Padre Dk Faustin Kamugisha
Uvumilivu au ustahimilivu ni siri ya mafanikio. Uvumilivu ni kuanguka mara 99 na kuinuka mara
ya 100. Katika msingi huu Julie Andrews alisema, “Uvumilivu ni kushindwa mara 19 na
kushinda mara ya 20.” Matone yanayodondoka mwishowe humomonyoa mwamba. Ni methali
ya China. “Kama Columbus angerudi alikotoka, hakuna mtu yeyote ambaye angemlaumu.
Lakini hata hakuna mtu yeyote angemkumbuka,” alisema R.B. Zuck.
Miguu ya Christopher Columbus (1436-1506) mtalii, nahodha, baharia, mvumbuzi ilikuwa miguu
ya kwanza ya mtu wa Ulaya kukanyaga Amerika ya Kaskazini. Safari ya baharia huyu iliibadili
Marekani. Mafanikio yanahitaji muda na uvumilivu.
Kuna hadithi ya mtu ambaye alipita karibu na tembo. Alishangaa kuona wanyama hawa
wakubwa wameshikiliwa kwa kamba ndogo ambazo zilifungwa kwenye mguu wa mbele wa kila
tembo. Hapakuwapo na mnyororo. Na wala hawakuwekwa kizimbani. Ni ukweli usioficha kuwa
tembo hawa wangetaka kutoka walikofungiwa wangetoka, lakini hawakufanya hivyo.
Mtu huyo alimuuliza mfundishaji wa tembo namna gani anaweza kuwafunga tembo kwa kamba
ndogo. Mfundishaji huyo alisema: “Tembo wakiwa wadogo na wenye umri mdogo tunatumia
saizi ya kamba hii kuwafunga. Inatosha kuwashikilia. Wanapokua wanawekwa kwenye hali ya
kuamini kuwa hawawezi kukata kamba na kutoka. Wanaamini kamba bado inaweza
kuwashikilia, hawawezi kujiweka huru.”
Kama tembo, baadhi ya watu tunaishi tukiamini kuwa hatuwezi kufanya jambo la kutuletea
mafanikio kwa vile wakati fulani tulijaribu na kushindwa.
“Haijalishi kama unatembea polepole, ilimradi husimami,” alisema Conficius. Polepole ndiyo
mwendo. Tofauti kati ya kushinda na kushindwa ni nguvu ya kuvumilia. Mvumilivu hula mbivu.
Kuwa kama stempu kwenye bahasha. Haitoki kwenye bahasha mpaka bahasha imemfikia
mlengwa. Baada ya onyesho zuri sana la muziki Ludwig van Beethoven alikuwa amezungukwa
na marafiki na mashabiki wake wakimpongeza alivyolimudu piano, mwanamke mmoja alipaza
sauti na kusema: “Ee, bwana, kama Mungu angenipa zawadi ya akili nyingi sana! Si akili nyingi
sana, mama, na wala si uchawi. Unachotakiwa kufanya ni kufanya mazoezi kwenye piano
masaa manane kila siku kwa muda wa miaka arobaini unakuwa mtaalamu kama nilivyo.”
Kufanya mazoezi kila siku ya muziki au jambo jingine, uvumilivu unahitajika.
Tuna mifano ya watu mbalimbali ambao walifanikiwa kutokana na nguvu ya uvumilivu. Kuna
kijana ambaye alijiunga na chuo kilichoitwa State Teachers College huko Warrenburg,
Marekani. Alikuwa maskini sana. Alitumia farasi kusafiri mwendo wa maili tatu kuhudhuria
masomo. Alikuwa na suti moja tu. Alijaribu kucheza mpira lakini alikataliwa. Wazo la kujidharau
lilianza kujengeka.
Mama yake alimwambia ajaribu kufanya kitu ambacho kitaonesha uwezo wake wa kweli.
Alijaribu mambo ya kuzungumza mbele ya hadhara. Lakini mwanzoni alishindwa katika hili. Kila
alilolijaribu alishindwa. Kijana huyu ambaye anaitwa DALE CARNEGIE aliendelea kuvumilia na
kujaribu na baadaye kuwa mwalimu mashuhuri wa ufundi wa kuzungumza kadamnasini katika
historia ya dunia.
Yeye ambaye alishindwa kuzungumza mbele ya hadhara wakati fulani alikuwa meneja wa radio
na alitengeneza mtaala wa kufundishia somo la namna ya kujipatia marafiki na kuwashi watu.
Jambo hili lilimfanya awe milionea.
“Kupitia kufanya kazi kwa bidii, uvumilivu na imani kwa Mungu unaweza kuziishi ndoto zako,”
alisema Ben Carson. Hakuna mtu aliyefanikiwa bila kuwa na sifa ya uvumilivu. Mungu anabariki
uvumilivu. Ufanye uvumilivu uwe rafiki yako. Mtu anaweza kushindwa si kwa sababu ya
kutokuwa na kipaji bali kwa sababu ya kutokuwa na uvumilivu. Kuna hadithi juu ya konokono
aliyechekwa alipokuwa anapanda mti kwa spidi ndogo kutafuta matunda. Aliambiwa kuwa
hakuna matunda juu ya mti. Konokono alijibu: “Mpaka nifike juu ya mti yatakuwa yamejitokeza
na kuiva.” Vumilia.

Please follow and like us:
Pin Share