Mwigulu NchembaWakazi wa Jiji la Dar es Salaam wameomba Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Bodi ya Nyama kuchukua hatua

ya kuzifunga machinjio zilizokithiri kwa uchafu jijini humo.

Wameieleza JAMHURI kwamba kero ya uchafu uliokithiri katika Machinjio za Kimara Suka, Vingunguti, Ukonga, Mbagala na Tegeta, umechangiwa na utendaji mbovu wa taasisi hizo na ukiritimba unaolenga maslahi binafsi.

Awali usimamizi wa machinjio yote ulikuwa unasimamiwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo nchini kabla ya majukumu yake kupewa taasisi hizo zinazoonekana kushindwa kufanya kazi iliyokusudiwa na wakati mwingine hujikuta wakigongana katika jukumu moja.

Akielezea suala hilo, Mohamed Abdallah, mkazi wa Vingunguti, Dar es Salaam, anasema Serikali inapaswa kurejesha huduma zote zinahusu mifugo hadi ukaguzi wa nyama katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo badala ya kuwa na taasisi nyingi zinazofuatilia suala moja huku matokeo ya utendaji wake yakiwa hafifu.

“Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo yeye ndiye mhusika mkuu wa mifugo na jukumu lake linaishia pale mfugo unapochinjwa, TFDA wanaanzia ndani ya machinjio, Bodi ya Nyama, NEMC wao wanakuwa nje ya machinjio kwa ajili ya kulinda mazingira na Manispaa kazi yao ni kukusanya ushuru tu.

“Huu ni urasimu na lengo la kupokonya mamlaka yaliyokuwa yakisimamiwa moja kwa moja na Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo na kulinda maslahi ya watu wachache wenye ubinafsi,” anasema mwananchi huyo.

Kwa kupunguza kero za machinjio Dar es Salaam, Serikali ilijenga machinjio makubwa ya kisasa Ruvu ili mifugo inayotoka mikoani iishie huko, na nyama tu isambazwe katika maeneo yote ya jiji, lakini hadi sasa hakuna kinachoendelea kuhusu machinjio hayo.

Pamoja na kutokamilika kwa ujenzi wa machinjio hiyo, yaliyopo sasa yalijengwa zaidi ya miaka 30 iliyopita kabla ya ongezeko la idadi ya wakazi wa jiji hilo huku idadi ya mifugo iliyokuwa ikichinjwa ikiwa kati ya ng’ombe 30 hadi 40 kwa siku kwa chinjio moja.

Licha ya kuwa na miundombinu chakavu, JAMHURI imebaini machinjio ya Vingunguti na Ukonga yanachinja ng’ombe 800 hadi 1,000 kwa siku zaidi ya uwezo wake, huku kasi ya uharibifu wa mazingira ikizidi kukithiri na taasisi zinazohusika kuamua kufumbia macho suala hilo na maisha ya wananchi waishio jirani na machinjio hayo kuwa hatarini kukumbwa na magonjwa ya mlipuko.

 

NEMC

Mara kadhaa NEMC imekuwa ikizikumbusha mamlaka za afya na mazingira katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam pamoja na Manispaa zake tatu za Ilala, Kinondoni na Temeke kusimamia sheria za usafi wa mazingira katika machinjio yote yaliyomo ndani ya jiji lakini hakuna hatua zinazochukuliwa.

Mapema mwaka jana, NEMC iliyafunga machinjio ya Vingunguti, Ukonga, Mbagala na Tegeta kwa sababu ya uchafu uliokithiri katika machinjio hayo. 

Kwa kutumia Sheria ya Hifadhi ya Mazingira ya mwaka 2004 (Environmental Management Act 2004 and Environmental Impact Assessment and Audit Regulation of 2005), Mkurugenzi Mkuu wa NEMC aliyafunga machinjio ya Punda yaliyoko Western Industrial Area mkoani Dodoma, yaliyokuwa yakimilikiwa na wawekezaji kutoka China kwa kutumia hati ya dharura ya ulinzi.

Sababu za kufungwa kwa machinjio hayo ya Punda ya Huacheng ni kampuni hiyo kutokuwa na hati ya uhifadhi wa mazingira, kutiririsha maji machafu bila ya kuyadhibiti na udhibiti hafifu wa taka ngumu.

Hata hivyo, NEMC imelalamikiwa na wananchi kwa kushindwa kutumia sheria hiyo ya hifadhi ya mazingira kuzifunga machinjio za Dar es Salaam zinazotiririsha uchafu wa damu na kinyesi cha ng’ombe kwenye makazi ya watu ikiwamo machinjio ya Kimara Suka.

Imeelezwa kwamba hata hatua zikichukuliwa na Baraza hilo linakosa nguvu kutokana na minyukano ya rushwa huku kila taasisi ikitumia mamlaka yake kujinufaisha binafsi badala ya kulenga maslahi ya umma.

