Ndugu Rais, ndivyo alivyo Mwenyezi Mungu; huwatuma watu wake wema walio kati ya watu wake kuwafikishia ujumbe watu wake walio kati yao. Wenye masikio ya kusikia husikia, bali wenye viburi Bwana huwaadhibu kwa mwisho wao wa aibu.

Nukuu katika kitabu cha Mwalimu Mkuu wa Watu inasomeka kuwa Bwana Mageuzi alisema madhara yangekuwa makubwa zaidi kama si kwa ubunifu na busara iliyoonyeshwa na mama mmoja aliyemtaja kwa jina moja tu, Nakamanga! Aliuambia ule umati kuwa ni desturi ya maisha kuwaficha watu wake bora kabisa mpaka jambo kubwa litokee!

Jaji Msataafu Barnabas Samatta katokea wapi? Amekuja kuwaambia Watanzania kuwa kwa ibara ya 46(3) ya Katiba yetu, Rais mstaafu anayo haki ya kushitakiwa kama raia wengine kwa makosa aliyofanya akiwa rais, lakini si makosa aliyofanya kama rais! Akinukuu; alisema jambo la huzuni kubwa sana si ukandamizaji na ukatili wanaofanyiwa watu wabaya, bali ukimya juu ya hayo wanapofanyiwa watu wema. Mwenyezi Mungu aliniepusha na mambo ya siasa tangu ningali kijana ndiyo maana sina ushabiki wa chama chochote cha siasa.  Jumapili moja nikaamua kwenda Segerea kumwona Freeman Mbowe aliyekuwa mahabusu. Ni zaidi ya miaka 20 sijawahi kutembelea magereza yoyote.

Nikiwa mstarini askari akaniambia “tunaruhusu watu watatu tu kumwona mtu mmoja. Nikikuruhusu utakuwa wa 20”. Nikamuomba kuwa tulichukulie hili kama changamoto ili tujitahidi na sisi kuishi kwa mfano wake. Tuishi kwa namna ambayo tutakapofariki dunia hata mtu anayefanya biashara ya kutayarisha mazishi atakuwa na masikitiko juu yetu jinsi tulivyoishi vema na watu. Akaniruhusu. Kule ndani nilipangiwa sehemu ya kusubiri. Nilimwona amesimama upande wa pili wa nondo za gereza. Aliponiona akaweka mkono wake wa kushoto kifuani pake akaniinamia. Na mimi nikaijibu salamu yake kwa staili ile ile. Tulipopata nafasi ya kuongea tuliongea, nikaondoka.

Kabla sijaufikia mkweche wangu mwili ulinizizima. Nikajisemea kifuani mwangu, “Yawezekana Nelson Mandela hakuwa mtu muhimu sana kabla hajafungwa. Makaburu wakidhani wanamkomoa wakamfunga gerezani, kumbe ndiyo walikuwa wanamboresha zaidi!” Dunia sasa inajua kuwa Freeman alifungwa gerezani bila kuwa na hatia.

Hayati Shaaban Robert aliwahi kusema kuwa, kweli itashinda kesho kama leo haitoshi. Kama isingetolewa ripoti ya uongo kuhusu Richmond, hali duni ya maisha waliyonayo Watanzania isingefikia kiwango hiki.

Bila aibu tena hadharani Watanzania waliambiwa kuwa ungesemwa ukweli wote serikali ingeporomoka yote. Baada ya waziri mkuu kujiuzulu serikali iliporomoka yote akabaki rais peke yake. Kweli serikali ni rais. Kabla akitoa mwelekeo wa serikali ya awamu ya nne, Waziri Mkuu wa kwanza wa serikali ya awamu ya nne aliwaahidi Watanzania, “Tutaanza na ujenzi wa shule za sekondari kwa kila kata nchi nzima.

Tukimaliza; tutajenga zahanati kwa kila kata nchi nzima.’’

Wangefanikisha hayo adui umaskini angeondoka mwenyewe. Walijikita katika misingi ile ile ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Kwa kuyapuuza haya na wala siyo kwa ujenzi wa TAZARA, KIA na makubwa mengine; Watanzania wataendelea kumlilia Nyerere. Wanalilia utu wao!

