pg 1Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu (mstaafu), Cleopa David Msuya ameingia kikaangoni kutokana na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) inayozimiliki Kampuni za Tanzania Distillers Limited (TDL), Darbrew Limited na Tanzania Breweries Limited kuingia katika kashfa ya ukwepaji kodi na kutoa takwimu zinazotiliwa shaka kwenye ripoti ya mwaka.

Uchunguzi wa JAMHURI, unaonyesha kuwa uongozi wa TBL, chini ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Msuya na Mkurugenzi Mkuu Roberto Jarrin katika taarifa yao ya mwaka wa fedha unaoishia Machi 31, 2015 kwa wanahisa inayotoa hesabu za wa TBL zinazotofautiana na hivyo kutia shaka juu ya usahihi.

“Unapojua kuna kitu unataka kuficha, inakuwa kazi kweli kupatia wakati wote. Taarifa ile haina uhalisia. Mwenyekiti ana takwimu zake juu ya mauzo kushuka na faida waliyopata, na Mkurugenzi Mtendaji ana taarifa zake. Je, hii haituaaminishi kuwa ‘wanaumba’ hizi takwimu na kuwalisha upupu wanahisa?” kinahoji chanzo chetu cha habari.

Katika taarifa hiyo ya fedha ukurasa wa 6, Msuya aliwambia wanahisa hivi: “Tumepata ongezeko la asilimia 10 kwenye mauzo sambamba na kukua kwa faida ya uendeshaji ya asilimia 7 sawa na shilingi milioni 318,339. Pamoja na kupungua kwa wingi wa bidhaa zilizouzwa, mapato yatokanayo na mauzo yaliongezeka kutokana na kufanya marekebisho katika bei, kubana matumizi haswa ya uzalishaji, ongezeko la mauzo ya bidhaa zilizo na faida kubwa na ufanisi mkubwa kutoka kwenye vinywaji vikali na mvinyo.

“Kiwango cha mauzo ya bia kwa ujumla kilishuka kwa asilimia 6.5 kutokana na ongezeko la ushuru wa bidhaa, lakini kwa upande wa mvinyo na vinywaji vikali, mauzo yaliongezeka kutokana na kuhama kwa wateja wa bia kwenda kwenye vinywaji vikali. Ubora wa bidhaa zetu umebaki kuwa wa hali ya juu usiolinganishwa kutokana na uboreshwaji na mfumo endelevu wa ubora.

“Licha ya kushuka kwa mauzo, faida ya uendeshaji imeongezeka kwa asilimia 7 ukilinganisha na mwaka uliopita. Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) imeendelea kuwa moja ya vyanzo vikuu vya mapato serikalini kwa kulipa kodi mbalimbali kama kodi ya mapato, ushuru wa bidhaa na kodi ya ongezeko la thamani kama kampuni. Malipo hayo yalikuwa ni shilingi milioni 476,601, ongezeko la asilimia 15.8 zaidi ya mwaka uliopita.”

Wakati Msuya akisema walipata faida ya asilimia 7 sawa na shilingi milioni 318,339 (Sh bilioni 318.3), mauzo kushuka kwa asilimia 6.5 na kulipa kodi Sh milioni 476,601 (Sh bilioni 476.6), Mkurugenzi Mtendaji, Roberto Jarrin katika ripoti hiyo hiyo ya mwaka katika ukurasa wa 18 wa ripoti hiyo, anasema:

“Kampuni ya Bia Tanzania na washirika wake wameweza kufikia ongezeko la asilimia 7 katika faida ya uendeshaji ukilinganisha na mwaka uliopita licha kuanguka kwa mauzo kwa asilimia 4… Maboresho ya ufanisi na usimamizi mzuri wa gharama kuliwezesha faida ya uendeshaji kukua kwa asilimia 7 ukilinganisha na mwaka jana. Fedha zilizotokana na uendeshaji zilifikia shilingi milioni 365,312, ikiwa ni asilimia 16 zaidi ya mwaka jana.

“Kati ya fedha hizo, kiasi cha shilingi milioni 95,342 kilitumika kulipia kodi ya mapato, ikiwa ni ongezeko la asilimia 11.4, wakati kiasi kilichobakia kilitumika kulipia riba kwa mabenki, ununuzi wa rasilimali za kudumu, na malipo kwa wenye hisa.”

