naona ni afadhali nimpe kiwanja changu auze niondokane na kadhaa ya meseji kila siku.

“Na wakati huohuo kumbe huyu bwana akimpigia simu anamrekodi. Anatengenezea mazungumzo ya namna ya kumrekodi. Mtu akiamua kukurekodi. Unajua kama mtu amemua kukurekodi na siku anakutafuta, anatengeneza mazingira ya namna ya kukirekodi. Kwa hiyo wakawa wanarekodiana.

“Baadaye kama wiki mbili, tatu zilizopita yule bwana anasema mimi nataka kutoa vitu mtandaoni na mambo. Nipe hela yangu. Anamwamba sister kwamba nitawalipua, mimi nikamwambia mwache aweke mtandaoni kwani kuna kosa gani limefanyika. Kama mtu ametengeneza rekodi, amezi-edit ili ionekana kama makosa basi watu watajua tu, lakini huwezi kukubali kuwa blackmailed yaani mtu anakutengenezea shinikizo la kipuuzi, basi nadhani kwamba mwishowe ndio, inakuja kutokea hiyo.

“Na huyu bwana, ikabidi niulize sasa yuko wapi na anafanya shughuli gani, nilichosikia ni kwamba ile biashara ilikufa kwa sababu alijingiza kwenye matumizi ya madawa. Akafukuzwa kwenye nyumba anayokaa. Sasa hivi anakaa hapo Hyatt Hotel na chumba chenyewe wamemzuia kutoka kwa sababu ya madeni.

“Kwa hiyo yote hii ni desperation ya kutaka apewe hela ambayo hastahili. Alipe madeni yake, Eeeh kwa hiyo. Sasa kama anadhani kuchafua watu na kutengeneza uongo kutasaidia. Hakuwezi kusaidia, mimi sihusiki na haya mambo sijui. Mambo ya mahusiano, mapenzi na kuna kipindi huko nyuma wakati natengeneza website yangu ya Bumbuli.

“Nilimwambia dada yangu anichangie, akanichangia kidogo, sasa inaelekea kumbe walipeana hela huko kwa hiyo na mimi nadumbukizwa humo ndani. Kwa hiyo halina ukweli wowote na kama kuna usahihi. Haki inatafutwa mahakamani, haitafutwi mtandaoni. Ukiona mtu anapeleka mambo ya kudai haki yake mtandaoni, basi ujue kuna siasa na kuna kuchafuana. Nadhani hicho ni kikubwa,” anasema Makamba.

Kwa upande wake, Mwamvita akizungumzia jambo hilo, anasema: “Ni suala la 2010 na 2011. Huyu bwana ni dalali yeye. Ni mtu ambaye nilikuwa na uhusiano naye kimapenzi, kwa muda mfupi sana.”

“Sikujua kwamba alikuwa dalali, tapeli alikuwa anataka kunitumia mimi kujuana na watu. Kujua hapa na pale, halafu ndiyo maana sikumtambulisha. Haya mambo ni ya kwake mwenyewe, unajua mtu ambaye anatapatapa, anatafuta kick. Hii yote ni maneno na mtu ambaye ni mkosaji. Hakuna kitu chochote.

“2010…halafu baadaye unaanza kumrekodi mtu halafu unazungumza yeye kum-lead kuona kwamba amekosea,mambo gani hayo? Hamna lo lote katika hili suala January, hahusiki kabisa kabisa. Huku ni kutafuta tu kick na kumhusisha mtu ambaye hayupo.

“If anything, mimi ndiye niliyekuwa namfahamu huyo bwana, nilikuwa namtambua. Lakini yeye ilikuwa kila kitu tunachofanya, kwa sababu kutafuta kick kujuana na watu. Nilim-introduce kwa watu wawili, watatu ambao wote aligombana nao na amewatapeli. Hamna lolote, hamna lolote kabisa kwenye hili suala na hata waseme nini. Watengeneze sijui makaratasi. Ni tapeli na anajulikana. Ukimchunguza. Watu wanamjua mjini miaka mingi sana, baba yake alikuwapo miaka ya 80 unajua biashara gani walikuwa wanafanya miaka yote Tanzania.

“Hali ngumi kidogo ndio maana anatafuta mtu wa kumlalamikia. Lakini, hamna lolote katika hili suala na ninashangaa wanaobeba hili suala na kuliweka kwenye mtandao hawajui undani wake. Is real ninayosema.”