Mafisadi wajipanga

*Ni vigogo wazito serikalini, waanza figisu ujenzi wa reli ya SGR

*Washirikiana na wazabuni wa nje kuhujumu ‘Lot 3’ na ‘Lot 4’

*Waanzisha kundi wakijiita wazalendo, latajwa ni fedha mbele

*Kenya walipigwa bilioni 18.4 kila kilomita, wailengesha Tanzania

DODOMA

Na Mwandishi Wetu

Sikio la kufa halisikii dawa. Hili ndilo linaloweza kusemwa kutokana na baadhi ya wanasiasa na watendaji serikalini kuanza mpango wa hatari wa kukwamisha ujenzi wa Reli ya Kati ya SGR; JAMHURI limebaini.

Mpango huo unaosukwa kwa umakini mkubwa, una malengo mawili. Kwanza, kujipatia fedha kwa njia yoyote ile na pili ni kuihujumu Serikali ya Awamu ya Sita kuonyesha kuwa haiwezi kusimamia ujenzi wa reli kama ilivyokuwa awali.

Hivi karibuni kumekuwapo taarifa inayosambazwa na watu wanaojiita ‘wazalendo’ ikitoa shutuma za kuhusu mchakato wa ununuzi unaoendelea vipande viwili; ‘Lot 3’ na ‘Lot 4’, wakitaka utumike utaratibu uliokwamisha ujenzi wa reli tangu enzi za uhuru.

Kuna mgogoro mkubwa unapikwa chini kwa chini na baadhi ya wanasiasa na wataalamu wakitaka vipande viwili vya reli vya kutoka Makutupora hadi Tabora (Lot 3) na Makutupora hadi Isaka (Lot 4) zabuni itangazwe tena, waingize kampuni zao.

Tayari kuna kampuni kadhaa kutoka China ambazo zimewasilisha serikalini nia ya kujenga vipande hivyo na bei wanayotaka kutoza hata kabla zabuni haijatangazwa.

Mbaya zaidi, moja ya kampuni zilizoomba mwaka 2015, iliomba kujenga reli yote kwa gharama ya dola milioni 6.2 kwa kila kilomita, sawa na Sh bilioni 14.26 kwa kilomita. 

Kwa urefu wa reli unaojengwa wa kilomita 1,063 kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza, mkandarasi huyu alitaka alipwe dola za Marekani bilioni 6.59, sawa na Sh trilioni 15.2 za Tanzania.

Ukiacha ughali wa gharama, uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa mkandarasi huyu na wengine walikuwa na upungufu mkubwa uliomsukuma hayati Rais Dk. John Magufuli kuwakataa.

“Muhimu Watanzania wakajua hili group (kundi) la wanaojiita wazalendo ni kina nani. Kwa kudokeza tu hili ni group la watu ambao wanatetea masilahi binafsi, hasa kwa sababu tayari walishakula huko nyuma na wanataka ‘ku-retire imprest’,” anasema Ofisa Mwandamizi kutoka Wizara ya Fedha na kuongeza:

“Huu ni mlolongo wa matukio. Mwaka 2016 serikali ilipoanza hatua za ujenzi, kampuni pekee iliyojitokeza kuunga mkono serikali ilikuwa Kampuni ya Yapi Merkezi. Katika hatua za awali zilijitokeza kampuni 40, lakini wakati wa kurudisha zabuni kampuni 39 kutoka China zote zilijitoa. Cha kusikitisha hata benki moja ya China iliyokuwa imeahidi kutoa fedha, ilikataa ikitoa sababu zisizokubalika.

“Kwanza, benki hiyo ilisema Tanzania imeamua kujenga reli kufuata ‘standards’ (viwango) za kimataifa, yaani kwa kufuata AREMA Standard. Wao hawakulifurahia hili kwa sababu walitaka kufuata standard za Kichina, ikiwa na maana vitu vyote viwe vya Kichina. Kama kuna mtu haelewi tunachozungumza, waulize majirani zetu Kenya. Walifanyiwa mchezo huu.

