Nianze na salamu kama mtu muungwana, maana itakuwa si busara kukurupuka na mawazo yangu kichwani bila kuwajulia hali.

Najua kuwa si kila mtu yuko sawa kichwani, hasa katika kipindi hiki cha mpito wa mabadiliko ya mambo mengi, hasa yale yahusuyo mifuko yenu, natoa pole.

Salamu zangu zingine, tena za kipekee kabisa nazituma kwa wale ambao hawajatetereka katika kipindi hiki cha kukaza kwa vyuma, hawa nawapa kongole kwa sababu nina uhakika kabisa walikuwa katika kundi ambalo lilikuwa likiishi kwa kudra za Mwenyezi Mungu huko nyuma.

Hawa ni wale ambao walikuwa washamba kuhusu kitu kinachoitwa ‘misheni town’, ni kundi ambalo lilikuwa likiwaona watu wakiishi na wao walikuwa wasindikizaji, mambo huwa yanageuka na mstari wa jeshi huwezi kujua uko mbele au nyuma, nadhani sasa mko mbele na maisha yanasonga.

Maisha yanakwenda kasi sana sasa hivi na mabadiliko ya binadamu katika mfumo wa maisha ni wa haraka sana, japo wapo ambao wanaumia sana, wapo wanaoumia kwa sababu ya wengine kuteremka kwa kasi kutoka juu na wapo wanaoumia kwa sababu sasa wameanza kubeba mizigo isiyo yao na wapo wanaoumia kwa kuonewa na wenye dhamana ya kuwanyoosha warudi kwenye mstari ambao haukuwa wao.

Kiufupi ule msemo wa samaki mmoja akioza, wote wameoza, naona umedhihirika katika hili.

Lakini pamoja na kubadilisha mfumo wa maisha yetu kwa maana ya kuheshimu matumizi ya fedha kwa kuifanya fedha yetu kuwa na thamani, bado kuna mambo yanaongezeka katika kubadili taswira ya maisha yetu.

Kuna vitu vinashuka bei na kuna vitu vinapanda bei, kuna mambo yamerahisishwa na kuna mambo yamekuwa magumu zaidi.

Hakuna asiyependa kuwa katika mfumo huu, kwa sababu ule mfumo wa mpito wa zamani ulitugharimu sana baadhi yetu katika kuyaendesha maisha yetu. Pamoja na pongezi hizi, bado kuna mengi yanayokera ambayo nadhani yanatakiwa yafanyiwe kazi kwa uangalifu wa hali ya juu ili kuzuia watu wengine wasiendelee kuumia sana kwa kisingizio cha kuwanyoosha wachache.

Suala la rushwa naamini ni la mtu binafsi na mmojammoja, tuna taasisi ambayo imekabidhiwa dhamana ya kupambana na suala la rushwa, taasisi hii si chama cha siasa bali ni chombo cha kisheria cha kupambana na jambo lolote linalofikiriwa kwamba lina uhusiano na rushwa. Naamini wanajua kwamba rushwa si fedha peke yake, hata upendeleo mahali pa kazi na ngono ni sehemu ya rushwa.

Rushwa ya upendeleo kazini kwa sasa hivi imetamalaki, hasa kama jambo lenyewe linahusu mapato na marupurupu, wapo wafanyakazi ambao kwao kupanda vyeo ni jambo la kawaida, kuandikiwa ripoti nzuri ya kiutendaji haina shaka, lakini wapo ambao wanaonekana wana damu ya kunguni, hawana haki ya kupewa marupurupu au posho yoyote, wala kupandishwa vyeo.

Kibaya zaidi ni kushushwa vyeo na kuandikiwa ripoti mbaya. Tunao viongozi wa namna hiyo wengi sana serikalini na katika taasisi za umma.

Urasimu ni aina nyingine ya rushwa iliyojificha, ambayo nadhani tunatakiwa kuitafakari kwa kina, wapo watu ambao kwa namna ya utendaji kazi wao hawana jambo la kufanya isipokuwa wanatafuta uhalali wa kuwepo kwa kutengeneza daraja la urasimu, na hili tumeliona mara nyingi viongozi wa kitaifa wanapotaka kujua namna ya utendaji kazi wetu unavyokuwa na mipaka isiyo na sababu, utendaji unaoleta ucheleweshaji usio wa lazima kabisa, tuendako ni lazima tujue kuwa muda ni fedha, hivyo nao tuugeuze kama ni sehemu ya rushwa.

Katika hili la urasimu, suala la kutoa uamuzi sahihi, kwa wakati sahihi limekuwa ni tatizo kubwa, hakuna maelewano ya moja kwa moja, pia kuna siri nyingi baina ya idara moja na idara nyingine, hiyo tunalazimisha kurudi nyuma miaka mingi badala ya kwenda mbele kulingana na wakati tulio nao.

Nchi yetu pamoja na kupambana na suala la sheria, lakini kuna tabia ya kutofuata sheria, na hili nadhani linatokana na kushindwa kudhibiti wanaofanya makosa, bado tumejikita katika makosa ya kawaida, ya kizamani na kuacha sheria mpya zikikiukwa mbele ya macho yetu. Katika hili nitaandika waraka maalumu na kutoa ushauri tufanye nini ili uwe mwisho na sehemu ya kuinua uchumi wetu.

Wiki kesho nitawaandikia barua nyingine nikijaribu kujiuliza baadhi ya maswali.

Wasalamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.

Please follow and like us:
Pin Share