Na Mwandishi Wetu Jamhuri Media, Dar es salaam

Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imeeleza mafanikio makubwa iliyoyapata kwa kipindi cha miaka 20 tangu kuazishwa kwake.

Tangu ianzishwa 2003 kama taasisi hadi 2023 TMDA imepiga hatua mbalimbali za mafanikio na kuifanya kuwa kinara barani Afrika katika umahiri na utoaji huduma na kuwa kituo cha mafunzo kwa nchi zingine.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Adam Fimbo katika kikao kazi pamoja na waandishi wa habari kilichofanyika jijini Dar es salaam Septemba 22, 2023 ameipongeza serikali, wadau mbalimbali pamoja na waandishi wa habari kwa ushirikiano ulifoanya iweze kufika ilipo.

Fimbo ameeleza moja kati ya mafanikio makubwa waliyoyapata ni pamoja na kufikia hatua ya tatu ya Shirika la Afya Dunia (WHO) katika umahiri wa mifumo ya udhibiti (Maturity level 3) na kuwa nchi ya kwanza Afrika kufikia hatua hiyo tangu mwaka 2019 ambapo nchi kama Afrika Kusini, Ghana, pamoja na Nigeria zilifuatia kuanzia 2021.

“Tuna mengi ya kujivunia, TMDA sasa hivi ni taasisi ambayo imefanyiwa uhakiki kwanza na shirika la Afya Duniani, taasisi ambayo inaongoza barani Afrika kwenye maswala ya mifumo ya udhibiti wa dawa” amesema Fimbo

Amesema, mifumo ya usajili, ukaguzi wa viwanda na masoko, ufuatiliaji wa usalama wa dawa kwenye soko na uchunguzi wa kimaabara yote ilihakikiwa na WHO na hivyo kuvutia nchi mbalimbali kuja kujifunza na kuifanya Tanzania kuwa kitivo cha umahiri katika udhibiti wa Chanjo Afrika.

“Sasa hivi tunaongoza na tumekuwa tukitoa mafunzo kwa wenzetu wa SADC wanakuja hapa kujifunza taratibu za udhibiti wa dawa zikoje tunafanyaje kazi na tumekuwa tukitoa mafunzo hayo sana” amesema.

TMDA, kazi yake kubwa ikiwa ni kudhibiti ubora usalama na ufanisi wa bidhaa za dawa vifaa tiba, vitendanishi pamoja na bidhaa za tumbaku imefanikiwa pia katika utoaji wa taarifa za madhara ya dawa pamoja na ufuatiliaji wa bidhaa kwenye soko kupitia mifumo ya kielektroniki ambayo imesaidia kupungiza mda na gharama za wateja katika kupata huduma.

Katika upande wa huduma Mamlaka hiyo imeweza kufungua ofisi katika kanda nane nchini ikiwa ni pamoja na kujenga majengo katika mikoa ya Mwanza, Dodoma ambapo ni Makao makuu, Mbeya pamoja na Dar Es salaam ili iweze kuwa rahisi kutoa huduma katika kanda hizo.

Kwa kipindi cha miongo miwili Mamlaka hiyo imekuwa ikipata hati safi ambazo hazina mashaka yoyote kutoka kwa Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG)

Pia imeweza kutoa gawio kwa serikali ambapo kutoka mwaka 2016/ 2017 hadi mwaka huu wa fedha imeweza kutoa jumla ya Sh. Bilioni 52.5 katika mfuko wa serikali.

Vilevile TMDA imeeleza kuwa, imejitahidi katika kusimamia sera ya viwanda nchini ambapo jumla ya viwanda 17 vimejengwa tangu mwaka 1966, viwanda 11 vikiwa vya kuzalisha dawa za binaadamu na vingine 06 vya dawa za mifugo huku ikitarajia ongezeko la viwanda vingine 10 ambavyo viko katika hatua mbalimbali za ujenzi na hivyo kufikia jumla ya viwanda 27 vitakavyokuwepo nchini

By Jamhuri