Ukiacha kiasi cha kodi ya makampuni kilichotajwa na Jarrin, takwimu nyingine zote walizotaja katika taarifa zao Msuya na Jarrin hazionekani kwenye mizania ya hesabu za TBL walizowasilisha na hapo ndipo mtaalam wa kodi kutoka TRA, alipoliambia JAMHURI. “Ndiyo maana tumechukua kompyuta zao. Tunataka watueleze hizo tofauti zinatokana na nini na takwimu walizotoa kwenye taarifa ya hesabu wamezipata wapi,” ameliambia JAMHURI kwa sharti la kutotajwa jina akisema suala hili lipo katika hatua ya uchunguzi.

Wataalam wa masuala ya kodi, wanasema Sh bilioni 476.6 wanazotamba kulipa ni upotoshaji kwa jamii kwani uhalisia walicholipa ni Sh bilioni 95 tu. “Hizo kodi wanazosema wamelipa ni uongo. Hii ni sawa na wewe mwananchi wa kawaida kwenda Benki ukalipa kodi ya gari, benki haiwezi kutamba kuwa imelipa kodi hiyo. Benki inakuwa ni wakala wa kukusanya kodi kutoka kwa wananchi.

“Katika hili la ushuru na VAT kampuni ya TBL inapotosha umma. TBL wanapokusanya ushuru na VAT wao wanakuwa ni wakala tu, si kwamba wanalipa hiyo kodi. Sawa na benki zisivyoweza kutamba na kudai zinalipa kodi kwa kukusanya fedha za walipakodi za ushuru na VAT, TBL wanafanya kosa kujihesabia kuwa wao ndio waliolipa kodi hizo. Huu ni upotoshaji,” anasema mmoja wa wachambuzi.

 

Muzo nje ya nchi

 Malalamiko makubwa yamekuwa ni kwamba TBL inawaibia wanahisa ikiwamo serikali kwa kushusha bei ya bidhaa kama konyagi na bia inazouza nje ya nchi. Kinachotajwa hapa ni kuwa Konyagi zinapouzwa nje ya nchi kwa bei ndogo, mwisho wa siku serikali za Tanzania na Kenya au nchi nyingine yoyote inayopokea Konyagi hizo inapata hasara.

Katika tishio lao la kwenda Mahakamani, TBL na wakurugenzi wa Bodi wanaodai wameaibishwa kwa gazeti la JAMHURI kuueleza umma kuwa wao ndiyo wakurugenzi wa Bodi na mambo haya ya ‘kipuuzi’ yanafanyika chini ya usimamizi wao, wanashiriki dhambi ya kuudanganya umma kuwa kushusha bei ya bidhaa zinazouzwa nje ya nchi hakuna madhara kwa nchi au kodi kwa maana bidhaa zinazouzwa nje ya nchi hazilipiwi kodi.

Kwa maelezo yao wanasema Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) inalipwa wakati chupa ya kinywaji inapozalishwa na hivyo bidhaa zinazouzwa nje ya nchi hazitozwi kodi ya aina yoyote.

“Uhalisia ni kwamba, mauzo nje ya nchi yanaposhushwa bei kwa zaidi ya dola 9 kama walivyofanya TBL kwa kuiuzia kampuni mama ni kwamba wao wanapata faida ya ziada, na mwisho wa siku kampuni haionekani kupata faida kubwa, hivyo wanakwepa kodi kwa njia hiyo.

“Hii maana yake ni kwamba, kama wangeuza kwa bei halisi, kampuni ya TBL ingepata faida kubwa na hivyo ikipata faida kubwa kuliko hicho kiasi walichokitangaza, maana yake ni kwamba ile asilimia 30 ya kodi ya makampuni inayotozwa kwenye faida itakuwa kubwa zaidi. Sasa wanachukulia kuwa Watanzania ni mbumbumbu na hivyo hawawezi kuelewa kinachoendelea kwa wao kukwepa kwa njia hii,” kinasema chanzo chetu.

 

TBL, Msuya, Mpugwe, Kileo watishia kesi

 Kampuni ya TBL na wakurugenzi akina Msuya, Arnold Kileo na Ami Mpungwe wametishia kulipeleka mahakamani gazeti la JAMHURI kwa kuchapisha taariza za kuonyesha taasisi yao inavyokwepa kodi.

Wakati TBL imejiegemeza kwenye neno tax avoidance, ambalo Kamusi ya Kiswahili sanifu (TUKI) inatambua neno hilo kama ukwepaji, kina Msuya wanasema wameharibiwa majina kwa kutajwa kuwa wao ni wajumbe wa Bodi ya TBL, kitu kilichoacha maswali mengi kwa kila anayejua ukweli kuwa watu hao ni wakurugenzi wa Bodi ya TBL.

