Mwandishi wetu, Arusha

Taasisi ya Wanahabari ya kusaidia Jamii za pembezoni (MAIPAC) imeahidi kutoa msaada wa kompyuta kwa shule ya msingi ya Arusha Alliance ambayo inamilikiwa na Walimu ili kuwezesha wanafunzi kusoma masomo ya TEHAMA.

Mkurugenzi Mtendaji wa MAIPAC,Mussa Juma alitoa ahadi hiyo katika mahafali ya darasa la Saba ya 14 ya shule hiyo ambapo ni moja kati ya shule 10 bora katika Jiji na Arusha zinazoongoza Kila mwaka mwaka kwa kufaulisha.

Juma ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mahafali hiyo alisema kwa shule hiyo ni mfano wa kuigwa nchini kwani imeanzishwa na walimu baada ya kuamua kuungana na kuchangishana fedha .

“MAIPAC kama taasisi ya kijamii tumeona kuunga mkono jitihada za walimu wa shule hii na kwa kuwa hapa pia mnatpa elimu kwa watoto kutoka Jamii za pembezoni tutasaidia kompyuta ili kuendeleza elimu ya TEHAMA”alisema

Alisema kutokana na mabadiliko makubwa ya Sayansi na Technolojia Duniani elimu ya TEHAMA ni muhimu kwa wanafunzi kuanzia shule za msingi.

Juma ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha wafanyakazi katika vyombo vya habari Tanzania (JOWUTA) , alisema aliwataka wahitimu kuendelea kuwa na maadili ambayo ndio yatasaidia kufanya vizuri katika maisha Yao.

“Mmekuwa hapa miaka Saba walimu wamewafundisha maadili mazuri katika.jamii basi nendeni mkawe watoto wema msijiimgize katika matumizi ya dawa za kulevya,kucheza kamari na katika vitendo vya Ukatili wa kijinsia”alisema

“Arusha ni moja ya mikoa ambayo inaongoza kwa matukio ya Ukatili wa watoto Sasa mjuwe mnapoenda sio Salama sana jilindeni na matukio hayo msijiunge na makundi mabaya”alisema.

Juma pia aliwataka walimu nchini kuiga mfano wa walimu wa alliance kuungana na kuanzisha shule yao kwani Kuna wadau wengi wa kuwaunga mkono ikiwepo Serikali na Taasisi za fedha.

“Walimu nchini ni muhimu kujua kazi ya Ualimu ni fursa kubwa ya kuboresha maisha Yao na sio kazi ya kada za chini na ambayo haiwezi kuwafanya walimu kuwa matajiri wakubwa”alisema

Kaimu mwalimu Mkuu wa shule hiyo , Elimboto Mdiu alisema shule hiyo iliazishwa mwaka 2007 ikiwa na wanafunzi 18 tu lakini sasa Ina wanafunzi 800.

Mdiu alisema katika mahafali hiyo wanafunzi 114 wamemaliza darasa la Saba ambapo wasichana ni 56 na wavulana 48 na wanaimani wote watafaulu vizuri.

Awali Diwani wa Kata ya Olasiti,Alex Martin alisema Kata yake inajivunia shule hiyo kwani imekuwa ikiongoza kufanya vizuri lakini pia kutoa elimu na maadili mazuri kwa wanafunzi.

By Jamhuri