Mgeni ni mtu aliyetembelea eneo fulani kwa mara ya kwanza. Ni mtu anayepewa dhamana ya kuwa mtu muhimu, na aghalabu hupewa jukumu la kutekeleza shughuli rasmi inayofanyika. Mgeni ni mtu asiye na uelewa wa kutosha au ueledi katika fani fulani. Tunaweza kusema ni mwanagenzi.

Mimi na wewe tunamfahamu mgeni anavyopewa heshima, thamani na huba wakati wa mapokezi na mwenyeji wake. Watu hawa huchukuana kama chanda na pete katika kipindi hicho cha ugeni. Riwaya, historia na taarifa mbalimbali hububujika vinywani mwao, mithili ya maji ya chemchemi. Wakati wote ni furaha, vicheko na tabasamu.

Mara kwa mara tumefikwa, tumeona au kusikia shamrashamra ya mapokezi ya mgeni nyumbani, ofisini, shughulini na sehemu nyingine. Yote haya yanafanyika kwa heshima na huba ya mgeni. Vyakula na vinywaji, malazi na matembezi ya hapa na pale kijijini au mitaani hufanyika kukamilisha ratiba ya mgeni kwa upendo na amani.

Mgeni huleta ujumbe maalumu na pengine hubeba zawadi kwa mwenyeji wake. Wawili hawa hufanya mazungumzo kama vile ya utabibu, elimu na imani ya roho. Wakati mwingine hutafuta njia au maafikiano ya kujenga ushirikiano, ujirani mwema na urafiki katika serikali, siasa, uchumi na kadhalika. Tunasema: “Mgeni njoo mwenyeji apone.”

Lakini mgeni hupunguza thamani yake anapofika kwa mwenyeji wake mikono mitupu. Mwenyeji asiye na maarifa na utu hufanya utesi kwa mgeni na kunena vichochoroni: “Mkono mtupu haulambwi.” Uhusiano wa wawili hawa huwa si mzuri, na wakati fulani mgeni hunyimwa chakula, mgeni naye huzua kejeli, lawama na kutoa siri za ndani.

Nakumbuka enzi za utotoni nilipomtembelea bibi yangu pale kijijini Kilomo na babu yangu kule kijijini Kitopeni, wilayani Bagamoyo, Mkoa wa Pwani, wakazi wa maeneo hayo na mengine, walikuwa na utenzi wao usemao: “Mgeni siku ya kwanza, mpe mchele na panza, mtilie kifuuni, mkaribishe mgeni.

“Mgeni siku ya pili, mpe wali na samli, na mali ikizidia, mzidishie mgeni. Mgeni siku ya tatu, na ndani hamna kitu, mna vibaba vitatu, pika mle na mgeni. Mgeni siku ya nne, mpe jembe akalime, akirudi muagane, aende zake mgeni.  Mgeni siku ya tano, mwembamba kama sindano, ndani hamwishi nong’ono, atetwa yeye mgeni.”

Utenzi huo unaendelea kusema: “Mgeni siku ya sita, mkila na kajificha, na hapana afichwaye, afichwa yeye mgeni. Mgeni siku ya saba, si mgeni ana baa, hata moto mapatano, katia yeye mgeni. Mgeni siku ya nane, mwite ndani muagane, akitoka hapo nje, kwaheri nenda mgeni.

“Mgeni siku ya kenda, ewe nenda mwana kwenda, usirudiye njiani, usirudi we mgeni.” Wakazi hao wa Bagamoyo wanamalizia utenzi wao wakisema: “Mgeni siku ya kumi, kwa mateke na magumi, hapana afukuzwaye, afukuzwaye mgeni.”

Utenzi huu ukiusoma utabaini, unatoa mafunzo kwa mgeni anapokaribishwa, awe na hadhari na makazi yake ya muda. Kadhalika mwenyeji anapompokea mgeni awe makini na anapofanya hisani na mazungumzo awe mwangalifu ili atunze heshima na utu wake mbele ya jamii, kwa sababu uungwana ni dhima kwa watu.

Mgeni kukirimiwa ni tendo la kiungwana. Simulizi na mazungumzo matamu matamu yaonyeshe nia ya kujenga umoja, ujirani na urafiki katika shughuli zao za kila siku. Utii wa sheria, kanuni na haki za msingi za binadamu hazina budi nazo kufuatwa na kuzingatiwa. Wageni waovu hufurahi kutimiza nia zao na kuwaacha wenyeji wao solemba.

Kumbuka mgeni siku ya saba hutia moto mapaani. Hii ina maana gani? Si kila mgeni ni mwema, wengine ni wabaya wana yao moyoni na watakutia shimoni. Mwenyeji na mgeni wanaposhindwana kupata mwafaka, waachane kwa heri, si vema kukitana magumi na mateke. Kwa mgeni mbaya ni furaha, kwa mwenyeji muungwana ni fedheha kubwa.

Wenyeji ingawa mnapenda kukirimu wageni kwa kuwapa mchele na panza, wali wa samli na vingine vya siri, mkumbuke kubakisha maneno. Maneno yenu ya leo, kesho yatakuwa viboko vya kuwacharaza wenyewe. Elewa kuku mgeni ana kamba mguuni, kwa nini?

Nawe mgeni unapokirimiwa nyama ya kuku na kupewa kidari na kiga kwa mnofu na laini, jiulize huyu kuku ana hadhi gani? Mbona mwenyeji amekunyima kichwa, nani atakula? Namaliza fasihi kwa kusema kipya kinyemi. Tafakari.

Please follow and like us:
Pin Share