Ingawa ibara ya 194(2) ya Sheria ya Makampuni Na 212 ya Mwaka 2002 inazuia wakurugenzi wa Bodi kuwa na umri zaidi ya miaka 70, ibara ndogo ya 5 inasema wanaweza kuombewa ruhusa kwenye Mkutano Mkuu kuteuliwa tena kutokana na ‘kazi nzuri’ waliyofanya kwa kutaja umri wao waendelee kuwa wakurugenzi. Wapo wakurugenzi waliozidisha miaka 70 hadi 80.

 JAMHURI, halikutaja umri wao, lakini Kileo, Msuya na Mpungwe, kwa hali ya kustaajabisha, katika barua yao ya kusudio la kwenda mahakamani, wanadai wameaibishwa kwa kutajwa kuwa wao ni wajumbe wa Bodi walioteuliwa na SABmiller kama kielelezo kivyochapishwa ukurasa wa kwanza inavyoonyesha.

 

Wajumbe wa SABmiller

 Ukurasa wa 10 na 11 wa Taarifa ya Hesabu za TBL Group unaonyesha kuwa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni hiyo ina wajumbe wa Bodi 23 kati yao wakiwamo Watanzania 12 ambapo mmoja anatajwa mara mbili kwenye bodi hiyo kutokana na wadhifa wake, kati ya Watanzania hao, Watanzania 10 wameteuliwa na SABmiller kusimamia masilahi yake na wawili tu ndio walioingia kwenye Bodi kutokana na nyadhifa zao serikalini.

Kuna tuhuma kuwa wajumbe wa Bodi wamekiuka mkataba wa wanahisa unaotaka TBL kuajiri wageni wasiozidi 5, na kwa hali ya kustaajabisha barua ya Kileo, Msuya na Mpungwe ya nia ya kulishitaki gazeti la JAMHURI kwa kuwataja kama wajumbe wa Bodi, imesema idadi iliyotajwa na gazeti hili ya wafanyakazi wageni kuwa ni 43 si ya kweli, bali uhalisia wapo 26. Tishio lao halikujibu hoja mkataba unaruhusu wawepo wangapi. Uhalisia ni watano tu.

Hoja ambazo hazijajibiwa na TBL inayodai Sh milioni 500,000 au wakurugenzi waliotishia kwenda mahakamani kudai fidia ya Sh milioni 600,000 kwa kutajwa kuwa ni wajumbe halali wa Bodi ya TBL, ni pamoja na kuuza Konyagi Kenya kwa bei ya dola 15.52 kwa katoni ikilinganishwa na Kampuni ya Kapari Limited ambayo awali ilikuwa inauziwa dola 24.78, kupunguza kodi ya makampuni kwa kuuza nje bidhaa kwa bei nafuu na kuajiri wageni wengi kinyume na mkataba wa ubinafsishaji.

 Wajumbe wa Bodi ya TBL Group Watanzania walioteuliwa na SABmiller wanaotajwa kupewa masilahi manono na kufumbia macho uozo wa kuajiri wageni wengi kuliko inavyotakiwa kisheria, kufanya ununuzi nje ya nchi kwa bei kubwa kuliko uhalisia, kuruhusu Konyagi kushushwa bei na hivyo Serikali kupata kodi kidogo, kuruhusu malipo ya tozo za uongozi nje ya nchi nao wametajwa.

Wajumbe hao wanaotumikia SABmiller kwani ndiyo iliyowateua ni, Mwenyekiti wa Bodi, Cleopa David Msuya tangu mwaka 2005, Balozi Ami Mpungwe tangu mwaka 2001, Ruth Mollel, ambaye mwaka 1997 aliteuliwa na Serikali kuiwakilisha TBL, lakini mwaka 2002 SABmiller ikamteua kuiwakilisha kwenye Bodi na amestaafu ujumbe Septemba, 2014 na Anold Kileo aliyeteuliwa na SABmiller tangu mwaka 1999. Mwingine ni P. J. I. Lasway, Mshauri wa Biashara aliyeteuliwa mwaka 2010.

Kabla ya kutaja wengine, mtu tuliyemtaja kama Ruth Mollel, amewasiliana na gazeti hili na kusema huyo aliyekuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais anayetajwa kwa jina la R. O. S. Mollel si yeye.

