MAISHA NI MTIHANI (22)

Hatuoni ingawa tunatazama

Kuona ni mtihani. Si kila jicho lililofunguka linaona. Na si kila jicho lililofumbwa limelala. Kila mtu anatazama lakini si kila mtu anaona. Kuona ni mtihani. Je, unapotazama unaona? “Hatuoni vitu kama vilivyo, tunaviona kama tulivyo.” (Anais Nin).

Kwa msingi huo, kuona ni mtihani. Mfinyanzi atauona udongo kama kitu cha kumsaidia kutengeneza vyungu, kutegemea fani yake. Mkulima atauona udongo kupitia miwani ya kilimo kama ni mzuri wa kuwezesha mbegu kustawi. Mjenzi atafafanua udongo kupitia miwani ya ujenzi. Kwa msingi huu kuona ni mtihani. Helen Keller, ambaye alikuwa kipofu aliulizwa: “Balaa kubwa sana ni lipi?” Alijibu: “Kuwa na macho na usione.”

Methali ya Kiswahili inasema ukweli mtupu: “Penye miti hakuna wajenzi.” Miti ipo lakini baadhi ya watu hawaoni meza, viti au vitanda kutoka kwenye miti. Wakati mwingi tunatazama lakini hatuoni. Watu wengi walitazama ndege anaruka angani lakini ni wachache waliofikiria kutengeneza ndege, na kuiona ikipaa angani. Watu wengi walimtazama samaki akiogelea majini, ni wachache waliofikiria kutengeneza meli wakaiona iking’oa nanga. Ona uwezekano, lisilowezekana linawezekana.

Kutokana na neno kuona, tunapata neno maono. Maono ni ufundi wa kuona ambacho hakionekani. Unaweza kuiona kesho. Unaweza kuona nyumba ambayo hujajenga. Unaweza kuona gari ambalo hujanunua. Unaweza kuiona kampuni ambayo hujaimiliki. Kuwa na maono ni kuona mbali.

“Maono yanahitaji kuona ya nyuma, utambuzi (umaizi) na kuona mbele,” alisema William H. Taylor. Ingawa tunajenga kwa yaliyopita, usitazame nyuma sana, makubwa yapo mbele. Kioo cha pembeni mwa dereva kinamsaidia kuona ya nyuma lakini ni kidogo. Kioo cha mbele cha kumsaidia kuona ya mbele ni kikubwa. Ya mbele ni makubwa, tutazame mbali. Maono yanahitaji umaizi au utambuzi. Utambuzi ni kuwa na jicho la tatu. Ufundi wa kuona unazingatia yafuatayo:

Simama kwenye mabega ya watu wakubwa. Maono yanahitaji kuona mbali. Wakati mwingine ili kuona mbali unahitaji kusimama kwenye mabega ya watu wakubwa. Kwa mtazamo huo Sir Isaac Newton alisema: “Kama nimeona mbali zaidi yako…ni kwa kusimama kwenye mabega ya watu wakubwa.” Baadhi ya teknolojia za kisasa zimejengwa kwenye uvumbuzi wa watu wengine wa zamani.

Unaweza kujenga juu ya kilichopo. Unaweza kuchanganya vitu viwili ukapata kitu kimoja kipya. Kuna aliyesema: “Kila siku ukikutana na matajiri wanne, wewe ni tajiri wa tano ajaye. Na kila siku ukikutana na maskini wanne, wewe ni maskini wa tano ajaye.” Kutana na watu wanaokuzidi katika fani yako kila siku uweze kusimama kwenye mabega yao na kuona mbali zaidi.

Waza lile unalotaka kuliona. Unaona lile unalochagua kuliona. Mawazo yako yanafinyanga maono yako. Jione unavyotaka kuwa siku za mbeleni. “Kama hauna maono ya wewe unavyojiona wakati ujao, hivyo hauna jambo la kuishi kwa ajili yake,” alisema Les Brown. Jiwazie mazuri. Jizungumzie mazuri. Piga picha ya maisha yako mazuri siku za mbeleni.

Tengeneza kaulimbiu, sentensi au usemi wa maono yako. “Kaulimbiu ya maono yako inakufanya kutazamia yajayo ukiwa na matarajio chanya kwa ajili yako. Inakusaidia kubaki kwenye msitari na itakusaidia kufanya uamuzi wa shughuli za siku zijazo,” alisema Catherine Pulsifer.

Chukua hatua. Kuna watu wanawaza kuandika kitabu na kuna watu wanaandika kitabu. Haitoshi kuwaza, chukua hatua. Haitoshi kuota ndoto, chukua hatua. “Maono bila tendo ni ndoto. Tendo bila maono ni kupitisha muda. Tendo pamoja na maono ni kufanya tofauti chanya,” alisema Joel Barker. Matendo yana kauli kuliko ndoto.