“Pili, hawakutaka Tanzania ijenge reli kwa kutumia teknolojia ya mawasiliano ya kisasa, yaani ‘European Level 2 (digital)’, ambayo ndiyo inayotumiwa duniani kote. Walitaka kutuletea teknolojia ya zamani (analogy) kama ya Kenya.

“Tatu, hawakutaka kutumia upembuzi yakinifu wa kwetu. Walitaka wafanye upembuzi wao mpya, na watwambie wanatujengea kwa bei gani. Walitaka makandarasi wote watoke kwao, ‘consultant’ wa mradi wa kwao, ‘design’ Mchina, ‘insurer’ wao na pengine mwishoni kuwa na masharti ya kuendesha wao kama walivyowafanyia majirani zetu. Na hili halikukubalika, na halikubaliki serikalini Tanzania.

“Nne, hawakupenda kubadilishwa kwa mipango yao ya kushirikiana na mafisadi wachache kufuja fedha za walipa kodi waliopanga kufanya na watu wao ambao ndio wanaohaha kila mahala kuihujumu serikali iliyopo madarakani. Mipango haikuwa yenye heri kwa taifa. Kwanza, reli iliyokuwa ijengwe Tanzania ilikuwa kama ile ya Kenya ambayo ni ‘Second hand railway with old technology’, ambayo duniani haitumiki tena,” anasema mtoa habari wetu.

Mtaalamu huyo anatofautisha reli waliyotaka kujenga makandarasi hao na hii iliyojengwa sasa na Yapi Merkezi kwa kusema: “Kwanza, reli yetu ina uwezo mkubwa sana, kwa maana ya kubeba mzigo mkubwa ekseli 35. Reli nyingi zilizojengwa Afrika zina ekseli 25. Ni reli ambazo haziwezi kuchukua mizigo mizito, hasa kwa mtindo wa ‘double stack’.

“Ukitaka kubadilisha reli ya ekseli 25 kwenda ekseli 35, hii pekee itaongeza bajeti kati ya asilimia 15-17.5 ya jumla ya gharama yote ya ujenzi wa reli.

“Pili, reli inayojengwa Tanzania inatumia teknolojia ya kisasa ‘digital’ (European Train Control System Level) ikilinganishwa na analojia inayotembea kasi ya kilomita 80 kwa saa hapo kwa jirani zetu. Kubadilisha mfumo kutoka ‘analogy’ kwenda ‘digital’ unahitaji kutumia asilimia 7 hadi 7.5 ya jumla ya bajeti ya ujenzi wa reli ya kisasa. Na ujue kwamba unapozungumzia teknolojia kwenye reli, unazungumzia mawasiliano (signaling na telecommunications).

“Tatu, reli inayojengwa Tanzania inafanyiwa kitu kinachoitwa ‘continue welding’. Maungio ya reli yamechomelewa kwa teknolojia ya hali ya juu sana. Kubadilisha reli kuipeleka kwenye ‘continue welding’ bajeti inaongezeka kwa asilimia tano ya bajeti ya ujenzi wa reli.

“Nne, reli inayojengwa Tanzania ni ‘electrified line’ (ya umeme). Reli itatumia umeme badala ya dizeli, lakini pia itaweza kupitisha treni za dizeli ukilinganisha na walizotaka kujenga za injini za dizeli pekee.

“Mambo mawili muhimu; kwanza, treni ya umeme ni rahisi mara tatu kuliko treni ya dizeli. Ukitaka kubadilisha treni ya dizeli uweke miundombinu ya umeme inabidi utumie asilimia 25 ya gharama yote ya ujenzi wa reli.

“Tano, reli inayoijenga Tanzania ina kasi ya kilomita 160 kwa saa ikilinganishwa na hiyo waliyotaka kutujengea ya kilomita 80 kwa saa waliyojenga Kenya. Kubadilisha kasi ya kilomita 80 kwa saa kwenda kilomita 160 kwa saa, itahitaji kutumia bajeti isiyo chini ya asilimia 15 ya gharama zilizotumika kujenga reli yote,” anasema.