 

Wakazi wa Kimara waeleza

Mwaka 2012 wakazi wa Kimara Stopover walifanya vikao ili kuondokana na kero hiyo na kuomba Manispaa ya Kinondoni kufunga machinjio ya Kimara Suka hadi mmiliki wake atakapochimba shimo la kuhifadhia uchafu badala ya kuuelekeza katika makazi ya watu. 

Wanasema baada ya madai yao kutopatiwa ufumbuzi, waliamua kufungua shauri katika Baraza la Kata ya Saranga lililopewa Na. 110 la mwaka 2013 lililohusu kero wanayoipata ya harufu mbaya ya kinyesi na damu. 

Katika shauri hilo, mdai Chinollo Victor Ndunguru akiwawakilisha wananchi 72 wa mashina namba 5 na 27 wa mtaa wa Stopover dhidi ya Yahaya Saidi Singano, mmiliki wa machinjio hayo ya Suka. 

Baraza hilo liliridhika na malalamiko ya wananchi wa mtaa wa Stopover kutokana na kero ya harufu mbaya inayowapata na kwamba machinjio hayo yako katika makazi ya watu na pia karibu mno na Barabara Kuu ya Morogoro. 

Hata hivyo, Baraza hilo liliamuru machinjio hayo yafungwe ili wananchi waondokane na kero hiyo ya harufu mbaya inayotokana na kuzagaa kwa kinyesi na damu katika makazi yao. 

Naye, Mjumbe wa Mazingira wa Mtaa wa Stopover, Godfrey Misana, ameieleza JAMHURI kwamba kero hiyo ni ya muda mrefu na hata Baraza lilipotoa amri ya kufungwa kwa machinjio hayo waliona tena yakifunguliwa bila kufahamu nini kilichojitokeza na imefunguliwa tena kwa maelekezo ya nani. 

Misana anasema machinjio hayo yameendelea na uchafuzi wa mazingira katika makazi ya watu huku Manispaa ikiendelea kukusanya mapato kwa kila ng’ombe anayechinjwa kutozwa ushuru wa Sh 5,000, lakini mmiliki hataki kuboresha miundombinu na kuwaondolea kero wananchi. 

Anasema wakati mwingine idadi ya mifugo inayochinjwa inafikia zaidi ya 200 kwa siku moja, lakini wahusika hawaangalii kero inayowakabili wananchi kwa kuchimba shimo la kuhifadhia uchafu huo, na badala yake wamekuwa wakiangalia mapato tu. 

Ofisa Mifugo wa Manispaa ya Kinondoni, Mbonea Mgonja, ambaye pia ni msimamizi wa machinjio yote ya Manispaa hiyo, alipohojiwa na JAMHURI anasema kwamba machinjio yote yanamilikiwa na manispaa lakini wananchi wameyafuata maeneo hayo. 

 

Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo

Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo, Dk. Abdu Hayghaimo, alipohojiwa na JAMHURI kuhusu kero za uchafu unaohatarisha maisha ya wananchi kutoka katika machinjio za Dar es Salaam, anasema kwa sasa ofisi yake haihusiki na usimamizi wa machinjio hayo.

Anasema wananchi wengi wamekuwa wakifikisha malalamiko yao katika ofisi yake kuhusu kero zinazotokana na uchafu wa machinjio hizo lakini wahusika kwa sasa ni uongozi wa manispaa, NEMC na TFDA. 

 

TFDA wakwepa lawama

Meneja wa Mawasiliano na Uhusiano wa TFDA, Gaudensia Simwanza, ameieleza JAMHURI kuwa licha ya kugongana kwa taasisi hizo katika kutekeleza majukumu yao, wamekuwa wakishirikiana kwa pamoja.

Simwanza anasema kwa kushirikiana na halmashauri ambao wamekuwa wakitoa wataalamu wao wa Afya na Mifugo kufanya ukaguzi kwenye machinjio na mabucha kuhakikisha wananchi wananunu nyama iliyo na ubora.

“Tuliyafungia machinjio ya Suka, Vingunguti na machinjio ya kuku Shekilango kutokana na uchafu uliokithiri hadi wamiliki wa machinjio hayo walipoyafanyia marekebisho.

“Machinjio ya Suka hayakuwa na vyoo, matangi ya kuhifadhia maji na mazingira yake kwa ujumla yalikuwa machafu kupita kiasi,” anasema.

Alipoulizwa kuhusu machinjio hayo kuendelea kutiririsha uchafu wa damu na kinyesi cha mifugo inayochinjwa kwenye makazi ya watu wakati wanadai awali waliifunga kwa uchafu uliokithiri, anasema kwa kushirikiana na taasisi ikiwamo NEMC, wanaendelea kuwakumbusha wahusika kuthamini afya za watu wote.

2730 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!