“R. anaweza kuwa Rehema, Rahabu au anything that stars with R. Si mimi,” alisema Mbunge wa Viti Maalum Mollel. Kwa nia njema na kutotaka kusumbuana na Watanzania, ngawa baadhi ya wananchi wanasema ndiye, kwa kuwa amesema yeye siye, gazeti hili linamuomba radhi Mollel kwa kutajwa, ingawa linavitaka vyombo vya dola kuthibtisha iwapo jina hili limetumika kimakosa au kwa ‘kufoji’ katika Bodi ya TBL.

Watanzania wengine ambao ni wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi kutokana na nyadhifa zao kama watumishi wa TBL Group wakati ripoti hii iliyochapishwa Machi, 2015 ni Mwanasheria wa TBL Group, S. F. Kilindo, Mkurugenzi Mtendaji wa TDL (aliyefukuzwa) Mgwassa, Mkuu wa Idara ya Vinywaji Baridi, K. Suma na Mkuu wa Utumishi, D. Magese.

Watanzania pekee wasio na uhusiano wa moja kwa moja na SABmiller katika Bodi hiyo ni aliyekuwa Katibu Mkuu wa Viwanda, Biashara na Masoko, Uledi A. Mussa, aliyeingia kwa wadhifa wake na E. Nyambibo, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, anayeiwakilisha Serikali hadi sasa.

Wachambuzi wa masuala ya biashara za kimataifa, wanasema kwa hali yoyote Watanzania walioteuliwa na SABmiller kuingia kwenye Bodi na wafanyakazi wa TBL Group wanaoingia kwenye Bodi kwa nyadhifa zao, kwa kila hali hawawezi kutetea masilahi ya Tanzania, bali ya SABmiller aliyewateua kuingia kwenye Bodi.

Wafanyakazi 43 wa kigeni wametajwa kuwa kila mmoja analipiwa tozo ya usimamizi ya dola 88,000 kwa mwaka sawa na dola 3,784,000 (Sh bilioni 8.3) zinazopelekwa kampuni ya Bevman Services International BV iliyoko Uholanzi, nchi inayotajwa kuwa pepo ya kodi (tax haven country).

Kiasi hiki kinatajwa kuwa ni njia ya kuchota fedha kutoka nchi zinazoendelea kwenda mataifa yaliyoendelea kwa kutumia kampuni tanzu na kinaweza kusitishwa kwa kurejea katika mkataba unaowataka kuajiri wafanyakazi wa kigeni watano tu.

Ukiacha hiyo tozo hiyo ya usimamizi, wafanyakazi hao 43, ambao akina Msuya wamesema ni 26, wanalipwa mshahara kati ya dola 9,000 (Sh 19,800,000) na dola 15,000 (Sh 33,000,000) kwa mwezi. Ukizidisha mara miezi 12 ikiwa utachukua wastani wa dola 12,000 (sh 26,400,000) kwa kila mfanyakazi kati ya hao 43 inakuwa sawa na dola 6,192,000 (Sh bilioni 13.6) kwa mwaka.

“Kiasi hiki ukikichanganya na zile bilioni 8.3 nchi inapoteza mapato mengi mno,” kinasema chanzo chetu na kutaka nafasi za wageni zishikwe na wazawa.

TRA wakamata kompyuta

Chanzo cha kuaminika kimelijulisha gazeti hili la JAMHURI, linaloaminika kwa habari za uchunguzi lililosifiwa na Rais John Mafuguli kwa kufukua uozo katika mita za kupimia mafuta na maeneo mengine Februari 13, mwaka huu kuwa ni gazeti la uchunguzi makini, kwamba maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania wamevamia TBL baada ya gazeti hili kuchapisha habari za ukwepaji kodi wiki iliyopita na wamechukua komputa tatu.

“Tunaamini kompyuta tulizozichukua zina takwimu muhimu kwa ajili ya kubainisha kodi waliyostahili kulipa na kiasi walicholipa,”anasema mtoa habari.

Pamoja na kuangukia kwenye kundi la walipa kodi wakubwa, uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa kwa mbinu na utaratibu wanaofanya unawafanya walipe kidogo

 

Kapari Limited Wazungumza

Katika toleo lilipia JAMHURI limezungumza na Kampuni ya Kapari Limited ya Jijini Nairobi, Kenya inayokiri kuwa uamuzi wa TBL Group kuwabadilishia masharti ya biashara umewaumiza kwa kiasi kikubwa. Kampuni hiyo imesema ilianza biashara kwa taabu mwaka 2008 ikipigwa vita ya hali ya juu, huku viwanda vya Kenya vikifanya kampeni mbaya dhidi ya Konyagi vikiitangaza kama Chang’aa ikakosa soko, lakini baada ya kukubalika sokoni TBL Group ikabadilisha masharti ya Mkataba.

