Hofu ya Chadema sheria mpya ya vyama vya siasa

Katika taarifa kwa umma, Machi 22, 2019, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimefanya uchambuzi wa sheria mpya ya vyama vya siasa iliyotiwa saini na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivi karibuni kama ifuatavyo:

Tumeiona Sheria mpya ya Vyama vya Siasa ambayo imesainiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli, Februari 13, 2019 na kuchapwa kwenye Gazeti la Serikali la Februari 22, 2019.

Sheria hii pamoja na kupigiwa kelele na wadau mbalimbali wa nje na ndani ya nchi kama vyama vya siasa, asasi mbalimbali, taasisi na mashirika ya dini, vyama vya wanataaluma mbalimbali na wapenda demokrasia kuwa ni sheria mbaya na haifai, bado wabunge wa CCM waliupitisha muswada huo na sasa rais ameusaini kuwa sheria.

Sheria hii ni mbaya kutokana na vifungu vyake ama kukiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na misingi ya utawala bora pamoja na mikataba mbalimbali ya kimataifa ambayo Tanzania tumetia saini.

Mathalani vifungu vifuatavyo:                 

1. Kifungu cha 3 (b) kimempa Msajili wa Vyama vya Siasa jukumu la kusimamia chaguzi za ndani ya vyama ikiwa ni pamoja na teuzi za wagombea wa nafasi mbalimbali. Hii inampa Msajili mamlaka ya kuingilia vyama na kuviamulia ni nani awe kiongozi wa chama husika au mgombea wa nafasi ya kiserikali, kama mgombea urais na ubunge,  hii ni kinyume cha Katiba ya nchi, ambayo imetoa fursa na haki ya kujumuika kwa wananchi wake.

2. Kifungu cha 3 (g) kinamfanya Msajili wa Vyama vya Siasa kuwa mshauri wa serikali kuhusu vyama vya siasa, huyu anakwenda kuwa mshauri wa serikali badala ya vyama, hivyo kumuondolea sifa muhimu ya kuwa mlezi wa vyama na badala yake anakwenda kuwa msimamizi wa vyama.

3. Kifungu cha 5A (i) kinampa Msajili wa Vyama vya Siasa mamlaka ya kuamua aina ya mafunzo ambayo chama kinatakiwa kupata kutoka kwa mashirika na taasisi mbalimbali za nje. Huku ni kuvinyima haki vyama kupata utaalamu na mbinu za kisasa za kufanya siasa, kwani Msajili wa Vyama vya Siasa anaweza kuzuia mafunzo kwa hisia tu kuwa kama yakitolewa yanaweza kukifanya chama husika kuwa na mbinu za kukiondoa chama tawala madarakani.

Aidha, vyama vya siasa viko kwenye muungano wa kiitikadi za kidunia, hivyo kuvifanya kunufaika na mafunzo mbalimbali yanayotolewa kutokana na mirengo hiyo, kumpa Msajili wa Vyama vya Siasa uamuzi wa mwisho kuhusu mafunzo ya vyama ni kuendelea kuzuia haki za vyama kujumuika na kushirikiana.

4. Kifungu cha 5B (i) kinampa Msajili wa Vyama vya Siasa mamlaka ya kudai taarifa yoyote kutoka ndani ya chama cha siasa au kiongozi, wakati wowote hata kama taarifa hiyo ni mbinu na mikakati ya ushindi ya chama husika,  na kama asipopatiwa, basi chama au kiongozi anaweza kulipishwa faini ya kiasi cha shilingi milioni 10.

5. Kifungu cha 6B (d) kinampa mamlaka Msajili wa Vyama vya Siasa ya kusajili chama cha siasa Mtanzania mwenye miaka 18, lakini kwa mujibu wa Katiba ya mwaka 1977, Sheria ya Uchaguzi ya Mwaka 1985 na ile ya Serikali za Mitaa inamnyima haki ya kugombea nafasi ya urais, ubunge, udiwani na uongozi kwenye kijiji, mtaa au kitongoji kama mtu huyo hajafikisha miaka 40 kwa urais au miaka 21 kwa nafasi nyingine. Sheria hii inampa fursa mtu kusajili chama lakini haruhusiwi kuwa kiongozi, hii ni kinyume cha tamko la ulimwengu la haki za binadamu juu ya haki ya kuchagua na kuchaguliwa.

6. Kifungu cha 8C (2) kinampa Msajili wa Vyama vya Siasa mamlaka ya kukisimamisha chama cha siasa kwa sababu tu hakijampelekea kwa ufasaha orodha ya wanachama wake. Hivi ingekuwaje kama sheria hii ingekuwa inatumika kabla ya Maalim Seif kujiunga na ACT – Wazalendo na wanachama wa CUF Zanzibar kuamua kumfuata?