Wanawema tujiulize katika umoja wetu, kwanini Watanzania bado wanamlilia Nyerere mpaka leo? Rais Julius Kambarage Nyerere alijenga treni ya kisasa zaidi wakati huo, TAZARA – Afrika nzima hakukuwa na mfano wake. Lakini kwanini hakukuwa na kelele mabarabarani za kudai kuwa Rais Nyerere anaifanyia nchi mambo makubwa? Tunajenga treni ya kisasa japo kwa mafungu, lakini ni jambo kubwa na ni jambo la maendeleo. Iweje leo kuwe na kelele kila mtaa kuwa tunaifanyia nchi makubwa kama vile tunaiteremshia nchi mbalamwezi? Hata kwa ndugu zetu hapa Kenya tu, hiyo ni treni ya kawaida kabisa.

Rais Nyerere wakati wake alijenga kiwanja kikubwa, cha kisasa zaidi na cha kimataifa cha Kilimanjaro (KIA). Na kwa upeo wa kuona mbali katika kiwanja hicho alijenga na banda la ndege Waingereza wanaita, ‘hangar’.

Alijua kuwa kama hata baiskeli tu inahitaji servisi sembuse ndege! Pia kelele hazikusikika.

Watanzania wanazidi kumlilia Rais Julius Kambarage Nyerere hadi leo kama vile hakuna marais wengine waliotokeza baada yake ni kwa namna alivyothamini utu wao! Aliwapatia elimu bora mpaka chuo kikuu kwa malipo ya kodi ya wazazi wao. Alimtibia kila Mtanzania bila malipo zaidi ya kodi yake. Leo Watanzania wanatangaziwa tu kuwa kuna mbailioni yametengwa, lakini dawa katika hospitali hazipo, na kama zipo, basi hazitoshi.

Ndugu Rais, Jaji Mkuu Mstaafu Samatta kama mtu bora aliyefichwa na maisha kuhusu rushwa anasema, “Mimi binafsi sijasikia yeyote kati ya viongozi hao akipoteza kazi yake kwa kukutwa na mali zaidi ya uwezo wake kifedha au vinginevyo! Ndiyo kusema hata utaratibu unaowahitaji viongozi waandamizi wa umma kutoa ripoti kila mwaka juu ya mali walizonazo na madeni yao kwa Kamishna wa Maadili haujazaa matokeo yaliyotarajiwa na umma.’’

Akaongeza kuwa kuna haja ya utaratibu huu kumulikwa ili uweze kusaidia katika mapambano dhidi ya rushwa.’ Isionekane namuwekea Jaji wa watu maneno mdomoni, lakini kinachosemwa hapa ni kwamba kama kuna vita dhidi ya rushwa, vita hiyo haionekani kwa macho ya nyama!

Kuna ulemavu mkubwa katika nchi hii watu kushindwa kubadili misimamo yao hata pale kweli inapojidhihirisha. Likitamkwa neno wanaulizana limetamkwa na mtu wa chama gani! Marehemu Boutros Boutros Ghali akijibu swali aliloulizwa ni kwa nini alibadili msimamo wake wa kutogombea awamu ya pili ya wadhifa wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), alijibu, “Ni wapumbavu pekee ndio ambao hawabadili mtazamo wao.’’

Leo, Jaji Mkuu Mstaafu Samatta ameyatamka maneno hayo hayo,

lakini kwa mtazamo wake. Huyu ni kati ya viongozi wetu wakuu wastaafu wachache ambao hawanuki itikadi yoyote ya kisiasa, kidini wala kikabila! Hawa ni watu wa haki. Maswali aliyouliza yanathibitisha kuwa mafanikio makubwa yanayosemwa hayaonekani! Hatafutwi mshindi hapa.

Bali maneno ya Jaji Mkuu Mstaafu Samatta yatusaidie vipi sisi wote kurudi katika mstari?

Please follow and like us:
Pin Share