“Kwa mwaka 2008, kontena moja tuliliuza kwa miezi sita. Tulikuwa na wafanyakazi, tumekodi maghala, lakini Konyagi ikawa inatangazwa vibaya kuwa hiyo ni Chang’aa ya Tanzania. TBL wala hawakuwa na mpango wa kuizua Konyagi nchini Kenya. Kulikuwa na ugumu wa aina yake.

“Tuliendelea kuiuza kwa tabu, na ilipofika mwaka 2012 ndipo biashara ikaanza kuwa nzuri. Mwaka 2013 na 14 mwanzoni, tukaanza kuuza hadi kontena 15 kwa mwezi. Konyagi ikapendwa Kenya na ilikuwa inaelekea kuwa spiriti namba moja kwa mauzo. TBL walivyoona hivyo, wakaamua kuipa biashara kampuni yao inaitwa Crown Beverage.

“Crown Beverage wao waliangalia tunachouza, lakini hawakujua tunatumia mifumo gani kusambaza Konyagi na kama tulikuwa tunapata tasilimu kwanza au tunakopesha. Ghafla tukabadilishiwa masharti. Tukaambiwa tutauza Nairobi tu, na Crown Beverage watauza nchi nzima eneo lililosalia.

“Kwetu hii, haikuwa sahihi kwani tulikuwa tumeajiri watu wengi, tulikuwa tumefungua maghala, tulikuwa tumechukua mikopo benki na kununua malori 10 ya kusambaza Konyagi nchi yote ya Kenya, hivyo kilichotokea baada ya uamuzi huu biashara ikafa.

“Ninachokiona, sisi tumepoteza, Serikali ya Kenya imepoteza na Serikali ya Tanzania imepoteza. Tumepoteza wote kutokana na TBL kuwauzia Crown Beverage kwa dola 15 kwa katoni, wakati sisi walikuwa wanatuuzia dola 24. Hiyo kwa upande wa Serikali za Kenya na Tanzania wamepoteza kodi.

“Sisi kama wafanyabiashara tumevuruga soko. Crown Beverage wanajitangaza kuwa wao ndiyo wenye kuuza Konyagi kihalali, hali iliyoleta ushindani usio wa lazima katika soko, ikawaogopesha wateja na sasa biashara inashuka. Mimi naona sote tumepoteza, na wakati umefika sasa tukae chini tuzungumze, TBL iangalie ilikuwa inapata fedha kiasi gani kutoka Kenya na sisi tuonyeshe kodi tulizokuwa tunalipa turejee katika biashara. Tumepoteza asilimia 80 ya biashara,” anasema Meneja wa Kapari Limited Peter Manga.

 

Crown Beverege wazungumza

 Meneja Mkuu wa Crown Beverage Kenya, Ellis Muhimbise, amezungumza na JAMHURI akiwa jijini Nairobi na kusema yeye haoni tatizo kwa TBL kuamua kuwauzia Konyagi wao kwani ni kampuni dada.

Alipohojiwa kwa nini wanapewa bei ndogo ikilinganishwa na ya Kapari Limited, akasema: “Hii ni biashara kati ya kampuni na kampuni zenye udugu, hivyo usitaraji tutauziwa bei sawa na mteja wan je.”

JAMHURI lilipomhoji kwa nini hawatumii kanuni ya biashara ya kimataifa inayozitaka kampuni zenye udugu kuuziana bidhaa kwa bei ya soko (arm’s length principle – ALP), akasema: “Hii ni mipango ya ndani.”

Muhimbise, alikiri Serikali ya Kenya kufungua kesi dhidi yao na kudai kodi kubwa, hata hivyo akasema: “Suala hili lilijitokeza, tumelishughulikia na sasa ni kama limefungwa.”

 

Ukwepaji wa kodi

 Wachunguzi wa masuala ya kodi wanasema TBL imefanya utaratibu maalum wa kukwepa kodi kwa kuamua kuiuzia konyagi kampuni dada ya Crown Beverage nchini Kenya inayomilikiwa na kampuni mama ya SABmiller, hali inayopunguza mapato ya TBL kwa mwaka, hivyo kuchangia ilipe kodi ya mashirika ndogo.