Kingefutwa ACT au CUF Lipumba? Nani angehukumiwa kwa kupeleka orodha ambayo si sahihi?  Vyama vya siasa ni taasisi ambazo zinabadilika kulingana na wakati na matukio, hivyo kufanya wanachama wake kupungua au kuongezeka kutokana na matukio husika, hivyo si sahihi kuvisimamisha vyama kwa sababu tu ya orodha ya wanachama wake.

7. Kifungu cha 8D (2) kinampa mamlaka Msajili wa Vyama vya Siasa kuamuru vyama kubadilisha katiba zao ndani ya kipindi cha miezi sita bila kujali kuwa katiba za vyama zimeweka utaratibu wa kubadilisha katiba zao na kuna hatua za kufuatwa ambazo zinaweza kuchukua muda wa zaidi ya miezi sita ili kukamilisha mchakato wa kubadilisha katiba ya chama husika. Kifungu hiki kinamfanya Msajili wa Vyama vya Siasa kuwa ndiyo mikutano mikuu ya vyama na ana mamlaka makubwa kuliko vyombo vya vyama husika na juu ya katiba za vyama.

8. Kifungu cha 8E kimepiga marufuku vikundi vya ulinzi ndani ya vyama na kama chama kikiwa na walinzi kwa ajili ya mali na viongozi wake, basi adhabu yake ni chama husika kufutwa na wanachama wake kufungwa. Huku ni kuingilia haki ya kikatiba ya kujilinda wakati ambapo sheria hii haijaweka kifungu chochote kuhusu wajibu wa serikali na vyombo vyake kutoa ulinzi kwa viongozi wa vyama na mali zao wakati wote.

9. Kifungu cha 11A (2) kimeweka masharti juu ya vyama kushirikiana kuwa ni lazima vifanye hivyo miezi mitatu kabla ya uchaguzi kufanyika, huku ni kuingilia uhuru wa vyama, kwani suala la kushirikiana linatokea kulingana na mazingira ya kisiasa ya wakati husika na hata kitendo cha kutaka vyama kupeleka kwa Msajili wa Vyama vya Siasa hati ya makubaliano ya kuungana haina mantiki yoyote zaidi ya kuingilia uhuru wa vyama husika. Aidha, kifungu kidogo (2) kinasema kuwa ili vyama vishirikiane ni lazima mikutano mikuu ya vyama hivyo ndiyo ifanye uamuzi huo. Huku ni kuingilia katiba za vyama ambazo zimeweka utaratibu, kwa mfano kwa upande wa Chadema jukumu hilo lipo kwenye mamlaka ya Baraza Kuu na si Mkutano Mkuu.

10. Kifungu cha 23(7) kimeweka sharti kuwa chama kikipata hati chafu kinyimwe ruzuku ya serikali kwa kipindi cha miezi sita. Hii ni sheria ya kibaguzi ambayo inavibagua vyama vya siasa na kuziacha taasisi nyingine za umma ambazo zinapata fedha kutokana na kodi za wananchi na ambazo hazijawekewa masharti kama hayo. Ubaguzi huu ni kinyume cha Katiba ya nchi na Bunge limevunja Katiba kwa kutunga sheria yenye ubaguzi kama hii.

Mwisho, Kifungu cha 21E kinampa mamlaka Msajili wa Vyama vya Siasa kumsimamisha uanachama wa chama cha siasa mwanachama yeyote na kumzuia kushiriki shughuli za kisiasa, huu ni ukiukwaji mkubwa wa Katiba na ni mpango wa watawala kwenda kuwasimamisha wagombea wa nafasi mbalimbali ndani ya vyama kutokugombea na jambo hili ni hatari kwa amani na ustawi wa nchi yetu.  Mathalani fikiria Msajili wa Vyama vya Siasa anamsimamisha uanachama mgombea urais wa chama chetu na kumnyima sifa za kugombea, hali itakuwaje?

Hatua tutakayochukua

Kama ilivyokuwa dhamira yetu ya awali ya kupeleka shauri mahakamani, nia na dhamira hiyo iko palepale na tunaendelea kushauriana na vyama vingine vya siasa na wadau mbalimbali njia nzuri zaidi ya kufungua shauri mahakamani mapema iwezekanavyo.

Hitimisho  

Sheria hii imekwenda kufanya shughuli za kisiasa nchini kuwa ni jinai, kwani kila kifungu cha sheria hii kimeweka adhabu ya faini, kifungo au vyote kwa pamoja kwa wanasiasa, ila Msajili wa Vyama vya Siasa na serikali na vyombo vyake, hakuna kifungu hata kimoja ambacho kinawagusa kama wakikiuka utekelezaji wa sheria hii.

John Mrema ni Mkurugenzi wa Itikadi, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema.