JamiiForums yawashitaki wasiotaka ufisadi uanikwe

Kampuni ya Jamii Media, inayoendesha mitandao ya JamiiForums.com na FikraPevu.com; hatimaye imeamua kutafuta haki mahakamani dhidi ya kile kinachoonekana kuwa ni matumizi mabaya ya Sheria ya Makosa ya Mtandao yanayolenga kudhoofisha vita dhidi ya ufisadi iliyotangazwa na Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais John Magufuli.

Mkurugenzi Mtendaji wa Jamii Media, Maxence Melo, wiki iliyopita, kupitia taarifa kwa vyombo vya habari, alieleza hatua iliyochukuliwa na mtandao huo katika kuhakikisha Watanzania wanapata haki ya kuibua matendo ya ufisadi kupitia mitandao na vyombo vya habari kwa jumla.

“JamiiForums imejijengea heshima na umaarufu kwa muda mrefu kutokana na namna inavyoendesha na kusimamia shughuli zake ambazo kwa kiwango kikubwa ni za kimtandao.

Mtandao wa JamiiForums ni mtandao mkubwa wa Kiswahili kwa Afrika Mashariki na

duniani ukiwa na wasomaji wasiopungua milioni 4 kwa mwezi ambapo kwa mwaka 2016,

mtandao huu unatimiza rasmi miaka 10 tangu uanzishwe.

“Mtandao huu unasifika kwa kutoa fursa ya kipekee kwa watumiaji wake kutoa yaliyo mioyoni mwao huku wengine wakijifunza mbinu kadha wa kadha za kijasiriamali, afya, elimu na hata kuibuka wanasiasa wapya waliofundwa na wana JamiiForums.

“Pamoja na kuendelea kutoa huduma hata katika nyakati ngumu, mtandao wa JamiiForums unakumbana mara kwa mara na changamoto nyingi zinazosababisha waanzilishi na

waendeshaji wake kuwa katika misukosuko mara kwa mara.

“Kwa takribani miezi mitatu iliyopita, Jeshi la Polisi limekuwa likiushinikiza mtandao huu (kwa njia ya barua rasmi) kutoa taarifa za baadhi ya wateja wake wanaoonekana kutoa taarifa zile ambazo kwa namna moja ama nyingine zinaibua ufisadi mkubwa na ukwepaji kodi.

“JamiiForums katika kuhakikisha inasimamia usiri (privacy) wa wateja wake, imekuwa ikihoji mashinikizo hayo yanazingatia sheria gani na kutaka kujua ni vifungu gani vya sheria ambavyo wadau wa mtandao huo wamevivunja bila kupewa maelezo yanayoridhisha zaidi

ya kuelezwa kuwa hatua zaidi zitachukuliwa kama hautatolewa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi.

“Baada ya kupata mashinikizo takribani manne yanayoashiria kuwa haki ya Watanzania watumiao mtandao wa intaneti na hasa watumiaji wa mtandao wa JamiiForums, Jamii Media imeshauriana na wanasheria wake na kuona ni wakati sasa wa kuilinda haki ya

wananchi kupata taarifa na kulindwa kwa Uhuru wao wa Maoni na Kujieleza inayolindwa kwa mujibu wa Katiba ya Nchi ibara ya 18 ambapo imefungua Shauri katika Mahakama Kuu ya Tanzania (Kesi namba 9 ya mwaka 2016); kutaka Sheria ya Makosa ya Mtandao,

kifungu cha 32 na 38 viangaliwe upya kwa kuwa vinasababisha kuvunjwa kwa haki za msingi za Watanzania watumiao mitandao ili kulinda maslahi ya umma kwa kuzingatia vifungu 26(2) na 30(3) vya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

“Mtandao wa JamiiForums utaendelea na shughuli zake kama kawaida na utaendelea kuwahakikishia watumiaji wake kuwa mahala salama pa kutolea madukuduku yao na hata kuisaidia Serikali kuonyesha nyufa zilipo kwa maslahi mapana ya Taifa (wakizingatia

mwongozo wa ushiriki wa mijadala anuai).

“Mwisho, JamiiForums inamuunga na itaendelea kumuunga mkono Rais Magufuli katika jitihada zake za kupambana na ufisadi kwa kutoa uwanja/fursa salama na rahisi kwa wananchi kuweza kuyaainisha yale wanayoyabaini kuwa yanachelewesha maendeleo ya Taifa lao.”