Anaongeza kuwa iwapo Kenya wangependa kujenga reli sawa na ya Tanzania katika hiyo gharama ya dola za Marekani milioni 6.2, sawa na Sh bilioni 14.26 kwa kilomita, ilibidi waongeze asilimia 70 ya bei hiyo na kuwa dola milioni 10.5, sawa na Sh bilioni 24.15 kwa kilomita au asilimia 70 ya gharama zote za kujenga reli.

Hii ina maana kuwa Tanzania imejenga reli hii kwa gharama ndogo ikilinganishwa na nchi zinazoizunguka. Kwa wastani hii reli ya umeme ya ‘Standard Gauge’, Tanzania inajenga kilomita moja kwa dola milioni 4.1, sawa na Sh bilioni 9.43.

Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa ujenzi wa kipande cha kwanza kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro; ambacho ni kilomita 300, kwa maana ya kilomita 205 za njia kuu na kilomita 95 za njia ya kupishania, kimejengwa kwa gharama ya dola za Marekani bilioni 1.22 ikijumuisha na VAT. Ukigawa kilomita 300 kwa kiasi hicho cha fedha, unapata wastani wa dola milioni 4.07 kwa kila kilomita, ikiwamo Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).

Kipande cha pili cha Morogoro mpaka Makutupora ya Singida chenye urefu wa kilomita 422, zikiwa kilomita 336 za njia kuu na kilomita 86 za njia za kupishania, kinajengwa kwa gharama ya dola bilioni 1.924. Ukigawanya kwa kilomita 422 ni sawa na dola milioni 4.6 kwa kilomita moja ikijumuisha VAT.

Ikumbukwe kipande hiki cha reli kimepita milimani kwa zaidi ya kilomita 120, ikiwamo na kuchoronga mahandaki (tunnels) zaidi ya kilomita 2.7.

Kipande cha tano cha Mwanza mpaka Isaka chenye urefu wa kilomita 341 kikiwa ni njia kuu kilomita 249 na kilomita 92 zikiwa njia za kupishania, kimejengwa kwa gharama ya dola bilioni 1.33. Ukigawa kwa kilomita 341 inakuwa dola bilioni 3.9 kwa kila kilomita moja, gharama hii ikijumuisha VAT.

“Sasa angalia kituko cha upembuzi yakinifu uliofanywa Novemba 2015 na kampuni inayoomba sasa kujenga vipande vilivyobaki kwa kutumia wanasiasa na wataalamu wachumia tumbo. Hawa walitaka wapewe mradi wote wa reli kuanzia Dar es Salaam hadi Mwanza na Kigoma. Kila kilomita moja walitaka kuijenga kwa dola milioni 6.2, sawa na Sh bilioni 14.26 kwa kilomita moja,” anasema mtoa taarifa na kuongeza:

“Na hiyo reli ambayo ingejengwa ni kama ya Kenya. Na kama ingejengwa tukataka ‘ku- upgrade’ ifanane na ya sasa ya kwetu, serikali ingetakiwa kutumia gharama zaidi ya asilimia 70. Maana yake nini? Ukiongeza asilimia 70 ya dola milioni 6.2 kwa kilomita moja, maana yake tungejenga kilomita moja kwa dola milioni 10.5 ili tupate reli ya ‘standard’ inayojengwa na Yapi Merkezi.

“Nini maana ya gharama hizo nilizozitaja? Maana yake ni kuwa gharama inategemea na eneo (terrain) ukipita kwenye milima na kuchoronga mahandaki, gharama ni tofauti na ujenzi wa sehemu nyingine. Hao hao waliotaka kutujengea reli ya kizamani kwa kilomita moja kwa dola milioni 6.2, leo ndio wanaopigiwa debe na wanataka kuwaamanisha Watanzania kuwa ni wazalendo. Walikwisha kusaini mkataba mwaka 2015 ambao Rais Magufuli alisema hautambui,” amesema.

