George Weah(kushoto) na Makamu wa Rais Joseph Boakai (kulia)

Mahakama kuu ya Liberia imesema kuwa ushahidi wa vitendo visivyokubalika katika uchaguzi wa Rais duru ya kwanza mwezi Oktoba hautoshi kuufanya uchaguzi kurudiwa.

Hii inamaanisha kuwa mzunguko wa mwisho wa uchaguzi kati ya wagombea wawili waliokuwa wakiongoza yaani George Weah na Makamu wa Rais Joseph Boakai unaruhusiwa kuendelea.

Sasa inasubiriwa tume ya uchaguzi kuweka na kuitangaza siku ya kupiga kura.

Mwakilishi wa chama cha Liberty Charles Brumskine ambaye alikuwa katika nafasi ya tatu katika mzunguko wa kwanza alikuwa ameyapinga matokeo akitaka uchaguzi urudiwe.

Mzunguko wa pili wa kumchagua mrithi wa rais Ellen Johnson Sirleaf awali ulikuwa umepangwa kufanyika mwezi uliopita, Novemba.

Liberia ambayo ni nchi iliyoundwa na watumwa walioachiwa huru huko Marekani katika karne ya 19, haijawahi kuwa na makabidhiano ya madaraka kawa miaka 73.

Bi Sirleaf alitwaa urais mwaka 2006 baada ya mwaka 2003 waasi kumwondoa kwa lazima kiongozi wa wakati huo Charles Taylor, tukio hilo likikomesha vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka mingi.

Hivi sasa Taylor anahudumia kifungo cha miaka 50 jela nchini Uingereza kutokana na makosa yanayohusiana na majirani zao Sierra Leone.

 

Please follow and like us:
Pin Share