Ukiacha ujanja huo, wanaofanya kwa kutumia udhaifu wa mfumo wa kisheria na hivyo kulitishia gazeti hili kuwa watakwenda mahakamani kulishitaka kwa kuanika uozo huo, kwa kuchezea vichwa vya Watanzania kutokana na maneno ya kisheria ya Kiingereza ya Tax Evasion na Tax Avoidance, ambayo Kamusi ya TUKI toleo la 3 ya mwaka 2006 imethibitisha pasipo shaka kuwa maneno yote yanamaanisha ukwepaji kodi, wanasema wao ni walipaji wazuri.

 

Mauzo yashuka

Taarifa lilizonazo gazeti hili zinaonyesha kuwa mauzo ya Konyagi  nchini kama unavyoonyesha mchoro katika ukurasa wa kwanza yameshuka kwa zaidi ya asilimia 40 tangu Mtanzania David Mgwassa aliyekuwa anaongoza TDL alipotimuliwa kazi.

Zinaonyesha kuwa wageni wamekuw awakiruhusu fedha kupelekwa nje ya nchini kwa kuweka mazingira ya kuonyesha kuwa bidhaa za kuzalishia bia na konyagi zinauzwa bei gari, kinyume na uhalisia.

 

TBL wakwepa ukweli

 Katika tangazo walilotoa kwa vyombo vya habari, TBL wamekwepa kujibu hoja za msingi zilizotolewa katika toleo lililopita kuwa wanakwepa kodi kwa kujiuzia vinywaji kutoka Tanzania kwa bei nafuu katika nchi za kigeni.

TBL walishindwa pia kufafanua kwa nini hawafuati sheria za kimataifa zinazowataka wanapoziuzia kampuni tanzo bidhaa zao kuuza kwa bei ya soko. Wenye hisa pia wanahoji: “Hivi wanavyouza kwa bei nafuu Kenya, hii maana yake si kwamba sisi tunapoteza katika malipo yetu ya hisa?” alihoji mwanahisa.

Mkurugenzi Mtendaji wa TBL, Roberto Jarrin amezungumza na JAMHURI Jumatano iliyopita katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere, Dares Salaam, na kusemaTBL ni kampuni iliyoandikishwa katika soko la hisa la Dar es Salaam, hivyo akasema inafuata sheria na kanuni zote za uwekezaji.

 Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Dk. Adelhem Meru, ameliambia JAMHURI Jumatano iliyopita jijini Dar es Salaam kuwa wamepata taarifa za Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) wanavyokwepa kodi kupitia JAMHURI.

 “Lakini kwa upande wa Serikali masuala ya kodi yanafanyiwa kazi na TRA (Mamlaka ya Kodi Tanzania), nadhani ingekuwa vema wao wakakufafanulia hili,” anasema Dk. Meru.

Kwa upande wa TRA, mmoja wa maofisa kutoka Kitengo cha ukusanyaji kodi za kampuni kubwa, amelithibitishia JAMHURI kuwa wameanza kufuatilia kwa kina namna TBL wanavyolipa kodi.

“Ndiyo kwa kipindi cha miaka mitano, TBL imekuwa ikifanya vema ikilinganishwa na makampuni mengine hasa makubwa, lakini swali la kujiuliza hapa, ni je, hicho kinacholipwa kinastahili kulipwa na TBL? Kuna kampuni ndogo, zinalipa kodi inayostahili, lakini zipo kubwa ambazo zinalipa kodi, lakini si ile inayostahili.

“Taarifa yenu tumeipokea na nikwambie tu kwamba kuanzia siku gazeti limetoka, tumefanyia kazi taarifa ile na kufuatilia kwa kina. Of course (bila shaka), TBL wametuambia kwamba watatoa ufafanuzi kwenye matangazo kupitia magazetini ili umma ufahamu. Hilo halituhusu, ila sisi tunalifanyia kazi kitaalamu.

“Tunafanya kazi si kwa TBL tu, ni kwa makampuni nyingi na ndio maana utasikia hata makampuni ya simu yamelipa malikimbikizo makubwa ya kodi. Kwa sasa kampuni yoyote kubwa ikija na kutoa sababu tunasema tu, unatakiwa kulipa na tunawabana walipe au tunawaambia nenda kajieleze mwenyewe kwa wakubwa halafu uje na kimemo.

“Hivi sasa hakuna vimemo, ni kulipa tu. Hakika suala la kuwaona wakubwa limekuwa gumu na hili linatusaidia kweli sisi TRA kufanya kazi, ndiyo maana tunakusanya kodi kubwa,” anasema.

4335 Total Views 4 Views Today
||||| 4 I Like It! |||||
Sambaza!