JAMHURI limefahamishwa kuwa nchi nyingi Afrika zimeliwa katika ujenzi wa reli kwa kutumia gharama ya kati ya dola milioni 5.1, sawa na Sh bilioni 11.73 hadi dola milioni 8.0, sawa na Sh bilioni 18.4 kwa kilomita bila asilimia 18 ya VAT.

“Sasa kelele zimeanza wanataka tuwape hawa kazi hii. Sisi tunasema hapana. Tumsaidie Rais Samia [Suluhu Hassan] nchi yetu isiingizwe majaribuni. Utaratibu uliotumika kupata wazabuni kwa ‘Lot 2’ na ‘Lot 5’ ndiyo utumike kupata wa ‘Lot 3’ na ‘Lot 4’. Kinacholengwa kufanywa hakina masilahi kwa taifa letu,” amesema mtoa habari mwingine.

Duniani ujenzi kama uliofanywa na Tanzania kwa takwimu za mwaka 2015, wastani wa ujenzi wa kilomita moja ya reli ni dola milioni 3.5, sawa na Sh bilioni 8.05 bila kodi ya VAT.

Kwa mabadiliko yaliyotokea ya bei za vifaa ikijumuisha na kupanda kwa bei ya chuma, bei ya mafuta, bei ya saruji na vifaa vingine inakadiriwa sasa kuwa wastani wa kujenga reli ya umeme kilomita moja inagharimu dola milioni 4.0, sawa na Sh bilioni 9.2.

Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa kelele zinazoendelea zinatokana na kuzipigia debe kampuni tatu za Kichina ambazo zimewasilisha serikalini maombi ya kujenga kipande cha 3 na cha 4 kwa wastani wa bei ya dola milioni 5.5, sawa na Sh bilioni 12.65 kwa kilomita. Gharama hii iko juu kwa zaidi ya dola milioni 1.5, sawa na Sh bilioni 3.45 ikilinganishwa na gharama za sasa za ujenzi zinazotumika.

“Kaka hapa kinachofanyika ni watu wanataka wagawane hizo Sh bilioni 3.45. Tukiwakubalia nchi itapoteza zaidi ya Sh trilioni 2. Hizi fedha zitaingia mifukoni mwa watu na kwa kweli haikubaliki. Tujenge reli kwa utaratibu wa zamani ambao tumeanza nao. Huu mchakato wa zabuni ukianza sasa, kwanza, hautakamilika, lakini hata ukikamilika ni miaka mitatu ijayo. Tutapoteza mwelekeo. Tuendelee kama tulivyokuwa tumalize hii reli, wanaopigania matumbo yao tuachane nao,” amesema mtoa habari mwingine.

JAMHURI limezungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania, Masanja Kadogosa, aliyekiri kuyasikia hayo maelezo wanayotaka mchakato uanzishwe wa kutangaza vipande vya 3 na 4 vya reli naye akasema: “Sisi tupo kumsaidia Mheshimiwa Rais. Tunaamini kwa masilahi mapana ya nchi hii, reli hii ujenzi wake ulianza na unaendelea vizuri.

“Kuna utaratibu wa kisheria wa ‘single sourcing’ ikiwa anayetoa zabuni anazifahamu gharama halisi za mradi. Naamini utaratibu huu ni mzuri na utatupunguzia kelele. Rejea yaliyotokea mwaka 2016. Kelele zilikuwa nyingi kuliko sasa na tuliendelea kwa masilahi mapana ya taifa letu. Matunda bora kabisa ya ujenzi yanaonekana.”

Kadogosa anasema anasubiri mchakato wa kumpata mzabuni unaondelea serikalini ukamilike ‘Kazi Iendelee’.

JAMHURI linafahamu kuwa kuna kundi la watu wanaoamini kuwa baada ya kufariki dunia Rais John Magufuli, kwa sasa wanaweza kupenyeza masilahi yao binafsi katika miradi ya kitaifa na kujipatia fedha nyingi. Gazeti hili litaendelea kufuatilia sakata la mradi huu kuhakikisha nchi haiingizwi katika gharama zisizostahili na wajanja wachache.