Home Makala Mafanikio yoyote yana sababu x (1)

Mafanikio yoyote yana sababu x (1)

by Jamhuri
Wanatoka tumbo moja lakini hawafanani. Ni methali ya Tanzania. Watoto wenye wazazi walewale, walionyonya titi lile, na kusoma shule ile ile kimafanikio wanatofautiana. Kinachowatofautisha ni sababu x.
Wanadarasa wakiwa na viwango tofauti vya ufaulu darasani. Inatokea aliyetangulia darasani hapati mafanikio katika maisha kuzidi aliyekuwa wa kumi. Tofauti ni sababu x. Sababu x ni siri ya mafanikio.
Watu wanatoka chuo kimoja wamefundishwa na walimu wale wale. Utendaji kazi wao na mafanikio yanakuwa tofauti. Sababu nyuma ya hayo yote ni sababu x. 
Ukweli kwamba kuna sababu x ya mafanikio unabainishwa na mhubiri katika Biblia: “Tena nimeona kitu kimoja hapa duniani, kwamba wenye mbio hawafaulu katika riadha, wala wenye nguvu hawashindi vita; wenye busara hawapati chakula, wenye akili hawatajiriki; wala wenye ujuzi hawapandi vyeo; lakini wakati wa bahati huwapata wote pamoja” (Mhubiri 9: 11).
Watu wana wakati ule ule. Tajiri mkubwa sana Bill Gate wa Marekani ana masaa ishirini na nne kwa siku. Maskini sana wa makazi duni ya SOWETO Afrika ya Kusini au Kibera nchini Kenya ana masaa ishirini na nne kwa siku. Tofauti inaletwa na sababu x.
Kufanya mambo tofauti na wengine wanayofanya ni sababu x. Kuna aliyeweka sababu x katika maneno haya: “Amini wakati wengine wana mashaka. Panga wakati wengine wanacheza. Soma wakati wengine wamelala. Amua wakati wengine wanachelewa. Andaa wakati wengine wanaota ndoto za mchana.
Anza wakati wengine wanasitasita. Fanya kazi wakati wengine wanategemea kufanya kazi. Weka akiba wakati wengine wanatapanya hovyo. Sikiliza wakati wengine wanazungumza. Tabasamu wakati wengine wanakasirika. Toa sifa wakati wengine wanapaka matope. Vumilia wakati wengine wanajiuzulu.”
Sababu x ni kufanya mambo tofauti, bora na mazuri. Mafanikio ya mtu mkubwa ni kufanya lile ambalo wengine hawatafanya.
Katika methali za Kiswahili sababu x inaitwa bahati. Inasemwa bahati ya mwenzio isikulaze mlango wazi. Wanachokiita bahati wahenga wengine wanakiita “neema.” Mfano wa methali ya wahenga wa Kihaya: Neema ni kama baridi hata ukifunga mlango inaingia.
Kuna mtu aliyemuuliza mwandishi wa Ufaransa Jean Costeau kama anaamini katika bahati: “Bila shaka, namna gani unaeleza mafanikio ya wale usiowapenda?” Baadhi ya watu huwa wanatoa sababu ya bahati kama siri ya mafanikio ya wale wasio wapenda. Lakini tukumbuke bahati umwendea yule aliyejiandaa.
Zimetolewa sababu x kwa utajiri. Kuna aliyesema: “Matajiri hawafanyi kazi kwa ajili ya fedha. Wanafanya fedha ifanye kazi kwa ajili yao.” Hiyo ni sababu x.  Jim Collins Mtaalamu wa Manejimenti ya biashara alisema: “Sababu x ya uongozi uliotukuka si haiba, bali ni unyenyekevu.”
Aliona unyenyekevu ni siri ya mafanikio katika uongozi. Katika ulimwengu wa kuuza na kununua kuna aliyesema: “Watu wanamnunua mtu kabla ya kununua kitu chake.” Ukweli huu ulibainishwa na Seth Godin pia: “Watu hawanunui bidhaa na huduma. Wananunua mahusiano, hadithi…” Kumuona mteja kama mfalme ni jambo muhimu.
Kuna ambao wameona sababu x ni Mungu. Methali za Kiswahili zinasema yote: “Aliyekupa wewe kiti ndiye aliyenipa mimi kumbi.” Mungu akikupa kilema, hukupa na mwendo wake. Mungu hatoi kwa mvua, wala hanyimi kwa jua. Mtu aliyefanikiwa ni yule anayemwacha Mungu atawale akili zake, mwili wake na kitabu chake cha fedha.
“Mafanikio ni kuishi kwa namna ambayo unatumia vile Mungu alivyokupa – akili yako, uwezo wako na nguvu zako kufikia lengo ambalo analenga kwa maisha yako,” alisema Kathi Hudson.
Alexander Maclaren alipoulizwa juu ya mafanikio katika utume alijibu: “Nimegundua kuwa faraja yangu na utendaji wangu vimewiana moja kwa moja na wingi na kina cha mazungumzo yangu na Mungu kila siku. Siri ya mafanikio  katika kila kitu ni kumtumaini Mungu na kufanya kazi sana.”

You may also like